Uongozi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro umemkamata mwenyeji wa mkoa wa Kigoma na mkazi wa Liti mjini hapa, Karume Habibu (22) kwa kujifanya daktari.
Daktari huyo bandia, alikamatwa na uongozi wa hospitali hiyo baada ya muuguzi mmoja aliyekuwa zamu, kumhisi hakuwa daktari wa kweli, na kuamua kutoa taarifa kwa uongozi.
Alisema wauguzi kwa kushirikiana na madaktari walifanikiwa kumdhibiti daktari feki huyo.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Francis Semwene, ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji hospitalini hapo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, timu ya madaktari 12 na watumishi wengine, walimhoji mtuhumiwa huyo na kubaini hakuwa daktari, na alionyesha vitambulisho mbalimbali ambavyo vingine alikiri kuvitumia kwa maslahi yake binafsi.
Alisema miongoni mwa vitambulisho, ni vya kurudia masomo ya kidato cha nne, na kwamba alidai alikuwa na koti jeupe la kidaktari, ili alitumie kuingia ndani ya hospitali hiyo bila kupata bugudha kutoka kwa walinzi, na aweze kuwapa huduma ndugu zake wawili aliowatambulisha kwa jina moja moja, ambao alidai walilazwa hospitalini hapo, ingawa uongozi wa hospitali haukuwa na uhakika wa ukweli wa jambo hilo.
Hata hivyo, alisema baada ya kubaini hila za daktari huyo feki, ambaye ilidaiwa kwa zaidi ya wiki mbili alikuwa akionekana hospitalini hapo, walilazimika kufikisha suala hilo polisi, na kumtia mbaroni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alikiri kushikiliwa kwa mtuhumiwa huyo, na kwamba alikutwa na vitambulisho vitatu tofauti, kikiwemo kimoja cha kurudia masomo ya kidato cha nne katika kituo cha The Great Education Centre, katika manispaa ya Morogoro, na alionekana kumaliza kidato cha nne mwaka 2012 mkoani Kigoma.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa majira ya asubuhi katika hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, akijifanya kutibu na mipango mingine feki ya kitabibu, na wanaendelea kumhoji zaidi na kuchunguza iwapo katika huduma zake aliweza kusababisha madhara yeyote. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment