BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

AKAUNTI YA ESCROW IPTL NAMNA ILIVYOITIKISA TANZANIA NA KUIWEKA NCHI KIPINDI CHA MPITO.

http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/1890896/highRes/531746/-/maxw/600/-/dtf1gqz/-/anna.jpg 
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, amesema sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), limetikisa Taifa na kwa sasa nchi iko katika kipindi cha mpito.


Makinda aliyasema hayo jana katika viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam, baada ya halfa ya Rais kumuapisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Juma Assad, aliyechukua nafasi ya Ludovick Utouh, aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, alisema mtikisiko huo ni mzuri kwa kuwa unaweka mazingira ya uwajibikaji na kujenga msingi imara wa nchi.

“Kwa sasa nchi ipo katika kipindi cha mpito baada ya sakata la Escrow, ndicho kipindi cha kutengeneza sura halisi ya nchi yenye uwajibikaji na nidhamu ya fedha ya umma,” alisema na kuongeza:

“Mtikisiko ni mzuri katika uendeshaji wa nchi, unatufanya tukae sawa kwa kujenga nidhamu ya fedha, ili nchi isimame vizuri ni lazima ipite kwenye hali iliyopo sasa na baadaye itasonga mbele,” alisema.

Makinda alisema kitimtimu kilichopo ni kawaida ili nchi iweze kusimama na kwamba lengo la msingi ni kujenga nchi yenye nidhamu katika fedha.

Alisema CAG mpya ni mwenye ujuzi mwingi katika masuala ya fedha, hivyo matarajio ya Watanzania wengi ni kufanya kazi kwa bidii zaidi kwa kuzingatia maslahi ya nchi.


Sakata la Escrow liliibuliwa bungeni, Mei, mwaka huu, na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na kuzua mvutano mkali bungeni kiasi cha kutakiwa kufuta kauli kwa kulidanganya Bunge.

Mbunge huyo aliendelea na msimamo wake na kutaka Bunge kuunda kamati ya kuchunguza sakata hilo kwa kueleza kuwa kiasi cha Sh. bilioni 300, zimechotwa kwenye akaunti hiyo.

Juni mwaka huu, Bunge liliagiza Ofisi ya CAG kufanya ukaguzi wa fedha hizo na ripoti yake kuwasilishwa bungeni.

Katika kikao cha Bunge kilichomalizika Jumamosi iliyopita, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), iliwasilisha ripoti ya uchunguzi baada ya kukabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa CAG na kuipitia kisha kutoa mapendekezo mbalimbali, yaliyosababisha mvutano mkali wakati wa mjadala bungeni.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuwafuta kazi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutokana na kutoa kauli mara kwa mara kuwa fedha hizo hazikuwa za umma kinyume na taarifa ya CAG na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwa ni za umma.

Wengine ambao PAC ilipendekeza wafutwe kazi ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema; Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu, Eliakim Maswi. Mwingine ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, kwa kupokea Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engeneering and Marketing, James Rugemalira ambaye ni mwanahisa katika IPTL.

Hata hivyo, Bunge katika mazimio yake liliwaondoa Pinda na Masele.

UTOUH: UTEUZI WA CAG ULICHELEWA
CAG Mstaafu, Ludovick Utouh, alisema uteuzi huo ulichelewa kwani ofisi hiyo ni nyeti sana, hivyo kukaa bila CAG kamili inakosa nguvu kwani tangu alipostaafu Septemba 19, mwaka huu, ilikuwa ikisimamiwa na Kaimu CAG.

“Nimewaachia ofisi iliyo imara, madhubuti na yenye wachapakazi madhubuti, natumaini mazuri yote yataendelezwa kwa manufaa ya Taifa letu,” alisema.

PROF. ASSAD AAHIDI
Akizungumza mara baada ya kuapishwa alisema atatekeleza kwa uaminifu majukumu yote ya ofisi ya CAG kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Alipotakiwa kueleza majibu yaliyopo kwenye ripoti ya Kamati ya PAC juu ya sakata ya akaunti ya Tegeta Escrow, ambayo taarifa ya CAG ilieleza inawezekana fedha zilizokuwamo kwenye akaunti hiyo ni za umma, alisema hawezi kuzungumza hadi atakapoiona na kuisoma ripoti hiyo.

“Siwezi kusema majibu, nikishaisoma nitajua majibu hayo yalitoka wapi,” alisema na kuongeza:

“Nitafanya kazi kwa kushirikiana na timu iliyopo kuhakikisha mapato na matumizi ya serikali yana kwenda vizuri,” alisema.

WAZIRI WA FEDHA
Naye Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, alisema wizara yake inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha taratibu, kanuni na sheria za fedha zinafuatwa.

Baada ya hafla ya kuapishwa CAG Prof. Assad, alipokelewa katika ofisi yake na baadaye kukabidhiwa ripoti yenye kurasa 78, ikieleza changamoto, ofisi ilivyo na shughuli za ofisi kwa ujumla.

Baada ya kupokea ripoti hiyo, alishukuru na kueleza kuwa utaratibu huo unastahili kuigwa kwa kuwa unarahisisha utendaji kazi kwa kiongozi mgeni na kwamba amefanyakazi maeneo mbalimbali, lakini hakuwahi kupewa ripoti kama hiyo.

Viongozi waliohudhuria halfa hiyo ni Makamu wa Rais; Dk. Mohamed Gharib Bilal; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande; Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Magereza, John Minja.

Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu; Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe na Makamu wake, Deo Filikunjombe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Mahusiano), Stephen Wassira. CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: