KASI YA MAAMBUKIZI YA VIRISI VYA EBOLA SASA YAITISHA DUNIA, WATU WATANO WAAMBUKIZWA NDANI YA SAA MOJA NCHINI SIERRA LEONE.
SHIRIKA la Msaada la Save the Children limeonya kuwa kiwango cha maambukizi kilichopo sasa nchini Sierra Leone, kinamaanisha kuwa nchi hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa na tiba.
Shirika hilo, limebainisha kuwa kwa sasa nchini humo kiwango cha maambukizi kimefikia watu watano hupata maambukizi ya ugonjwa huo ndani ya saa moja.
Limesema hadi sasa kuna wagonjwa wapya 765 wa ugonjwa huo wa ebola walioripotiwa katika nchi hiyo, huku kukiwa na vitanda 327 pekee vilivyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa ugonjwa huo.
Wataalamu na wanasiasa wanatarajiwa kukutana jijini London nchini Uingereza kwa ajili ya majadiliano yatakayohusisha nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kujadili namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Hadi sasa ugonjwa huo hatari kuwahi kutokea duniani, umeua watu takribani 3,338, huku katika nchi za Sierra Leone, Liberia na Guinea kumeripotiwa kuwa na wagonjwa wenye maambukizi ya ugonjwa huo 7,178.
Shirika hilo la Save the Children, limebainisha kuwa ugonjwa huo unasambaa kwa kasi ya ajabu nchini Sierra Leone huku idadi ya wagonjwa ikizidi kuongezeka mara mbili ndani ya wiki chache.
Shirika hilo pia lilibainisha kuwa wakati mamlaka za afua zikijaribu kudhibiti ugonjwa huo katika eneo moja, hali katika maeneo mengine nchini humo inazidi kuwa mbaya.
Aidha Save the Children limesema hadi sasa ukubwa wa tatizo la ugonjwa huo bado haujabainishwa kutokana na idadi kubwa ya watu wakiwemo watoto wanaopoteza maisha kutokana na ebola mitaani na majumbani bila kuripotiwa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment