Dar es Salaam. Joto la Katiba
Mpya linazidi kupanda nchini, huku baadhi ya wasomi na makundi
mbalimbali ya watu wakizidi kutilia shaka utapatikanaji wa Katiba hiyo.
Mkurugenzi wa Shule ya Sheria ya Kenya (KSL),
Profesa Patrick Lumumba na mwandishi wa habari mkongwe nchini, Jenerali
Ulimwengu wameonya kwamba kwa hali ilivyo hivi sasa hakuna Katiba Mpya
inayoweza kupatikana.
Wakizungumza katika mdahalo uliohusu mivutano ya
makundi katika mchakato wa Katiba Mpya jana jijini Dar es Salaam,
walisema kuwa CCM haikuwa na nia njema tangu mwanzo, huku Rais Jakaya
Kikwete akitajwa kushindwa kusimamia ipasavyo.
Profesa Lumumba alisema Katiba ya Tanzania imejaa
viraka na kwamba inahitajika Katiba Mpya ambayo itakidhi matakwa ya
Watanzania na karne ya 21, itakayokwenda sambamba na changamoto za
Afrika Mashariki.
Alisema nchi za Afrika Mashariki zilipata katiba
zao kwa njia ya machafuko, hivyo Tanzania lazima itafute njia sahihi
inayokubalika kwa wananchi wote bila ya kuwepo kwa kundi moja linalotaka
kuhodhi mchakato wa Katiba Mpya.
“Tanzania ina nafasi ya pekee na kihistoria
kujipatia Katiba Mpya bila vita na itakuwa ni jambo la kusikitisha ikiwa
kwa mtazamo finyu ya kivyama utanyimwa na wanasiasa ambao fikra zao si
za kukidhi matakwa ya katiba,” alisema Profesa Lumumba.
Alieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete amekiri kuwa
alifanya makosa katika kusimamia mchakato wa Katiba Mpya, hivyo
Watanzania wanapaswa wamsamehe ili mambo yaende sawa.
“Nimesikiliza hotuba za Rais (Jakaya Kikwete)
alikubali kwamba alikosea, tukumbuke Rais wa nchi hawezi akaja akapiga
magoti, cheo chake cha rais hakikubali hivyo, akisema alitoa maoni kama
mwananchi kile ambacho anasema ni kwamba nisameheni,” alisema huku
akishangiliwa na wajumbe ukumbini. Aliongeza kuwa iwapo Watanzania
watataka Rais afanye jambo la ziada kuliko hilo alilofanya watashusha
hadhi ya kiongozi huyo wa nchi.
Alisema Watanzania walipotunga sheria ya kufanya
marekebisho ya katiba walifanya dhambi mbili za asili. Alizitaja dhambi
hizo kuwa ni kuruhusu kuyataja baadhi ya mambo kwenye katiba kuwa ni
matakatifu na kuvunja tume ya mabadiliko ya katiba.
“Mkiwa mnazungumzia mambo ya katiba hakuna mambo
matakatifu yote lazima yazungumziwe. Tanzania siyo nchi ya kwanza Afrika
Mashariki kutafuta katiba ni nchi ya mwisho,” alisema huku
akishangiliwa na wajumbe wa kongamano hilo.
Akiizungumzia dhambi ya pili alisema: “Lakini
jambo ambalo halieleweki na wengi ni kwa nini Tume ya Marekebisho ya
Katiba ya Jaji Warioba (Joseph) iliyokuwa na uzoefu ikavunjwa ? Katika
mataifa yote unaihifadhi tume mpaka mwisho.”
Alisema tume hiyo ilitekeleza kazi yake kwa
kiwango kikubwa na kwamba hakuna nchi Afrika iliyowahi kukusanya maoni
kutoka kwa kila mwananchi.
Akizungumzia namna wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba linaloanza
kikao chake cha pili Jumanne mjini Dodoma wanavyotakiwa kufanya kazi
zao, alisema siku zote mjumbe ni mtu anayepeleka taarifa mahali fulani
kama ilivyo na siyo kuibadilisha.
“Hilo ndilo jambo linalotambulika na mataifa yote
na nyinyi Watanzania ndiyo mtakuwa wa kwanza kufikiri tofauti…Tume ya
Warioba imefanya mambo yenye ubora yaliyopita viwango vya kimataifa,”
alisema huku akishangiliwa kwa makofi na miluzi.
Alisema Ukawa wamefanya vizuri kujiondoa bungeni
kwa kuwa walikuwa na sababu zinazoeleweka, lakini kwa kuwa sasa ujumbe
wao umefika CCM wanaweza kurudi bungeni.
“Kama umejiondoa pindi ujumbe wako unapoeleweka unarudi bungeni ili upambanishe hoja,” alisema.
Profesa Lumumba alisema wanachama wa TLS
wanatakiwa kuchukua hatua ya kufungua kesi mahakamani kuhoji uhalali je,
katika kujadili Mamlaka ya Bunge hilo yanaishia wapi.
Jenerali Ulimwengu
Mchambuzi mkongwe wa masuala la kisiasa nchini,
Jenerali Ulimwengu alitaja sababu zilizosababisha kukwama kwa mchakato
wa Katiba Mpya ikiwa ni pamoja na CCM kutokuwa na nia ya dhati ya kupata
katiba hiyo.
Alisema vyama vya upinzani vilidhani vingeweza
kutumia mchakato wa Katiba Mpya kuingia Ikulu huku CCM nao wakidhani
iwapo katiba ingepatikana wangepoteza madaraka yao.
“Watawala walisema hatuhitaji mabadiliko, hasa
mtawala mkuu kuliko wote akasema tutakuwa na katiba mpya. Kwa hiyo
tulikuwa mahali ambapo watumishi hawataki tajiri anasema atafanya,”
alisema Ulimwengu.
Rais Mstaafu wa TLS, Francis Stolla alisema
kufungua kesi ni lazima kuwapo na mlalamikaji lakini wataona ni jinsi
gani wataweza kufungua kesi mahakamani ili mahakama itoe ufafanuzi wa
mamlaka ya Bunge hilo.
Naye Mwakilishi wa Chadema, Tundu Lissu alisema
mjadala kama huu umechelewa ulitakiwa kufanyika miaka mitatu nyuma
ambapo tungejiuliza wapi tunataka kwenda na tunataka kitu gani.
Ukawa watoa msimamo.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeendelea na msimamo wao
wa kutorejea bungeni Agosti 5 mwaka huu na nguvu zao wanazielekeza
katika vyama vyao kwenda kujipanga ili kuhakikisha harakati za kupigania
Katiba Mpya zinafanyika nje ya Bunge.
Pia, Ukawa wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kuacha
kuwa kigeugeu na awe na msimamo katika jambo hili lenye masilahi mapana
kwa kila mwananchi.
Kauli ya Ukawa unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF
na NCCR-Mageuzi inatolewa ikiwa ni siku moja kupita baada ya kuvunjika
kwa kikao cha usuluhishi kilichokuwa chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa
Nchini, Jaji Francis Mutungi.
Kikao hicho kilichofanyika Hoteli ya Sea Cliff
jijini Dar es Salaam, kilianza saa 4 asubuhi na kumalizika saa 1.30
usiku kwa Ukawa na CCM kuondoka bila kuafikiana hasa uhalali wa mamlaka
ya Bunge Maalumu la Katiba ni yapi.
Jaji Mutungi akizungumza juzi na gazeti hili
alisema hatima ya Watanzania kupata Katiba Mpya itategemea busara za
viongozi wa vyama vya siasa.
“Ninavyoona mimi, hapa hatima ya Watanzania ya
kupata Katiba Mpya itategemeana na busara za viongozi wetu wa vyama vya
siasa pekee na si kitu kingine,” alisema Jaji Mutungi.
Wakizungumza jana na waandishi wa habari kwenye
ofisi za makao makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam, viongozi wa Ukawa
walisema hawatarejea katika Bunge Maalumu la Katiba na wataendelea
kuyaheshimu maoni ya wananchi yaliyomo katika Rasimu ya Mabadiliko ya
Katiba.
“Ukawa hatuko tayari kuendelea na mazungumzo na
CCM wala kurudi katika mkutano wa Bunge Maalumu kwa kuwa kufanya hivyo
ni kusaliti maoni ya wananchi na kutumia vibaya fedha za umma na
kubariki uchakachuaji wa msingi wa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na
Tume,” alisema Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema.
Aliongeza: “Kila chama kinakwenda kujadili na
wanachama wake kupitia Kamati kuu zake kisha tutakutana ili kuona ni
hatua gani zingine tuzifuate katika kuipigania Katiba Mpya.”
Naye Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa juzi amewapotosha Watanzania na
kuendelea kuuvuruga mchakato huo kama alivyofanya wakati akilizindua
Bunge Aprili mwaka huu.
“Rais Kikwete alipewa fursa na Tume ya Katiba
kutoa maoni yake, lakini alikataa sasa kule bungeni alitoa maoni ya nini
wakati alitengewa muda na akaukataa? Na juzi katika hotuba yake
ameendelea kusisitiza kuwa alitoa maoni kama mwananchi, anauharibu
mchakato huu,” alisema Profesa Lipumba.
Aliongeza: “Rais Kikwete anafanya mchezo kama
ingekuwa ngoma ya kikwere angefanya hivyo lakini kwa jambo hili la
kitaifa anatakiwa kuwa makini sana.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
alisema katiba mpya itapatikana kwa utashi wa kisiasa na si maridhiano.
Naye Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema
marekebisho yaliyofanywa na Bunge Maalumu la Katiba Aprili 25 mwaka huu
baada ya wajumbe wa Ukawa kutoka yalikuwa ni batili.
“Mabadiliko hayo yaliingiza kanuni mpya ya 32 (6)
inayoliruhusu Bunge Maalumu kupendekeza sura mpya kwenye rasimu sasa hii
hata tukirudi CCM watataka kuibadili rasimu nzima na kuitupilia mbali
Rasimu ya Tume ya Katiba,” alisema Lissu.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment