Na Hamida Shariff, Morogoro.
Wakati jamii ikiwa bado haijasahau mateso aliyoyapata mtoto Nasra Mvungi na kusababisha kifo chake, tukio lingine la aina hiyo limetokea katika Kijiji cha Matongola, Tarafa ya Magole Wilaya ya Kilosa, baada ya kubainika mtoto wa miaka sita akiwa amefichwa uvunguni mwa kitanda na kufanyiwa vitendo vya kikatili na mama yake mzazi.
Wakati jamii ikiwa bado haijasahau mateso aliyoyapata mtoto Nasra Mvungi na kusababisha kifo chake, tukio lingine la aina hiyo limetokea katika Kijiji cha Matongola, Tarafa ya Magole Wilaya ya Kilosa, baada ya kubainika mtoto wa miaka sita akiwa amefichwa uvunguni mwa kitanda na kufanyiwa vitendo vya kikatili na mama yake mzazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo
alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa taarifa za mateso ya mtoto
huyo zilifikishwa Kituo cha Polisi wilayani Kilosa za saa za mchana
jana, baada ya uongozi wa kijiji na kata kutoa taarifa na tayari
mwanamke huyo amekamatwa kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Mama aliyefanya ukatili huo anafahamika kwa jina
la Sala Mazengo ambaye alimficha ndani mtoto wake aliyefahamika kwa jina
la Devota Malole na kumfanyia vitendo vya kikatili ikiwa pamoja na
kutompa chakula, wala kumfanyia usafi.
Baada ya kufichuliwa kutoka alipofichwa, mtoto
huyo alionekana kuwa dhaifu kiafya kutokana na kukosa lishe pamoja na
mazingira aliyokuwa akiishi kutoridhisha, jambo ambalo ni kosa kisheria,
pia ukiukwaji wa haki za watoto.
Inadaiwa kuwa tangu mwka 2009 Sala amekuwa
akimficha mtoto wake huyo ambaye sasa amelazwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya kupatiwa vipimo na matibabu.
Hata hivyo, mwanamke huyo alipoulizwa alidai kuwa
afya ya mtoto wake ilikuwa mbaya tangu alipozaliwa kutokana na magonjwa
ya mara kwa mara, pia hali ngumu ya maisha ilichangia kudhoofisha afya
ya mtoto huyo.
Alidai kuwa ana watoto sita, pia alikiri kumlaza
chini mtoto huyo kutokana na kuwa na kitanda kimoja, ambacho hakiwatoshi
watoto hao.
Aliongeza kuwa hata chakula amekuwa akikipata kwa shida kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa kuwa ana mtoto mwingine mdogo.
Kamanda Paulo alisema kuwa mwili wa mtoto huyo
umedhoofu kutokana na kufichwa ndani kwa muda mrefu na bado mwanamke
huyo hajaeleza sababu za kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto
huyo.
“Siwezi kutoa taarifa ya kidaktari, lakini
kutokana na afya ya mtoto yule na mazingira tuliyomkuta ni dhahiri
alikuwa akipata mateso na kufanyiwa vitendo vya ukatili. Hata hivyo,
uchunguzi zaidi tunaufanya na kwamba taratibu za kumfikisha mtuhumiwa
huyo Kituo Kikuu cha Polisi mkoani hapa zinaendelea,” alisema Kamanda
Paulo.
Alisema kuwa mpaka sasa bado haijafahamika kama
mtoto Davota ni mlemavu au la na kwamba taarifa za afya ya mtoto huyo
zitatolewa baada ya madaktari kumfanyia uchunguzi wa kina.
0 comments:
Post a Comment