WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAIKINGIA KIFUA KAMPUNI YA UWINDAJI, YATUMIA WATOTO KUWINDA WANYAMA KINYUME CHA SHERIA NDANI YA HIFADHI YA WANYAMA TANZANIA.
Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa.
Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, (pichani) ameilipua kampuni moja ya uwindaji kwa kufanya uwindaji haramu huku ikiwa na leseni halali ya uwindaji.
Pia, Msigwa ameitupia lawama Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kuendelea kuilinda kampuni hiyo licha ya kwamba inavunja sheria za uwindaji, kutumia magari binafsi, kuwinda bila utaalamu na kutumia watoto kuwinda wanyama.
Kabla ya kuwaeleza waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, Msigwa alionyesha CD kampuni hiyo, inavyoendesha uwindaji haramu ikiwamo kujeruhi wanyama, kuuwa wanyama wa jinsi ya kike, kuchezea watoto wa Pundamilia, mtoto akiwinda na kuua ndege aina tandawala weupe na weusi na matumizi ya silaha zisizo na sauti.
Alisema licha ya kuiwasilisha Bungeni CD hiyo Mei mwaka huu, wakati akisoma maoni ya kambi rasmi ya upinzania , lakini serikali imeendelea kuwa kimya na kampuni hiyo inawinda wanyama itakavyo.
Alisema baada ya kutoa video hiyo alitarajia serikali itachukua hatua za dharura ili kunusuru uchumi kwa kuwa kampuni hiyo inaonekana kutenda uhalifu wa wazi dhidi ya wanyama, kukiuka sheria za Tanzania na kimataifa katika uwindaji.
Alisema licha ya ukiukwaji mkubwa wa sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 serikali imeshindwa kuchukua hatua jambo ambalo linadhihirisha kuwapo kwa kampuni ambazo zinamiliki vitalu vya uwindaji kwa mgongo wa wazawa huku ukweli ukiwa ni kwamba umiliki upo kwenye mikono ya wageni.
“Kutokana na ubutu wa serikali katika kusimamia rasilimali, kuzuia uwindaji holela, unaokuza ujangili na kutishia hatima ya maliasili na utalii nchini, Kampuni ya Green Miles Safaris inakiuka kifungu namba 42 cha sheria ya wanyamapori,” alifafanua.
Kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu yeyote atakayejemjeruhi mnyama atatakiwa kutumia juhudi zote kadri ya uwezo wake kumuua mnyama huyo ndani ya muda mfupi iwezekanavyo, lakini watendaji wa uwindaji huo huchukua muda mrefu mnyama kuteseka na maumivu.
Msigwa alidai kuwa katika video hiyo watendaji wa uwindaji wamekwepa kumuua mnyama waliomjeruhi na kumuacha ateseke kwa muda mrefu na kwamba kwa mujibu wa kifungu 116 (2) (a) faini ya kati ya Sh. 200,000 hadi milioni 10 itatozwa kutokana na ukiukwaji huo wa uwindaji.
Alisema pia imeruhusu wateja wake kupiga risasi wanyama hususan nyumbu wa kike, mtoto wa nyati na wengine kinyume na kifungu namba 56 inayokataza kuwinda au kuua watoto wa wanyama wowote.
Alisema pia kampuni hiyo imeruhusu utumiaji wa silaha inayojiendesha yenyewe aina ya semi-automatic shotgun na silaha zilizowekewa vifaa vya kuzinyamazisha zisitoe mlio ambazo ni haramu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Larazo Nyalandu, alithibitisha kupokea video hizo na kwamba ameunda timu maalum kutoka idara ya wanyamapori kuangalia mambo matatu ambayo ni iwapo video hiyo ni ya kweli na siyo ya kutengeneza, sheria zilizovunjwa na hatua za kuchukua. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment