BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SAMWEL SITTA AWALAANI CHADEMA KWA KUWEKA NAMBA YA SIMU KATIKA MTANDAO, APOKEA SMS 50 ZA MATUSI NA VITISHO

Samuel Sitta.

MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, amesema amekuwa akitishwa kupitia simu yake ya mkononi na kutaka baadhi ya vyombo vya habari na watu wanaomchukia, kutenganisha chuki hizo na Bunge Maalumu la Katiba.
Akizungumza bungeni jana, Sitta alisema kwa siku anapokea ujumbe mfupi wa simu (SMS) 50 tofauti, wenye matusi jambo alilosema ni baada ya Chadema kuweka simu zake katika mtandao.

“Chadema wameweka simu zangu katika mtandao na kila siku napokea sms zaidi ya 50 za matusi, lakini nipo vizuri tu…haya ni mapambano na tutaendelea kupambana,” alisema Sitta.

Akitamba kwamba hana hofu na mapambano, aliwataka watu na vyombo vya habari vinavyomchukia, kuacha kuhusisha chuki zake na Bunge Maalumu la Katiba, bali wakiache chombo hicho waendelee na yeye binafsi.

Alieleza kushangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kupotosha habari kuhusu hukumu ya Mahakama Kuu, kuhusu uwezo wa Bunge Maalumu la Katiba kubadilisha vifungu vya Rasimu ya Katiba Mpya, iliyowasilishwa Bungeni na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, kusoma hukumu hiyo kwa wajumbe akisema baadhi ya vyombo vya habari kwa makusudi vimepotosha.

Pamoja na mambo mengine, hukumu hiyo iliweka wazi kuwa Bunge hilo lina haki ya kuboresha na kubadilisha rasimu hiyo na Mahakama haiwezi kuweka kiwango cha mabadiliko au uboreshaji huo, kwa kuwa mchakato huo ni wa kisiasa kuliko ilivyo wa kisheria.

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), linaloundwa na vyama vya siasa vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi, walisusa kushiriki bunge hilo kwa madai halina mamlaka ya kubadili baadhi ya vipengele vya rasimu hiyo.

Ukawa yenye wanasheria wazoefu, wamekuwa wakidai kwa wananchi kuwa Rasimu ya Pili ya Katiba, ina moyo ambao ni muundo wa muungano wa serikali tatu ambao kwa mtazamo wao, haupaswi kubadilishwa na Bunge Maalumu la Katiba.

Madai hayo yalichukuliwa na Mwandishi wa Habari Mwandamizi, Saed Kubenea, aliyefungua kesi katika Mahakama Kuu, kuhoji ukomo wa uwezo wa Bunge Maalumu la Katiba, katika kubadili rasimu hiyo.

Hii ni mara ya pili kwa viongozi na wajumbe kulalamikia vitisho, ambapo juzi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alikemea baadhi ya watu aliosema walianza kutoa vitisho kwa baadhi ya wajumbe wa Bunge kutoka Zanzibar.

Wajumbe hao wamedaiwa kuwa ni wasaliti jambo ambalo Balozi Seif alihoji akitaka abainishwe msaliti kati ya waliopewa kazi ya wananchi wakaacha kuifanya, wakatoka nje kwa kile alichosema walikwenda kupiga porojo.

Hata hivyo, Balozi Seif alisema vyombo vya dola vinafuatilia suala hilo na vitatoa ulinzi kwa wajumbe hao kutokana na vitisho hivyo.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: