KATIBA MPYA KUPIGIWA KURA YA KUIKUBALI AMA KUIKATAA NA WAJUMBE MAALUMU LA KATIBA BUNGENI DODOMA.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge akichangia baada ya kupewa nafasi kuhitimisha mjadala wa bunge hilo.
UPIGAJI kura kupata Katiba Inayopendekezwa, unatarajiwa kuanza leo ambapo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walio bungeni na nje ya Bunge, watapiga kura ya kuikubali, au kuikataa kwa njia ya wazi na siri.
Kwa wajumbe watakaokuwa nje ya ukumbi huo, wakiwemo watakaokuwa nje ya nchi, tayari utaratibu wa kupiga kura popote walipo kwa njia ya nukushi (faksi) na intaneti, umeshaandaliwa.
Akizungumza bungeni juzi wakati wa kuhitimisha mjadala wa mapendekezo ya mabadiliko ya Rasimu katika Katiba Inayopendekezwa, aliyekuwa Mwenyekiti Kamati ya Uandishi wa Bunge, Andrew Chenge alisema mjumbe wa Kamati hiyo, Dk Tulia Akson ndiye atakayewasilisha marekebisho yaliyofanywa katika rasimu hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, aliagiza kamati zote 12 za bunge hilo kukutana jana saa nane mchana bila kuwapa ajenda ya kikao hicho, ambacho alisema wenyeviti wa kamati hizo watakuwa nayo.
Jana gazeti hili lilimtafuta Katibu wa Bunge, Yahya Khamis Hamad kujua idadi ya watu watakaopiga kura nje ya ukumbi wa Bunge, watakaokuwa nje ya nchi na vituo vyao, lakini simu yake ilikuwa imezimwa.
Hata hivyo, taarifa kutoka miongoni mwa watendaji wa bunge hilo zilizofikia gazeti hili, zilieleza kuwa mpaka jana mchana kazi ya kuhakiki wajumbe ambao hawatakuwepo katika Ukumbi wa Bunge, ilikuwa ikiendelea.
Tayari Ofisi ya Bunge la Katiba, ilitoa taarifa kuwa itamtuma ofisa wake kwenda Makka, Saudi Arabia kusimamia upigaji kura kupitisha Katiba Inayopendekezwa kwa wajumbe wa Bunge waliokwenda Hijja ambao wanatarajiwa kuwa zaidi ya wanane.
Mbali na Makka, pia mabalozi wa Tanzania nchi za nje, wanatarajiwa kuwa wasimamizi wa kura zitakazopigwa kwa faksi na intaneti na baada ya hapo zitawasilishwa katika ukumbi wa Bunge kwa ajili ya kujumlishwa.
Theluthi mbili
Akizungumza juzi baada ya kupewa nafasi kutoa neno la kuunganisha wajumbe, mjumbe mzee kuliko wote, Kingunge Ngombale Mwiru aliwataka wajumbe wasiangalie mambo binafsi ambayo hayakuwekwa katika Katiba Inayopendekezwa, bali waangalie matakwa ya nchi.
“Wananchi wanataka Katiba, tusije tukazuia Katiba bora kwa sababu tunataka kila kitu kiingie katika Katiba. Nataka tufikirie nchi yetu na hatima yake. “Ili Katiba hii ipite, lazima ipate theluthi mbili ya wajumbe wa Tanzania Bara na theluthi mbili Zanzibar na hapa maana yake ni kura…kitendo cha kusema mh, tunaweza kukwama na mkwamo huo hauna tija kwa wafanyakazi, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo na wanawake,” alisema.
Alisisitiza kuwa yaliyowekwa katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, yanatosha kufanya Tanzania ipige hatua mpya katika miaka hamsini ijayo.
Ubora wa Katiba
Akielezea ubora wa Katiba inayotakiwa na wananchi, Kingunge alisema wajumbe wote kwanza watambue kuteuliwa kwao na makundi yao kwa upande mmoja na Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, kwa upande mwingine, hatimaye wametumwa na wananchi, ambao wanataka Katiba mpya.
Katiba hiyo ili iwe bora kwa mujibu wa Kingunge, inatakiwa iimarishe mafanikio ya miaka 50 ya Tanzania, na ili kufanikisha hilo Bunge hilo lilikataa muundo ambao ulikuwa ukielekea kusambaratisha nchi.
Kigezo cha pili cha Katiba bora, Kingunge alisema ni uwezo wake wa kuondoa kero za wananchi na kutoa mfano wa uamuzi wa Bunge Maalumu la Katiba, kurudisha nafasi ya Rais wa Zanzibar, kuwa Makamu wa Pili wa Rais.
“Uamuzi wetu wa nyuma (kumuondoa Rais wa Zanzibar katika nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) ulikuwa na upungufu…tuliangalia zaidi ujio wa vyama vingi na kusahau walioungana walikuwa pande mbili za Zanzibar na Tanganyika,” alisema na kusisitiza kwa mabadiliko hayo, Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ni bora.
Eneo jingine la Katiba bora kwa mujibu wa Kingunge, ni Katiba husika kuingiza mambo mapya ambapo kwa sasa Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, imeimarisha nafasi ya wananchi katika nchi.
“Ndio maana tunazungumzia haki kwa mara ya kwanza ya wakulima, wafugaji, wachimbaji wadogo, wanawake, vijana, walemavu na makundi mengine,” alisema.
Alisema baada ya mkutano huo wa Bunge Maalumu la Katiba, Tanzania haitakuwa kama ilivyokuwa huko nyuma, kwa kuwa makundi yote ya jamii, yamekutana na kufanya uamuzi.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment