KAMANDA MSTAAFU WA JESHI LA POLISI ANAYETAKA TANZANIA ITAWALIWE NA RAIS DIKTETA KUANZIA MWAKA 2015
Alfred Tibaigana alipokuwa kazini siku chache kabla ya kustaafu.
Muleba. Iko dhana kuwa ili Tanzania ipige hatua kimaendeleo inahitaji kiongozi anayethubutu kufanya uamuzi mgumu hasa kuwawajibisha viongozi wabadhirifu na wazembe, lakini Kamanda wa Polisi mstaafu wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Alfred Tibaigana amekwenda mbali zaidi; anataka rais dikteta.
Kamishna Tibaigana alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake Buganguzi wilayani Muleba, mkoani Kagera hivi karibuni.
Ametoa kauli hiyo wakati nchi ikijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa rais na wabunge uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka ujao, huku tayari watu mbalimbali, hasa kutoka chama tawala cha CCM wakiwa wameshaanza kujinadi.
“Mimi ningetaka rais ambaye, kwa lugha yangu na gazeti lako lilishanihoji, nikasema nataka rais ambaye atakuwa dikteta kidogo,” alisema Kamanda Tibaigana ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
“Sasa ukisema hivyo, wanasheria wenzangu watasema kumbe wewe mwanasheria mzima, tena mkongwe unasema (unataka) dikteta. Lakini mimi ninataka mtu mwenye power (nguvu) ya kukemea na kutoa amri watu wakafuata.
“Unajua hapa kuna umaskini uliokithiri wa watu, tunajitakia wenyewe. Watu hawafanyi kazi, sheria zipo, wasimamizi hawatekelezi. Kwa hiyo umaskini tunaoililia Serikali, nataka rais ambaye akiungurumisha amri kwamba kuanzia saa moja asubuhi hadi saa sita wawe shambani kwao, kila mtu atii, yaani bila ya kumwona mtendaji wa kijiji wajue rais ametoa amri.”
Alisema tafsiri ya neno hilo ni pana, lakini yeye anataka rais atakayekemea na watu wakamtii.
Tibaigana, ambaye alikuwa akijibu swali lililomtaka aeleze sifa za rais ajaye, alisema hoja yake ya kutaka rais atakayekuwa dikteta inatokana na Taifa kuwa na umaskini uliokithiri licha ya kuwa na rasilimali za kutosha.
“Kama sheria zingesimamiwa vizuri, zingetumika kuondoa changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa, ikiwa ni pamoja na kuwabana wabadhirifu kuanzia katika ngazi za halmashauri za wilaya,” alisema Tibaigana.
“Tunakabiliwa na umaskini wa kujitakia kwa kuwa sheria zipo lakini hazisimamiwi vizuri ili zifanye kazi. Watu wanataka utajiri wa haraka bila kufanya kazi. Rais mwenye nguvu anaweza kulisaidia taifa kuondokana na umaskini,” alisema Tibaigana.
Kuhusu wagombea walioanza kujitangaza kuwania urais, Tibaigana alisema hana tatizo na watu kujitangaza mapema, lakini angependa rais ajaye awe na sifa ya ziada ya kuwa dikteta.
Taifa linahitaji rais anayejisimamia katika uamuzi ambao utasababisha viongozi mbalimbali kuwajibika katika utendaji wao kuanzia ngazi ya vijiji.
Alisema wananchi wanalalamikia mambo mbalimbali ikiwamo ufujaji wa mali na rasilimali zao na kuwa taifa likipata rais imara anayeipenda nchi yake, anaweza kusimamia mabadiliko ambayo yataonekana hata kwenye maisha ya wananchi vijijini.
“Nataka rais anayeipenda nchi yake, siyo uongo wa kisiasa; ambaye atasimamia vizuri rasilimali za nchi na zikatumika kwa manufaa ya wote; atakayetoa uamuzi na kuusimamia ili yawepo mabadiliko kwenye maisha ya wananchi,” alisema.
Pia aliunga mkono kitendo cha wagombea wanaotarajiwa kuwania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu mwakani kutangaza nia yao mapema, akisema kufanya hivyo ni kuwapa fursa wananchi wawatambue na kuwajadili kama wanafaa.
“Ni vyema wanaotamani kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao, wakajitangaza mapema ili kutoa nafasi kwa wananchi na watu mbalimbali kuanzisha mijadala dhidi yao kwa nafasi walizotangaza kuwania,” alisema.
Kuhusu ubunge
Tibaigana ambaye aligombea ubunge wa Jimbo la Muleba Kusini baada ya kustaafu, lakini akashindwa katika kura za maoni ndani ya CCM na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema hana mpango wa kurudi tena ulingoni kugombea ubunge.
“Wakati naomba kura ili niteuliwe na chama changu cha CCM kugombea ubunge, niliwaambia wananchi kuwa wanipe miaka mitano tu. Sasa, kwa kuwa muda huo umeshapita, nawaachia wengine,” alisema Tibaigana.
Alisema kuwa kama angetaka angeweza kugombea kama mgombea binafsi bila kupitia chama chochote kama suala hilo lingepitishwa katika Katiba Mpya, lakini ameamua kupumzika.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment