BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

FURAHA YA KUPITA KWA RASIMU YA KATIBA, UKUMBI WA BUNGE WAGEUZWA UKUMBI WA DISKO DODOMA


KATIBA Inayopendekezwa kwa wananchi, imepatikana jana na kukamilisha sehemu kubwa ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba, ulioanzia katika ukusanyaji wa maoni ya wananchi. Jumatano ijayo, Oktoba 8, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, anatarajiwa kukabidhi katiba hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mjini Dodoma.

Hofu ya kutopatikana kura za kutosha za wajumbe kutoka Zanzibar, iliyokuwepo kwa muda mrefu tangu wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walipotoka bungeni, ilitoweka na kufanya wajumbe kujisahau na kuanza kushangilia.

Kabla ya kuondoka kwa hofu hiyo, Naibu Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Dk Thomas Kashililah, alianza kusoma idadi ya kura zilizopigwa kutoka Zanzibar kuamua kupatikana kwa Katiba hiyo, ambazo zilizidisha hofu hiyo, baada ya baadhi ya wajumbe kupiga kura za wazi za Hapana.

Dk Kashililah alianza kutaja idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka Zanzibar wakiwemo wa Ukawa waliosusa bunge hilo, ambao kura zao zilihesabiwa kuwa ni Hapana ambao jumla yao ni 219.

Kwa mujibu wa idadi hiyo, theluthi mbili ya kura hizo kutoka Zanzibar ambazo ndio zilizokuwa zikihofiwa zaidi kufanya uamuzi, zilipaswa kuwa kura 146.

Theluthi mbili Akitangaza matokeo hayo, Dk Kashililah alisema katika kura za wazi kutoka Zanzibar katika kila ibara, kura za juu kwa ibara moja zilikuwa 109 huku kura za chini zikiwa 106, ambazo hazikutosha kutimiza masharti ya theluthi mbili.

Kura za wazi za Hapana kwa mujibu wa Dk Kashililah, kura za juu zilizokataa ni nane huku za chini kukataa ibara za Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, zikiwa kura tano.

Katika mchanganuo wa kura hizo, kura za siri ndizo zilizookoa jahazi, ambapo ibara iliyopigiwa kura chache zaidi za siri za Ndio ilipata kura 38 na ibara zilizopata kura za juu zilipata kura 39.

Kura za siri za Hapana zikiwa kura moja moja na katika ibara chache mno. Baada ya kutangaza matokeo ya kura hizo za wazi na za siri kwa upande wa Hapana na Ndiyo, ibara zote za Rasimu ya Katiba zilipata kura za chini za 146 na kadirio la juu la kura 148 na kuibua shangwe kubwa, kabla hata ya kura kutoka Tanzania bara kutangazwa.

Baada ya Dk Kashililah kumaliza kutangaza kura za Zanzibar, wajumbe wa pande zote za Zanzibar na Tanzania Bara walijikuta wakiwasha vipaza sauti na kusema “Mapinduziiii” huku wengine wakiitikia “Daima!” Salamu hiyo ilivyoanza kufifia, kuliibuka nyimbo mbalimbali kutoka kona mbalimbali za ukumbi wa Bunge, ambapo baadhi waliimba;“ Sisi tumekomboka, tutalinda mapinduzi kwa niaba ya ndugu zetu waliopotea na hiyo ndiyo imani ya nchi yetu”.

Wengine waliimba kuwa wao hawatarudi nyuma, daima watapigania taifa lao mpaka mwisho, huku wajumbe kutoka Zanzibar wakionekana kufahamu zaidi nyimbo hizo, kuliko wajumbe kutoka Tanzania Bara, waliokuwa wakiwasindikiza.

Katibu aingilia kati Hali hiyo ilimlazimu Naibu Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Dk Kashiliah kuomba wajumbe watulie, huku Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, akijikuta amekaa kimya bila kukemea wajumbe waliokuwa wakicheza na wengine waliokuwa wamehama katika viti vyao kwenda kupongezana.

Dk Kashililah alizidiwa, akajikuta amekaa kimya na kuachia wajumbe waendelee kupongezana na kucheza katika ukumbi wa Bunge, huku wengine wakienda kumwamsha Sitta na kumpongeza katika kiti chake.

Baadaye Sitta aliingilia kati na kutaka kuwanyamazisha, ambapo wajumbe walirejea katika viti vyao, lakini kabla ya kuanza kuzungumza, mjumbe mmoja alianzisha wimbo wa ‘Tanzania Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote’.

Kitendo cha kuibuliwa kwa wimbo huo, kiliamsha wajumbe ambao walionekana kuwa wameshaanza kumsikiliza Mwenyekiti kwa kutulia, wakaanza kuimba wimbo huo na kusababisha pia Mwenyekiti kuungana nao kuimba wimbo huo.

Sherehe zasitishwa Baada ya kumalizika kwa ubeti mmoja wa wimbo wa Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote, wajumbe walikaa na kutulia.

Kutulia kwa wajumbe, kulisababisha Sitta atoe tangazo kwamba wajumbe wote wamevunja kanuni, na kuongeza kuwa hali hiyo imefanyika kwa kuwa hata Mwenyekiti, alijikuta akivumilia.

Alipomaliza kutoa tangazo hilo, Sitta aliruhusu kura za Tanzania Bara zisomwe ambapo kati ya wajumbe wote wa Tanzania Bara 411 wakiwemo wa Ukawa, wajumbe 335 walipiga kura. Kwa mujibu wa Dk Kashililah, kila ibara ilipata wastani wa kura 331 mpaka 334, na hivyo kuzidi theluthi mbili iliyokuwa ikihitajika ya 274.

Kumalizika kwa tangazo hilo, kuliibua shangwe upya ukumbini hapo, ambapo wajumbe walianza kuimba wimbo mwingine wa “Tazama ramani utaona nchi nzuri, yenye mito na mabonde mengi ya nafaka.”

Wengine waliimba “Wanaumia wanaumia, Ukawa wanataka nchi na nchi yetu hatuitoi, huku wengine wakiimba “Mpeni raha Mwenyekiti mpeni raha”, na kuitikiwa “ayeeee!’ Na wengine wakisema ‘ma CUF wanataka nchi na nchi yetu hatutoi.”

Wajumbe waliendelea kupongezana, ikiwemo kutoka kwenye viti vyao na kwenda kwa Mwenyekiti wa Bunge hilo na katika viti vya viongozi wa juu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idi.

Tamko la Katiba Inayopendekezwa Baada ya kutulia kwa hali hiyo, Mwenyekiti Sitta alisimama na kusema;

“ Mimi Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, leo tarehe mbili, mwezi wa kumi mwaka 2014, natangaza kwamba Bunge Maalumu la Katiba, kwa kura zinazostahili limepitisha Katiba Inayopendekezwa”. Sitta pia alitangaza majina ya mawakala walioteuliwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kwenda kushuhudia kazi ya kuhesabu kura za maoni.

Wajumbe hao ni Marina Joel Thomas, Suzan Peter Kunambi, Charles Mwijage, Amina Nassor Makilagi, Waziri Rajab Salum, Idrissa Kitwana Mustafa, Paul Christian Makonda na Muhmmad Amour Chomboh.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: