BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KWANINI MWL NYERERE HAJAENZIWA KWA VITENDO ?, SUALA LA HAKI NA USAWA NDANI YA JAMII YA WATANZANIA LINAKOSEKANA.


IKIWA leo ni miaka 15 tangu kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, imebainika kuwa bado suala la haki na usawa ndani ya jamii ya Watanzania linakosekana na hivyo kushindwa kumuenzi vyema muasisi huyo wa taifa.

Aidha, imebainika kuwa kutokana na uongozi wa kuigwa aliokuwa nao Mwalimu Nyerere, viongozi wengi nchini wamejitahidi kuiga mfano wake, lakini bado wengi wao wameshindwa kumfikia.

Akizungumza na gazeti hili, kuhusu maadhimisho ya Kumbukumbu ya Kifo cha Mwalimu Nyerere, yanayofanyika nchini kote leo, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Jaji Joseph Warioba, alisema pamoja na kwamba tangu kifo chake, nchi imeendelea kupata maendeleo, bado hali ni tofauti ndio maana kiongozi huyo anaendelea kukumbukwa.

“Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi anayeongoza kwa mfano, alichokuwa anakisema na kukihimiza ndicho alichokuwa anakitenda, kama alizungumzia uzalendo hakuzungumzia kwa nadharia tu bali alionesha kwa vitendo, na alionesha kweli uzalendo aliokuwa nao kwa nchi yake,” alisema Jaji Warioba.

Alisema kiongozi huyo, alikuwa akiijali nchi na watu wake na aliwaongoza Watanzania kwa usawa, haki na uhuru bila kuweka au kujali maslahi yake.

Hakuna kama Nyerere “Aliwaunganisha Watanzania ndio maana nchi hii ikawa na umoja na yeye akawa ni kiongozi wa watu, kuna viongozi wengi ikiwamo mimi, tulijaribu kumuiga lakini siamini kwamba kuna mmoja wetu aliyeweza kumfikia Mwalimu Nyerere, na hiki ndicho tunachokitafuta hadi sasa,” alisisitiza.

Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe nchini, Gallus Abeid, alisema katika uongozi wa Mwalimu Nyerere aliamini katika dhana ya mambo manne ambayo ni watu, siasa safi, ardhi na uongozi bora ambayo ndio ulikuwa msingi wa maendeleo.

Alisema jambo la kusikitisha ni misingi hiyo kutokupewa kipaumbele na kuendelezwa katika kipindi cha sasa ambapo katika eneo la watu ambao waliaminika kuwa ndio nguvu kazi ya maendeleo, imebebwa na kupokonywa na wawekezaji huku katika eneo la ardhi iliyokuwa mali ya taifa enzi za Mwalimu sasa imekuwa ndio chanzo cha migogoro nchini.

“Zamani nchi ilikuwa ikiendelezwa na wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania wote, vyakula na uchumi uliendeshwa kwa kutegemea wakulima hawa wadogo, lakini sasa hivi eti utasikia wakulima wawekezaji, wapo kila sekta na matokeo yake si mazuri kama inavyotarajiwa,” alisema.

Alisema enzi za Mwalimu watu waliokuwa wakihodhi mashamba na kuyakodisha kwa wenzao walikuwa wakiitwa Nyambuja, kwa mtindo wa wawekezaji watu hao wanarejea taratibu kwani wawekezaji wengi wenye mashamba makubwa wameyahodhi na kuyakodisha kwa Watanzania ambao ni mali yao.

Kuhusu suala la ardhi, mzee Abeid ambaye pia kwa sasa ni Msaidizi wa mwanasiasa mkongwe na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisema kwa sasa eneo la ardhi limejaa migogoro mingi ambayo hapo awali haikuwepo kutokana na sera ya Mwalimu Nyerere kuwa ardhi yote ni mali ya taifa.

Alikufa akilia na rushwa
Akizungumzia suala la rushwa, alisema Baba wa Taifa hadi anaondoka duniani, vita yake kubwa ilikuwa ni tatizo la rushwa aliloliita kuwa ni adui wa haki lakini kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi wa kutosha katika eneo hilo, nchi nzima inanuka rushwa.

“Nawaomba katika kumuenzi baba wa taifa, haya mambo matatu inabidi yafanyiwe kazi, kwani Watanzania tusipokuwa macho, tutarudi tena kwenye hali mbaya, tutajirudisha wenyewe kwenye utumwa,” alisisitiza.

Kimiti, Shivji wanena
Naye mwanasiasa mkongwe na aliyekuwa Mbunge wa Sumbawanga Paul Kimiti, alisema katika kuadhimisha siku ya kumbukumbu ya baba huyo wa Taifa, Watanzania hawanabudi kumuenzi kwa kutekeleza kwa vitendo aliyoyaamini ikiwa ni pamoja na suala zima la siasa ya ujamaa.

Alisema enzi za uongozi wake, alikuwa akiamini juu ya suala zima la haki sawa, usawa na uhuru kwa kila Mtanzania lakini tangu Tanzania iingie katika uchumi wa soko, misingi yote hiyo imebomoka.

“Kwa sasa watu hawatendewi haki, watumishi wengi wanajali maslahi yao tu, uhuru uliokuwa unapiganiwa na Mwalimu haupo tena wala utii wa viongozi haupo, siku hizi kusikia mtu mzima anatukana hadharani si jambo la ajabu, kama Mwalimu angekuwa hai, haya yanayoendelea kamwe asingeyapenda,” alisema Kimiti.

Aidha, alisema zamani Tanzania haikuwa na tofauti kubwa ya wananchi wake kiuchumi na ndio maana kulikuwa na Sera ya Ajira ambayo ilionesha mtu mwenye kipato cha kima cha chini hatofautiani sana wa kipato cha juu.

“Leo hii ni hatari, aliye chini anazidi kukandamizwa na aliyenacho ndio anazidi kupata zaidi. Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji, alisema mambo mengi yanayoendelea kutokea nchini yanadhihirisha fikra na ukweli aliokuwa nao Mwalimu Nyerere.

Alisema kiongozi huyo alikuwa anaamini kuwa bila kujenga jamii yenye usawa, lazima kutatokea mfarakano na kusababisha ukosefu wa amani.

“Aliamini kuwa huwezi kuwa na amani kama hakuna usawa, hizi ni fikra ambazo alizijenga katika maandishi yake na hata kwenye hotuba zake.”

Alisema mfumo wa usawa uliojengwa na Mwalimu Nyerere sasa unabezwa na umeanzishwa mfumo tofauti na kusisitiza kuwa ni muhimu katika kumuenzi kuhakikisha kuwa tunazitekeleza kwa vitendo fikra zake zilizosisitiza kuwa binadamu wote ni sawa.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: