Kaimu Balozi wa Libya nchini, Ismail Nwairat, amejipiga risasi kifuani na kufariki dunia, jijini Dar es Salaam, katika mazingira ya kutatanisha.
Nwairat (39), ambaye mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ameripotiwa kujipiga risasi juzi nyakati za mchana, akiwa ofisini kwake, katika jengo la Ubalozi huo, eneo la Upanga, jijini Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi limethibitisha kaimu balozi huyo kujiua kwa risasi.
MAJIRANI WAZUNGUMZA.
Baadhi ya majirani waliliambia NIPASHE jana kuwa juzi mchana, walisikia mlio wa risasi ukitokea ndani ya jengo hilo, lakini awali hawakujua kilichotokea.
Mmoja wa majirani, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema walikuja kujua baadaye kilichotokea baada ya taarifa za kifo cha kaimu balozi huyo kuanza kuzagaa eneo hilo.
NIPASHE ilifika katika jengo la ofisi za ubalozi huo jana, saa 4.30 asubuhi, lakini maofisa waliokuwapo hawakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo kwa madai kwamba, siyo wasemaji.
Mmoja wa maofisa, ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema muda ambao timu ya waandishi wa NIPASHE ilifika, msemaji wa ubalozi huo alikuwa nje ya ofisi kwa dharura.
KAULI YA JESHI LA POLISI.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, aliliambia NIPASHE jana kuwa uchunguzi wa awali wa tukio hilo unaonyesha kuwa kaimu balozi huyo alijipiga risasi upande wa kushoto wa kifua na kufariki dunia.
Hata hivyo, Senso alisema polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kujua sababu za kaimu balozi huyo kujipiga risasi.
“Hata kama amejipiga risasi ni lazima tujue kwanini alijipiga risasi,” alisema Senso, ambaye hakutaka kuingia kwa undani akisema suala linalomhusu balozi siku zote huwa ni la kidiplomasia zaidi.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), ambaye ni kiongozi wa kwanza wa serikali kulithibitishia NIPASHE kifo cha kaimu balozi huyo, alisema alijipiga risasi juzi majira ya saa 7:00 mchana akiwa ofisini kwake, katika jengo la ubalozi huo.
Alisema baada ya mlio wa risasi kusikika ndani ya ofisi hiyo, baadhi ya maofisa wa ubalozi waliokuwapo nje, walivunja mlango wa ofisi yake na walipoingia ndani walimkuta akiwa amelala chini, huku akitokwa damu nyingi.
Alisema kutokana na hali hiyo, walimchukua na kumkimbiza katika hospitali binafsi ya Ami, iliyoko Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Alisema madaktari wa hospitali hiyo walimpima na kubaini kuwa alikwishafariki dunia.
Hata hivyo, alisema hadi sasa sababu za kaimu balozi huyo kujimaliza kwa risasi bado hazijajulikana.Alisema mwili wake utasafirishwa kupelekwa nyumbani kwake, nchini Libya kwa mazishi.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, serikali itatoa kila aina ya msaada unaohitajika kufanikisha kusafirishwa kwa mwili huo kwenda nchini Libya.
KAULI YA MAMBO YA NJE.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pia ilithibitisha kifo cha kaimu balozi huyo kilichotokana na kujiua.
“Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa leo (jana) imepokea taarifa kutoka Ubalozi wa Libya hapa nchini kuwa aliyekuwa Kaimu Balozi wa Libya, Ismail Nwairat, amefariki dunia jana kwa kujipiga risasi,” ilieleza sehemu ya taarifa ya wizara hiyo jana.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kifo hicho kimetokea majira ya saa 7 mchana ofisini kwake katika jengo la Ubalozi wa Lbya.
“Inataarifiwa kuwa Nwairat alijifungia ofisini na kujifyatulia risasi kifuani upande wa kushoto. Maofisa ubalozi walivunja mlango waliposikia mlipuko wa bunduki na kumkuta Kaimu Balozi Nwairat ameanguka chini,” ilieleza taarifa hiyo Iliongeza:
“Walimkimbiza hospitali ya Ami Oysterbay, ambako alitangazwa kuwa alikwisha kufariki na polisi walithibitisha kifo hicho. Maiti imehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.”
Taarifa hiyo ilieleza kuwa ubalozi unafanya maandalizi ya kusafirisha mwili wa marehemu Nwairat kwenda nyumbani kwa mazishi na kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeuhakikishia Ubalozi wa Libya ushirikiano wake katika kipindi hiki kigumu.
Afisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Algaesha, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mwili wa Hussein ulipokelewa hospitalini hapo juzi,.“Mwili wa kaimu balozi umepokelewa hospitalini hapa juzi.
Lakini hadi sasa bado haujafanyiwa uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo chake. Ila kesho (leo) utafanyiwa uchunguzi,” alisema Algaesha. CHANZO: NIPASHE
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment