UKAWA WAIBUKA NA MBINU MPYA LENYE LENGO LA KUGAWANA MAJIMBO, BAADA YA KUMALIZIKA KWA BUNGE MAALUMU LA KATIBA MPYA MJINI DODOMA.
Moshi. Baada ya kumalizika kwa Bunge la Katiba, hasira za Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) dhidi ya CCM zimehamia kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, safari hii ukiunda kamati maalumu kutafuta namna ya kumsimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana majimbo.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia ametoa maelezo hayo alipokuwa akizugumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu hivi karibuni.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema tayari kamati zimeundwa na zinaendelea na kazi ya kuratibu mpango huo mahususi, unaolenga kuiondoa CCM madarakani.
“Lengo letu ni kuhakikisha Ukawa ina nguvu ya kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na katika mpango huo, vyama vitaachiana majimbo na viti vya udiwani kulingana na nguvu ya chama katika sehemu husika,” alisema.
Ukawa; umoja ulioanzishwa Februari mwaka huu ukiwa ni kikundi shinikizi katika mchakato wa Katiba katika siku za mwanzo za Bunge Maalumu la Katiba, unaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
Mbatia alisema anaamini kwa mkakati huo uliopangwa na Ukawa, CCM itakuwa na wakati mgumu katika uchaguzi mkuu ujao.
“Sasa hivi ziko kamati zinaaendelea na maandalizi ya namna ya kushirikiana katika uchaguzi mkuu ujao na nataka nikuhakikishie siku za Serikali ya CCM zinahesabika,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Kamati hii inatafiti ni namna gani bora ya kuachiana madiwani, wabunge na rais ili tusimamishe mgombea mmoja katika kila eneo na tutakubaliana nani asimame wapi.”
Mbatia alisema uchaguzi mkuu ujao utamalizika kwa wabunge wengi wa upinzani kuingia bungeni na iwapo mambo yatakwenda kama walivyopanga, CCM kinaweza kuwa chama cha upinzani.
“Kwa sasa wagombea kutoka Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD ni ruksa kutangaza nia, lakini kamati yetu itasema nani miongoni mwao ateuliwe kupeperusha bendera ya Ukawa,” alisema.
Mbatia aliwahakikishia Watanzania kuwa ushirikiano wa vyama hivyo si nguvu ya soda na kusisitiza kuwa wanaofikiri ushirikiano huo utavunjika kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015 ni ndoto za mchana.
“Kwanza tumekwishaunda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, tuko pamoja na lengo letu tunakuwa na ushirikiano ambao umeonekana tangu Bunge la Jamhuri, Bunge la Katiba na sasa hivi Ukawa.”
Aionya CCM
Mbatia alisema kitendo cha CCM kutumia wingi wao ndani ya Bunge la Katiba kupitisha Katiba yenye masilahi yao, kinaweza kuleta machafuko nchini.
“Siku zote nawaambia na huu utaendelea kuwa wasia wangu kwamba kuandika Katiba Mpya ni tendo la maridhiano. Kunapokosekana maridhiano hiyo Katiba inakosa uhalali wa kisiasa,” alisema.
“Walipaswa kufuata busara za Jaji (Joseph) Warioba na timu yake. Miezi miwili na nusu walikaa kuzungumza na kuridhiana, hakuna hata siku moja walishindwana na kufikia hatua ya kupiga kura.
“Ndani ya Tume kulikuwa na wajumbe kutoka vyama vya siasa, majaji, wanasheria na viongozi wa dini. Walitanguliza Utaifa na uzalendo na hilo ndilo lililofanya wakapata rasimu bila kupiga kura.
“Ni ukweli wanasema wamepata theluthi mbili ya kura na wakapitisha Katiba Inayopendekezwa, lakini wajue wanajidanganya kwa sababu itakataliwa kuanzia siku ya kwanza.
“Suala la Katiba siyo wingi wa wajumbe wala wingi wa kura watakazozipata, bali ni maridhiano lakini wakilazimisha wanakaribisha machafuko.”
Hata hivyo, Mbatia alisema bado milango ya kutafuta maridhiano iko wazi na rais ajaye baada ya Kikwete, lazima aendeleze maridhiano kama kweli anataka kuinusuru Tanzania.
Akana kupewa maelekezo
Mbatia ambaye ni mbunge wa kuteuliwa, alisema pamoja na Rais Jakaya Kikwete kumteua kuwa mbunge, hajawahi kumshawishi hata siku moja kuhusu nini cha kuzungumza ndani ya chombo hicho.
Badala yake, alisema yote anayoyafanya yanasukumwa na utashi binafsi na misimamo ya chama chake.
Uteuzi wa Mbatia kuwa mbunge ulipokewa kwa hisia tofauti huku wengine wakidhani kuwa amepewa wadhifa huo ili kumziba mdomo au kupenyeza agenda zake ndani ya Bunge.
Hata hivyo, Mbatia alikanusha hisia hizo akisema tangu ateuliwe amekuwa wakitekeleza majukumu yake bila kupewa maelekezo na Rais Kikwete.
“Rais aliniteua kuwa mbunge wakati huo alijua kwamba mimi ni kiongozi wa chama cha siasa cha NCCR-Mageuzi na miongoni mwa waasisi wa mageuzi hapa nchini.
“Niliapa tarehe 12 Juni, 2012 kuwa mtiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninatekeleza majukumu yangu ya kibunge kwa mujibu wa Katiba,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Wale walioko serikalini wamekula kiapo cha kuwa watiifu kwa Serikali, yaani kwa JK (Jakaya Kikwete). Lakini kiapo changu mimi nimekula bungeni cha kuwa mtiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Wale wanakula kiapo chini ya Rais ni tofauti na mimi. Rais Kikwete anatoa maelekezo yake kwa chama chake (CCM) na Serikali yake siyo kwangu.”
Alisema hata Rais Kikwete alipomteua Ismail Jussa mwaka 2005-2010 kuwa mbunge, alikuwa anajua kuwa Jussa ni wa CUF na ameingia bungeni kwa misimamo ya CUF.
“Watu watofautishe hili jambo kwamba misimamo ya vyama vya siasa ndani ya Bunge ni kila chama kina sera yake, itikadi yake na kina misimamo yake na malengo yake,” alisema.
Mbatia alitoa mfano wa jinsi alivyoichachafya Serikali alipowasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu udhaifu katika kusimamia mitalaa ya elimu nchini.
“Kama utakumbuka, baadaye waziri mkuu aliniteua niwe mjumbe kwenye Tume ya Mchome, nilimkatalia Waziri Mkuu kwa sababu ilikuwa inakwenda kinyume na utashi wangu,” alisema.
“Niliwasilisha hoja ya elimu bungeni Januari 31, mwaka jana wao wakatumia wingi wao wa CCM kupinga hoja yangu, sasa ile hoja yangu ilikuwa ni maelekezo ya JK?” alihoji na kuongeza:
“Lakini Rais tulipokutana aliniuliza mbona malumbano makali, nikamwambia ukweli juu ya udhaifu wa mitalaa ya elimu na Aprili 30, mwaka jana akiwa Mbeya alikubaliana na mimi.
“Akiwa Mbeya anazungumza na wamiliki wa shule akasema anakubaliana na Mbatia na akasema elimu yetu ni dhaifu sana hata mitalaa ni migogoro mitupu. Nilifanya kwa masilahi ya nchi.”
Mvutano wake na Mrema
Kuhusu mvutano ulioibuka baina yake na Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, Mbatia alimtaka mwanasiasa huyo mkongwe kuacha kutafuta mchawi na kwamba atulie kwa kuwa hana hatimiliki ya jimbo hilo.
Mvutano huo uliibuka hivi karibuni baada ya Mbatia kutangaza nia ya kugombea ubunge Vunjo, kitendo ambacho Mrema alikitafsiri kama mapinduzi.
Mrema alikwenda mbali na kumshtaki Mbatia kwa Rais Kikwete akimtaka amfukuze ubunge aliompa kwa vile anamwingilia katika jimbo hilo akitaka kumng’oa.
Mrema aliyarejea malalamiko hayo ndani ya Bunge la Katiba mjini Dodoma akifichua namna alivyomshtaki Mbatia kwa Rais na kudai Rais alimhoji Mbatia kuhusu nia yake hiyo.
“Ninapaswa kuwa mwadilifu na kuheshimu vikao vya faragha. Kile kilikuwa ni cha faragha na nilishtuka sana nilipomsikia Mrema akivujisha kile kilichotokea mle ndani.
“Lakini nataka niseme kwa dhati ya moyo wangu kuwa sifahamu hasa msingi wa malalamiko yake. Nionavyo, kile kikao hakikuwa forum (jukwaa) la malalamiko ya aina ile.
“Tulikuwa tunajadili mustakabali wa amani ya nchi yetu. Tulikuwa tunajadili njia gani za maridhiano zitakazosaidia kuimarisha mshikamano na umoja wetu kama Taifa katika mchakato wa Katiba.
“Bahati mbaya sana, Mzee wangu Mrema alihama kabisa kwenye mada lakini hili nawaachia Wanavunjo wapime kama bado anastahili kuendelea kuwawakilisha,” alisema Mbatia.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment