JK AWATOLEA UVIVU WAKUU WA WILAYA NA WAKUU WA MIKOA, HANA MZAHA NAO WATAOSHINDWA KUTIMIZA KUJENGA MAABARA ZA KIDATO CHA TANO NA SITA.
RAIS KIKWETE.
RAIS Jakaya Kikwete amesema atawajibisha wakurugenzi watakaoshindwa kukamilisha ujenzi wa maabara ifikapo mwezi ujao kwani katika suala hilo, hatakuwa na mzaha. Aidha amesema kuanzia sasa, shule zote za sekondari za Serikali zenye Kidato cha Tano na Sita zitakuwa za kitaifa, kwa maana ya kuwa na mchanganyiko wa wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini, lengo likiwa ni kuendeleza utaifa kwa vijana.
Rais Kikwete ambaye alisema hayo juzi mjini hapa wakati akifungua kikao kazi cha kujadili usimamizi na uendeshaji wa Elimu ya Msingi na Sekondari, aidha amewashukia wakuu wa mikoa na wilaya akisema ambao hawajui wajibu wao ni bora wasiwepo.
Aliwaambia viongozi hao wa wilaya na mikoa kwamba, “Kama ajenda yako ni barua na posho ni bora usiwepo.’’ Wakurugenzi kitanzini Katika kikao hicho kilichoshirikisha wakuu wa mikoa yote nchini, wakuu wa wilaya, maofisa elimu wa mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na maofisa usalama, Kikwete alisema wakurugenzi wakishindwa kuhakikisha kila shule inakuwa na maabara, kazi itakuwa imewashinda.
Alisema alishatoa maagizo juu ya ujenzi wa maabara za sayansi kwani mtoto anayesoma bila maabara, hawezi kufaulu mtihani wa vitendo.
“Novemba nitauliza sina sababu ya kusahau, nasubiri Desemba 9, mwaka huu wakati wa miaka 53 ya uhuru nitauliza maswali na nitadai taarifa hizo lazima nizipate,” alisema.
“Nitamuuliza Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi, kama shule hazina maabara Mkurugenzi kazi imekushinda nitaanza na wewe, Novemba mwaka huu tutabanana, bado nitakuwa na mamlaka kamili na sitakuwa na masihara na mtu,” alisema.
Alisema katika ujenzi huo anataka kuwa na maabara za fizikia, kemia na baolojia. “Kuna mahali nilipita nikaoneshwa maabara nikanyamaza kimya nasubiri Novemba,” alisema.
Alisema maendeleo yote ya nchi hii yapo mikononi mwa wakurugenzi.
“Lakini kama Mkurugenzi hatimizi wajibu wake kwa nini yupo na kwa nini anaendelea kuwepo?” alihoji.
Shule za utaifa Akifafanua kuhusu utaifa kwa vijana, alisema kuanzia sasa shule zote za serikali zenye kidato cha tano na sita zitakuwa za kitaifa na hata zile ambazo ziko kwenye kata zitabadilishwa na lazima ziwe na mabweni ya kulala wanafunzi.
“ Tunataka kuendeleza utaifa kwa vijana, tuendelee kuwa na shule za taifa vinginevyo utakuta mtu amezaliwa Kanyigo amesoma shule ya Msingi Kanyigo, Sekondari Kanyigo, Kidato cha tano na sita Kanyigo mtu kama huyu anaelewa watu wote duniani ni Wahaya,” alisema.
Aliendelea kusisitiza, “kidato cha tano na sita lazima iwe ya taifa mwanafunzi akisoma Bukoba aende Ndanda (Mtwara) hapo watajua kuchanganyika na vijana kutoka nchi nzima, wasome shule hizo.”
Pia alisema sasa shule za kata zinaendelea kutoshelezwa kwa ubora na wanafunzi wengi wanaochaguliwa kwenda kidato cha tano na sita wanatoka shule za kata. Kuhusu uhaba wa walimu, alisema serikali imepunguza tatizo katika shule za msingi na sekondari ambapo mwaka jana walimu 18,000 waliajiriwa.
Alisema kwenye baadhi ya wilaya, kuna ziada ya walimu wa sanaa lakini tatizo lililopo ni upungufu wa walimu wa sayansi na hisabati, tatizo ambalo linaendelea kupatiwa ufumbuzi. Mahitaji ni walimu wa sayansi na hisabati 18,277 huku uwezo vyuo vyote ukiwa ni walimu 2,500.
Aliagiza mwaka 2016 kila mtoto awe na kitabu chake cha kila somo. Wanafunzi Vyuo Vikuu Pia alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoingia vyuo vikuu nchini kutoka 40,000 mwaka 2005 hadi kufikia 204,000 na kuweza kufikia Wakenya na kuwapita Waganda kwa idadi ya wanafunzi
Alisema Serikali imetoa wigo mpana kwa vyuo vikuu na wanafunzi wote wanapata mikopo na sasa hakuna mwanafunzi mwenye sifa anayeweza kukosa nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu.
Alisema Chuo Kikuu cha Dodoma kilichojengwa kwa fedha za ndani, kinachukua wanafunzi 20,000 na lengo ni kufikia wanafunzi 40,000.
Alisema wanafunzi wataongezeka taratibu kutokana na chuo hicho kuendelea kujitanua. Utoro Pia aliwataka viongozi hao kuhakikisha watoto wanaoandikishwa shule ya msingi wanamaliza Darasa la Saba tofauti na sasa ambapo wanafunzi wengi wamekuwa wakiacha shule. Wakati huo huo, alitaka kulindwa kwa maeneo ya shule yasivamiwe na wakurugenzi wasaidie vijiji kupata hati.
“Kila shule eneo lake linajulikana lipatiwe hati na liwekewe mipaka ili watu wasiliingilie,” alisema.
Pia alitaka kuwe na matumizi mazuri ya fedha kwenye masuala ya elimu. Viongozi waoga Alisema viongozi wengi ni waoga na si wabunifu hasa katika suala la ujenzi wa nyumba za walimu.
Aliwataka wakurugenzi kuacha kugeuza shule za sekondari yatima kwa kudhani wajibu wao ni kusimamia shule za msingi tu. “Kila kata ina sekondari kabla ya shule za kata zilikuwa chini ya wizara lakini sasa shule hizo ni za halmashauri,” alisema.
Alitaka wakurugenzi kusimamia vizuri walimu wapya waliopo katika maeneo yao wapate mishahara kama wanavyostahili kwani kucheleweshewa fedha zao ni kutokana na uzembe unaofanywa na baadhi ya watendaji Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia alisema kikao hicho cha siku tatu kinahudhuriwa na washiriki 908. Pia alisema kikao hicho kimeridhia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuwa Chuo Kikuu Huria cha Taifa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment