Sakata la escrow linatuchochea kuuliza swali hili: Je, Bunge letu limefunga ndoa na Serikali? Kuhusu Bunge, Katiba ya Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inasema:
“Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.”
Hii ni ibara ya 62 kifungu cha pili. Kifungu cha tatu kinaendelea kufafanua zaidi kazi ya Bunge kwa kusema:
“Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake, Bunge linaweza (a) Kumuuliza Waziri yeyote swali kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake;(b), kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa kati ya Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo.”
Kwa mujibu wa katiba yetu, Bunge likifunga ndoa na Serikali, linakuwa linaivunja Katiba, na kwa maneno mengine halipaswi kuwapo!
Huwezi kufunga ndoa na Serikali na papo hapo ukaendelea kuisimamia na kuishauri. Kawaida ya ndoa, inafanya wawili kuwa mmoja.
Kwa maneno ya ufafanuzi ni kwamba ndoa kati ya Bunge na Serikali ina maana ya kulifuta Bunge na kubaki na Serikali au kuifuta Serikali na kubaki na Bunge.
Haiwezekani baada ya ndoa vyote viwili viendelee kuwapo na kufanya kazi. Katika nchi ya kidemokrasi, hili haliwezekani.
Ushahidi ni nchi za kidikteta au zile zinazoongozwa kijeshi, ambako jambo la kwanza linalofanya baada ya jeshi kufanya mapinduzi au kuchukua madaraka kwa mabavu, ni kulifuta Bunge!
Hivi sasa kuna malalamiko kwamba Serikali imefunga ndoa ya mkeka na vyombo vya habari.
Vyombo vya habari vinasifu tu yale yote ya Serikali ya awamu ya nne na kwamba baadhi ya vyombo vya habari vimenunuliwa na vigogo au marafiki wa vigogo serikalini.
Je, tuanze kuamini kwamba na Bunge, letu tukufu limefunga ndoa ya mkeka na Serikali? Au kwamba Bunge letu tukufu limeingia mfukoni mwa vigogo? Kama hili ni kweli, basi tunaelekea pabaya.
Na kama kuna mtu anayeshauri mfumo huu, atakuwa ni adui mkubwa wa Tanzania. Mfumo wa kuviweka vyombo vya habari mfukoni, mfumo wa kuliweka Bunge, mfukoni, hauwezi kuleta neema kwa taifa letu.
Mfumo kama huu ulifanikiwa wapi duniani?
Kama Bunge, linafunga ndoa na Serikali, ni nani atawasemea wananchi? Ni nani ataisahihisha Serikali?
Wabunge ndiyo macho ya taifa, wabunge ndio mdomo wa taifa. Haiwezekani Serikali ikafanya kila kitu bila kukosea.
Serikali inaongozwa na watu na wala si malaika. Hivyo kutokea makosa ni jambo la kawaida.
Yakitokea basi, kuna vyombo vya kuyashughulika na kusaidia kuyaondoa. Ndio maana kuna vyombo kama Bunge.
Mbali na ndoa ya mkeka ni kwamba baadhi ya wabunge wetu hawajiamini. Kwa pande zote mbili, wawe wa chama tawala au wale wa upinzani.
Wanashindwa kukumbuka kwamba wako bungeni kwa kutumwa na wananchi. Wakibanwa kidogo na kuelekezwa katika barabara ya kupoteza donge nono mdomoni mwao, wanakuwa wepesi kutupilia mbali hoja, hata kama ni hoja yenye msingi namna gani.
Wabunge wa CCM, wakibanwa, wanalazimika mbele ya chama na kuwatelekeza wapiga kura wao ambao siyo lazima wote wawe wa CCM.
Hata hivyo, mbunge akishapitishwa, anakuwa mbunge wa wote. Tumeshuhudia wabunge wakiyeyuka na kuachilia hoja zenye uzito na zenye kulenga kutetea maslahi ya taifa. Wabunge wasiojiamini, ni kizingiti cha Bunge kuiwajibisha serikali.
Tunasikia wanasema kwamba bungeni kuna ‘vurugu’; tunasikia kwamba bungeni hakuna nidhamu; tunasikia wanasema kwamba watu waheshimiwe; na wabunge wenye tai na suti hawawezi kufanya vurugu.
Tunawajua wenye tai na suti majambazi; tunawajua wenye tai na suti lakini matapeli; na tunawajua wenye tai na suti lakini mafisadi.
Nani kasema Bunge ni uwanja wa kuwatafuta ‘warembo? Bunge ni uwanja wa mapambano; Bunge ni uwanja wa kugawana keki ya taifa.
Bunge ni chombo cha kuiwajibisha Serikali; Bunge si sehemu ya kwenda kustarehe; ni sehemu ya kwenda kufanya kazi na kupambana kuhakikisha keki ya taifa inagawanywa kwa usawa.
Katika hali hiyo ni muhimu na ni lazima kuwa na kanuni za hali zote; kanuni za kushangilia, kanuni za kushambuliana na kanuni za kuwajibishana.
Kosa, likifanyika la kuegemea upande mmoja wa kushangilia na kutukuza, kosa likifanyika la Bunge kufunga ndoa na Serikali ni lazima vurugu zitokee.
Ni bahati mbaya kwamba kanuni za Bunge letu zilitengenezwa kwa lengo la kuisifia na kuishangilia Serikali. Ni tofauti na kanuni za mabunge yote duniani.
Kanuni nyingi za mabunge zinalenga kuwabana wabunge ili nao waibane Serikali. Lakini kanuni za Bunge letu hazikutengenezwa kwa lengo la kuhakikisha Bunge linaiwajibisha serikali.
Ni matokeo ya chama kimoja, chama kushika hatamu na chama kuwa juu ya serikali. Ni bahati mbaya pia kwamba ‘zama’ hizi za Bunge kuishangilia na kuitukuza Serikali zinapita kwa kasi ya kutisha, bila maandalizi, maana ‘muda’ nao hauna maandalizi.
Kanuni za kuishangilia Serikali zikikutana na wawakilishi wa wananchi wanaotaka kuiwajibisha Serikali yao; matokeo yake ndio wenye kuona karibu wanaita vurugu.
Kuna vurugu gani kama watu wanataka haki itendeke? Kuna vurugu gani kama wabunge wanafanya kazi yao ya kuiwajibisha Serikali?
Tanzania, iko kwenye kipindi cha mpito na kwa namna fulani ni kujikuta njia panda: Tumetoka kwenye mfumo wa chama kimoja na kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi.
Tumeuzika ujamaa na kuukumbatia ubepari uliochanganyikana na utandawazi na ubeberu. Tumetupa analojia na kukumbatia digitali.
Sera yetu ni kuwakaribisha wawekezaji. Katika hali kama hii ni lazima kuwa na Bunge imara, vinginevyo ni kutaka kuiuza nchi.
Na Bunge, imara siyo lile la kuishangilia Serikali na kuitukuza, siyo la kuvaa tai na suti, bali Bunge linalofanya kazi, linalopambana kwa hoja hata ikilazimika kushikana mashati.
Tunahitaji Bunge linaloangalia utukufu wa taifa, zaidi ya kuangalia utukufu wa Spika, tunahitaji Bunge linaloangalia utukufu wa taifa zaidi ya kuangalia utukufu wa serikali.
Mtu anayeweza kuchangia kuwapo ndoa kati ya Bunge na Serikali ni Spika wa Bunge.
Mfano mzuri ni pale Bajeti ya Wizara mbalimbali zinapokuwa zikijadiliwa. Spika wa Bunge kwa namna mmoja au nyingine, anasaidia Bajeti za wizara nyingi kupita.
Kwa kufupisha muda wa majadiliano, kwa kuruhusu kura za ndio na hapana ambazo mara nyingi ni ushabiki bila kuzingatia hoja na kwa kujifanya kufuata kanuni za Bunge, zilizopitwa na wakati.
Wakati tunapiga vita ndoa ya vyombo vya habari na Serikali, tukumbuke pia kupiga vita ndoa ya mkeka kati ya Bunge na Serikali. Tumpige vita Spika wa Bunge la Muungano, kuchochea na kuhimiza ndoa hii ambayo inafungwa kinyume cha sheria.
za nchi yetu. Ndoa hii ni batili.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment