Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akihutubia katika mkutano mkubwa wa hadhara uliohudhuria na maelfu ya wananchi
katika uwanja wa shule ya msingi Mwaka mjini Tunduma wilayani Momba
mkoani Mbeya, hivi karibuni.
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesema vyama vya upinzani nchini vimeshindwa kufanya kazi za siasa badala yake vimegeuka kuwa vya wanaharakati. Aidha ametaka maandamano yanayohamasishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yapuuzwe kwa kile alichosema ni biashara ya kuuza picha za vurugu nje ya nchi kwa ajili ya kupata misaada kutoka mataifa makubwa.
Nape alisema hayo jana Korogwe Vijijini wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika mji mdogo wa Mombo huku katika baadhi ya maeneo nchini, jana polisi wakilazimika kutumia mabomu ya machozi kudhibiti maandamano baada ya wafuasi wa chama hicho kukaidi.
Katika mkutano huo ambao ni sehemu ya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana mkoani Tanga, Nape alisema vyama vya upinzani ni wanaharakati ambao kazi yao ni kutengeneza vitu na matukio ya ajabu waendelee kupata fedha nje ya nchi wafanye mambo yao.
“Hata kama yako matatizo ndani ya CCM, hakuna kitu kilicho kamili. Lakini (CCM) bado ni chama pekee cha siasa kilichobaki hasa kutokana na vyama vingine kuwa wanaharakati.”
Maandamano Alisema kwa muda mrefu kumekuwepo maswali juu ya kile ambacho Chadema kinapata kwenye maandamano ambayo mwisho wake huishia wananchi hasa vijana kupoteza maisha .
"Maandamano ni haki iliyopo kwenye katiba, lengo lake likiwa wakati mwingine kushinikiza jambo fulani lenye maslahi kwa walio wengi kufanyika.
“Maandamano yenyewe yanayoruhusiwa na Katiba yana utaratibu wake na sheria za kufuata kabla ya kuandamana, lakini toka Chadema wameanzisha utaratibu wa maandamano wamefanikiwa kubadili nini zaidi ya kupoteza maisha ya watanzania wasiokuwa na hatia,” alihoji.
Nape alisema alitegemea maazimio ya mkutano mkuu wa Chadema yangejikita kwenye mambo ya maendeleo hasa umoja na mshikamano tofauti na azimio kuu la kufanya maandamano nchi nzima bila kikomo.
“Lakini sasa tunajua siri ya maandamano yao, hali ya chama chao mbaya sana, kisiasa na kiuchumi. Katika kujaribu kutatua tatizo hilo wakabuni vurugu na fujo kupitia maandamano.
“Picha za maandamano hayo watazipeleka nje ya nchi ili kuombea misaada ya pesa kwa kisingizio cha kupambana kujenga demokrasia kana kwamba nchini hakuna demokrasia na utawala bora," alisema Nape.
Alisema uzoefu unaonesha maandamano yote yaliyoandaliwa na chama hicho, yamekuwa yakisababisha uharibifu wa mali na upotevu wa maisha ya watanzania hususani katika mikoa ya Arusha, Iringa, Singida, Morogoro, Mbeya na Mwanza.
"Ndugu zangu huwezi kujenga umaarufu wa chama kwa kutumia damu za watu,” Nape alisema na kuasa vijana na makundi mengine kuepuka maandamano hayo.
Aliendelea kusema, “Kisa cha kuandamana ni kutaka waonekane wanakamatwa na polisi, ndio maana wanapiga picha na kuwapelekea watu wao Ulaya, ili wawaletee fedha waendelee kushiba kwenye matumbo yao.
“…maana polisi wanataka mwenyekiti atoe maelezo wanakwenda kujazana kwa sababu wanajua kuwa polisi hawatawaruhusu kuingia, polisi wanapowazuia, wanaendelea kuwapiga picha,” alisema.
Kwa mujibu wa Nape, sera ya vyama vya upinzani imegeuka ya kugawa nchi na wananchi wake badala ya kushindana kwa sera na mipango ya maendeleo.
Katika mkutano mkuu wa Chadema wa hivi karibuni, azimio kuu lililotangazwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe lilikuwa ni kufanya maandamano nchi nzima bila kikomo kushinikiza bunge la katiba kusitishwa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment