MKOA WA DAR ES SALAAM NI MKOA UNAONGOZA KWA KESI NYINGI ZA MIGOGORO YA ARDHI.
Dar es Salaam. Jaji wa Mahakama ya Ardhi, Richard Mziray amesema Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na kesi nyingi za migogoro ya ardhi.
Alisema hayo juzi jijini hapa alipokutana na wadau wa mazingira, wakulima na wafugaji waliokuwa wakitoa malalamiko yao kwenye mahakama ya wazi.
Jaji Mziray alisema matapeli wameibuka kwa wingi na wanauza kiwanja kimoja kwa watu zaidi ya wawili na wote huwakabidhi hati miliki ambayo ni vigumu mtu kugundua bila kwenda kuithibitisha wizarani.
Alisema kesi zilizoripotiwa kwenye mahakama hiyo zinahusu migogoro ya viwanja na nyingine za wenye nyumba na wapangaji kutoelewana kwenye mikataba waliyokubaliana.
Alisema migogoro hiyo inaendelea kuongezeka kutokana na wananchi kutoelewa Sera za Ardhi na utekelezaji wake.
Aliitaka Serikali ifanye utaratibu wa kutenga maeneo ya wafugaji na wakulima kwa kuwapimia na kuwapa hati miliki ili kuepuka migogoro.
Jaji Mziray alisema uamuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji kwenye hifadhi ya Suledo iliyopo wilayani Kiteto, ulishatolewa na Mahakama ya Rufani na kuwataka watu wote waondoke kwenye eneo hilo.
Mfugaji kutoka Kijiji cha Sulendo, mkoani Arusha, Salome Raphael alisema mahakama iitake Serikali na vyombo vyake kutunga sera na sheria zitakazotekelezwa kwa ajili ya kulinda mazingira.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment