KINANA ASABABISHA MBUNGE, DIWANI KUPATA AIBU BAADA YA KUUMBULIWA NA WANANCHI KATIKA MKUTANO WA HADHARA TANGA.
MBUNGE wa Korogwe Mjini, Yusuf Nasir na Diwani wa kata ya Manundu, Robert Bago juzi walionja joto ya uongozi baada ya kuumbuliwa na wananchi kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
Walikumbwa na kadhia hiyo baada ya Kinana kuruhusu wananchi kuuliza maswali kuhusu masuala mbalimbali ya maisha yao.
Miongoni mwa wananchi waliosimama, wengi walimsifia Mkuu wa Wilaya, Mrisho Gambo kwa kufanya kazi kwa bidii ya kuhudumia wananchi lakini kwa upande wa mbunge na diwani, walidai wanashindwa kuwajibika.
Wa kwanza kuchangia alikuwa Ibrahim Abirah mkazi wa Korogwe aliyemwambia Kinana kwamba mbunge na diwani hawana uhusiano mzuri na wananchi na kwamba kazi nyingi zinafanywa na mkuu wa wilaya.
“Kuna tatizo katika jimbo hili, kwanza mbunge hana uhusiano mzuri na wananchi, na ndio maana kazi ambazo zinatakiwa kufanywa na mbunge na madiwani zinafanywa na Mkuu wa Wilaya, ambaye amefanya kazi nyingi sana za kutatua kero za wananchi,” alisema na kushangiliwa na wananchi kwenye mkutano huo.
Abirah alisema Halmashauri ya Mji imekuwa ikikusanya kodi kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato, lakini fedha hizo hazitumiki kuboresha miundombinu.
Alitoa mfano kwamba zipo barabara nyingi ambazo zinajengwa chini ya viwango. Kinana alimsimamisha Diwani wa Kata ya Manundu, Robert Bago na kumtaka atoe maelezo ya barabara kujengwa chini ya kiwango.
Bago alisema barabara hizo zina ubora unaotakiwa kwani baada ya kujenga lazima zikaguliwe na maofisa wa Wakala wa Barabara (Tanrods) Mkoa wa Tanga na kwamba pia madiwani hukagua.
“Kuharibika kwa barabara kulitokana na mvua kubwa na hasa kukosekana kwa mifereji katika barabara hizo na kuwa barabara nyingi ni nzuri na ziko katika kiwango kizuri,” alisema Bago na kupingwa na wananchi waliokuwa wakizomea.
Alipotakiwa kujibu hoja ya kujenga banda la kupumzikia abiria ambalo pia ni miongoni mwa mambo yaliyolalamikiwa, Bago alisema awali kabla ya kugawanywa kuwa halmashauri ya mji, stendi hiyo ilikuwa na banda la kumpuzikia ambalo liligawanywa na kuwa maduka, utaratibu uliofanyika kisheria.
“Ni kweli hoja ipo, kulikuwa na banda la jumuiya ya wazazi ambalo liligawanywa kuwa vibanda vya biashara,” alisema lakini hata kabla ya kumalizia maelezo yake, alikatishwa na zomeazomea kutoka kwa wananchi.
Kinana alihoji sababu za viongozi kuamua kugawana mabanda ambayo kimsingi yalikwa mali ya umma.
Badala ya kutoa ufafanuzi wa swali la Kinana, Diwani huyo alibadili kauli yake na kusema mabanda yalikuwa ya serikali jambo ambalo lilimfanya Kinana kuhoji iweje mali ya serikali watu wayagawane.
“Watagawanaje mali ya serikali? Huo ni wizi, huwezi kuchukua mali ya umma na kusema una sheria. Hili ni tatizo la kuchagua viongozi wezi. Mali ya umma ni ya Wanakorogwe wote, hamuwezi kukaa na kugawana, tungekuwa na uwezo tungewanyang’anya yote,” alisema Kinana, kauli ambayo ililipua vifijo kutoka kwa wananchi.
Wakati huo huo, Mkuu huyo wa Wilaya ya Korogwe amewalipua madiwani mbele ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana na kusema hawawajibiki.
Alisema badala ya kusimamia watendaji wa halmashauri, wamekuwa wakiwaunga mkono hasa wanapofanya mambo ambayo hayasaidii kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya wilaya hiyo, Gambo alisema madiwani wengi wanachojali ni kulipwa posho na si kusimamia miradi ya maendeleo ipasavyo.
Alitoa mfano wa suala la walimu walioajiriwa mwaka 2009 ambao hawajapandishwa madaraja hadi hivi sasa, na kusema pamoja na kuwapo tatizo hilo, madiwani wamekuwa mstari wa mbele kumtetea mtendaji wa halmashauri kutokana na uzembe huo wakidai kuwa alisahau.
“Unaweza ukasahau mtu mmoja au wawili, lakini walimu wote, haiwezekani. Pamoja na Aggrey Mwanri (Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) kuja na kupewa malalamiko hayo, aliagiza waliokosea wawajibishwe, lakini waliposikia wewe (Kinana) unakuja ndiyo juzi wamempa barua ya onyo Ofisa Utumishi,” alisema.
Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, ni vema ikaundwa tume ya kwenda kushawishi Tamisemi ili walimu hao walipwe malimbikizo ya malipo wanayostahili kutokana na kupandishwa madaraja, ingawa kosa hilo si la Tamisemi bali halmashauri.
Aidha, Gambo alisema kutokana na uamuzi wa madiwani, wamekuwa wakichangia malumbano na wananchi ikiwamo na wanaofanya biashara za boda boda ambao kabla hajaingilia kati walikuwa wakisumbuliwa na kukamatwa na polisi.
“Tulikaa na watu wa bodaboda na polisi tukazungumza na sasa watu wanafanya shughuli zao kwa raha.
Pia walikuwa wanalipa ushuru halmashauri, tukasema hilo haliwezekani kwani kazi ya serikali ni kutengeneza mazingira ya watu kujiajiri na sio kuwakamua. Tukafuta ushuru wa boda boda,” alisema.
Alisema pia madiwani waliwaongeza kiwango cha ushuru wafanyabiashara wa soko la Manundu kutoka Sh 2,000 hadi Sh 20,000 kwa mwezi ikiwa ni sawa na asilimia 1,000 jambo ambalo lilisababisha wananchi kugomea kulipa ushuru huo kwa mwaka mmoja.
Alisema kwa mwaka, halmashauri haikukusanya ushuru kwa mwaka mmoja kutokana wafanyabiashara hao kufungua kesi mahakamani ya kupinga ongezeko la ushuru wa asilimia 1,000.
Aidha, amelalamikia kitendo cha halmashauri kutoza ushuru wa Sh 50, 000 kwa wafanyabiashara katika soko la Saba Saba wakati Sh 10,000 ndizo hupelekwa halmashauri na Sh 40,000 kubakia.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment