Katika siku za karibuni, kumekuwa na uvumi kuwapo gari aina ya Toyota Noah jeusi linalotumika kuteka wanafunzi maeneo mbalimbali Dar es Salaam.
Hofu Tabata Shule
Taharuki ilitokea jana saa tano asubuhi katika Shule ya Msingi Mtambani iliyopo Tabata baada ya kijana mmoja kukamatwa kwa madai ya kusambaza taarifa za gari hilo kuonekana likipakia wanafunzi na kuondoka nao.
Chanzo cha habari kilisema baada ya mkasa huo, gari hilo lilipelekwa Kituo cha Polisi Buguruni kabla ya kurudishwa kituoni hapo.
Baada ya kusambaa kwa taarifa hizo, baadhi ya wazazi na wanafunzi walifurika kituoni hapo kushuhudia gari hilo kabla ya polisi kuwatawanya wakiwataka wanafunzi warejee darasani na wengine kuendelea na shughuli zao baada ya kuwaeleza kuwa ni uvumi.
Mmoja wa mashuhuda hao, Hassan Hevod alisema mbali ya kutoshuhudia gari hilo, bado kuna kila sababu ya kufuatilia ukweli kutokana na hofu iliyojengeka.
Akizungumzia tukio hilo, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Anna-Magreth Cheyo alisema: “Wazazi wamefurika hapa nikawapeleka kila darasa kuangalia ni mtoto gani aliyepotea au kama kuna mzazi hataona mwanaye, wote wakakutana na watoto wao, cha ajabu bado wanataka kuwachukua.”
Mkuu wa Kituo cha Polisi, Tabata, Leokadia Kobelo alisema wanamshikilia mtu mmoja kwa kueneza uvumi huo.
“Hakuna kitu kama hicho cha utekaji, lakini hatuwezi kupuuza, itabidi tuzungumze na huyu kijana tunayemshikilia atueleze vizuri taarifa hizo,” alisema. alizipata wapi.”
Kamanda wa Polisi Kanda ya Ilala, Maria Nzuki alipoulizwa jana alisema: “Taarifa hizo ni uvumi na jamii isiwe na hofu.”MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment