Juma Nkamia, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Serikali imesema haina mpango wa kuvifungia vyombo vya habari yakiwamo magazeti badala yake itaendelea kuvionya vinavyokiuka maadili.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, alisema hayo jana kufuatia gazeti la NIPASHE kuandikiwa barua na ofisi ya Msajili wa Magazeti, kutaka lijieleze baada ya kuchapicha habari kuhusu Bunge la Katiba jinsi linavyotumia mabilioni ya fedha.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC akiwa mjini Dodoma, alisema siyo nia ya serikali kuyafungia magazeti isipokuwa yanapokiuka taratibu yataonywa.
Hata hivyo, Nkamia alikaririwa hivi karibuni akisema serikali inajiandaa kuyachukulia hatua kali baadhi ya magazeti kwa madai kwamba yamekiuka maadili na kutishia usalama wa nchi,
Nkamia, alikaririwa kuyasema hayo aliposhiriki hafla ya uzinduzi wa nembo mpya ya kituo cha Redio Tripple A cha jijini Arusha, na kuwa utekelezaji wa azma hiyo hautajali mmiliki wa chombo husika.
Sababu iliyodaiwa kutolewa na Nkamia dhidi ya magazeti hayo ambayo hata hivyo hakuyataja, ni kwamba kuandika habari za uchochezi.
Lakini katika mahojiano ya jana, Nkamia akasema “siyo dhamira ya serikali kuyafungia magazeti, magazeti haya yameajiri vijana wengi ambao hawana kazi, lakini yanapokiuka utaratibu tunaitana tunarekebishana tu, sidhani kama serikali itafanya hivyo,” alisema.
Alisema habari iliyochapishwa na NIPASHE kwamba fedha zinazotumika katika Bunge la Katiba zinaweza kupangwa kutoka Dar es Salaam hadi Bukoba kimsingi halikuwa jambo zuri.
Hivi karibuni serikali ilimwandikia barua Mhariri Mtendaji wa NIPASHE kumtaka ajieleze kuhusiana na habari zilizochapishwa Septemba 15, mwaka huu kuhusu Bunge la Katiba.
Katika barua hiyo ya Septemba 16, mwaka huu kutoka Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, iliyotiwa saini na Raphael Hokororo, kwa niaba ya Msajili wa Magazeti ilieleza kuwa gazeti hilo lilichapisha habari za uchochezi ambazo zinajenga hisia mbaya kwa wananchi juu ya serikali yao kuhusu bunge hilo.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment