CHAMA CHA WABUNGE CHA KUHIFADHI NA KULINDA WANYAMAPORI CHAPELEKEWA KILIO CHA TEMBO NA FARU DODOMA.
Vitendo vya ujangili vinavyoendelea kukithiri nchini vinasababisha hatari ya kutoweka kwa wanyamapori nchini wakiwamo tembo na faru.
Profesa Davis Mwamfupe wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ametoa tahadhari hiyo bungeni mjini hapa wakati akitoa mada kwenye semina ya kuwajengea uelewa wabunge katika kulinda wanyamapori iliyoandaliwa na Chama cha Wabunge cha Kuhifadhi na Kulinda Wanyamapori.
Profesa Mwamfupe alisema kuwa hivi sasa, wanyama hao ambao walikuwa wengi katika mbuga na hifadhi mbalimbali nchini wamepungua kwa kiasi kikubwa na hivyo kuwa katika tishio la kutoweka.
Aliongeza kuwa hakuna takwimu zozote zinazoonyesha kuongezeka kwa wanyama hao bali zote zinaelezea kupungua kwa wanyama hao kutokana na vitendo vya ujangili uliokithiri nchini.
“Hali hii ndiyo iliyotupa mwamko wa kutoa elimu kuhusiana na hifadhi za wanyamapori na thamani ya wanyama hao.
Tumeona tukiwapa elimu ninyi waheshimiwa wabunge ambao ndiyo wawakilishi wa wananchi, itakuwa ni rahisi kuwaelimisha wananchi katika maeneo yenu,” alisema.
Alisema njia mojawapo ya kukabiliana na janga hilo ni kuangalia namna ya kuwapa motisha na kuwatia moyo wale ambao wamekuwa wakitoa taarifa muhimu za siri kuhusiana na matukio ya ujangili nchini.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment