BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BUNGE KUFUMUA SHERIA 33 IKIWEMO ILE YA BODI YA MIKOPO KATIKA VIKAO VYA BUNGE LA MWAKA 2014.


KAMATI ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, imepokea Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2014, unaopendekeza kuzifanyia marekebisho sheria 33, ambao pia utawasilishwa katika vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza Novemba 4, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Ngeleja, alisema kati ya sheria hizo 33, imo Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Sura Namba 370 inayopendekeza kuongeza wigo wa wanafunzi kupatiwa mikopo ya elimu ya juu.

“Ikumbukwe haya bado ni mapendekezo, tunatarajia kukutana na wadau kesho (leo) kwa ajili ya kuzijadili sheria hizi, lakini moja ya mapendelezo yaliyopo kwenye sheria hii ya mikopo ni pamoja na kuwajumuisha wanafunzi waliomaliza chuo wa Sheria wanaokwenda shule ya Sheria nao kupatiwa mikopo,” alisema Ngeleja.

Aidha, alisema katika sheria hiyo pia kipo kipengele kinachopendekeza walimu wanaosomea masomo ya sayansi nao kuingizwa kwenye utaratibu wa wanafunzi wanaotakiwa kupatiwa mikopo hiyo.

Alisema pia muswada huo umejumuisha Sheria ya Mbegu sura namba 308 iliyoongezewa makali kwa kampuni ambazo zinasambaza mbegu kwa wakulima kuhakikisha zinasambaza mbegu zenye viwango vinginevyo adhabu kali iliyoongezwa ya faini ya kuanzia Sh milioni 100 hadi 500 itawakabili.

Alisema kwa sasa takribani Watanzania asilimia 75 wanaishi vijijini na wanajishughulisha na kilimo lakini wengi wao wamejikuta wakipata matatizo katika eneo la mbegu kutokana na sheria zilizopo kushindwa kuzibana kampuni zinazozalisha mbegu.

Sheria nyingine zilizopo kwenye muswada huo ni pamoja na Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa mazingira sura namba 272 na Sheria ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi sura namba 179.

Aidha, Ngeleja alizitaja sheria nyingine 27 ambazo zote zina pendekezo moja lililofanana linalotaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushirikishwa kwenye mashauri au kesi zinazohusisha mamlaka au mashirika yanayotajwa katika sheria hizo.

Alitaja sheria hizo kuwa ni Sheria ya Shirika la ndege Tanzania sura namba 205, Sheria ya Benki Kuu sura namba 197, Sheria ya Bodi ya korosho Tanzania sura namba 203, Sheria ya wakala wa Serikali sura namba 254, Sheria ya Usafiri wa Anga sura namba 80 na Sheria Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji sura namba 14.

Nyingine ni Sheria ya Tume ya Ushindani sura namba 285, Sheria ya Bahati Nasibu sura namba 41, Sheria ya Mfuko wa Mafao ya Uzeeni sura namba 407, Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya sura namba 395 na Sheria ya Shirika la Nyumba la Taifa sura namba 295.

Muswada huo unajumuisha Sheria ya Mbuga za Wanyama sura namba 282, Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii sura namba 50, Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro sura namba 284, Sheria ya Mfuko wa Mafao ya Uzeeni PPF sura namba 373 na Sheria ya Bandari sura namba 166.

Nyingine ni Sheria ya Mfuko wa Uzeeni kwa watumishi wa umma sura namba 371, Sheria ya Wakala wa Nishati Vijijini sura namba 321, Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii sura namba 135, Sheria ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu sura namba 413 na Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano namba 172.

Sheria ya Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi sura namba 219, Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania sura namba 399, Sheria ya Bodi ya Utalii Tanzania sura namba 364, Sheria ya Chai namba 275 na Sheria ya Madaraka na Majukumu ya Msajili wa Hazina sura namba 370.

Alisema sheria hizo zote zimependekeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ihusishwe katika masuala yote ya kisheria kutokana na mashirika hayo mengi yao Serikali ina umiliki wa asilimia kubwa hivyo ni vyema kulinda maslahi ya taifa.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: