BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

AKAUNTI YA TEGETA ESCROW SASA YACHANGANYA WATANZANIA, PROF MUHONGO, TIBAIJUKA NJIA NYEUPE ?.

 
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Juma Assad.

WAKATI kukiwa na taarifa zinazochapishwa na vyombo vya habari kuwa akaunti ya Escrow iliyofunguliwa Benki Kuu (BoT), kwa mujibu wa makubaliano yaliyofanyika Julai 5, 2006, zilikuwa Sh bilioni 306.6, kabla ya kutolewa kwa fedha hizo mwaka 2013, taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imethibitisha sio kweli.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya CAG, ambayo Rais Jakaya Kikwete ameshaagiza iwekwe hadharani, ili Watanzania waisome na kuielewa, katika ukurasa wa 40 mpaka 42, imebainisha kuwa kiasi cha fedha kilichokuwa katika akaunti hiyo, kilikuwa Sh bilioni 182.7.

“Baada ya kufanya uhakiki wa taarifa zilizopatikana Tanesco (Shirika la Umeme), Wizara ya Nishati na Madini na Benki Kuu (BoT); timu ya ukaguzi ilibaini kuwa Tanesco pamoja na Wizara waliweka kwenye akaunti ya Escrow kiasi cha jumla ya Sh bilioni 182.7. Tanesco iliweka kiasi cha Sh bilioni 142 na Wizara iliweka Sh bilioni 40.7,” taarifa hiyo ilieleza.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa, kama kaunti hiyo ingekuwa na Sh bilioni 306.6, basi Tanesco wangepaswa kuweka kiasi cha Sh bilioni 123.9 zaidi ya fedha zilizowekwa katika akaunti hiyo.

“Kwa mujibu wa ankara zilizotolewa na IPTL kwa kipindi cha mgogoro, Tanesco ilipaswa kuweka kiasi cha Sh bilioni 123.9 zaidi ya fedha ilizoweka katika akaunti ya Escrow, ikiwa ni tofauti kati ya kiasi ilichotakiwa kuwekwa cha Sh bilioni 306.6 na kiasi kilichowekwa cha Sh bilioni 182.7,” ilieleza ripoti hiyo.

Mlipaji kodi
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, Mkataba wa kununua umeme kati ya Tanesco na IPTL wa mwaka 1995, kipengele namba tatu, kinaitaka Tanesco kulipa gharama za umeme kila itumiapo umeme na tozo ya uwekezaji (capacity charge) kila mwezi, ili kufidia gharama za uwekezaji wa mitambo ya IPTL.

CAG katika ripoti hiyo ameeleza kwa kuwa gharama za uwekezaji pamoja na VAT zililipwa kwa IPTL, wajibu wa kuwasilisha kodi hiyo katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ulikuwa wa IPTL kwa mujibu wa vifungu namba 3 na 4 vya Sheria ya Kodi la Ongezeko la Thamani ya mwaka 1997, iliyorejewa mwaka 2006.

“Hata hivyo katika mahojiano tuliyofanya na Kamishna Mkuu wa Kodi, alithibitisha kuwa TRA wanaendelea na hatua za kuikusanya kodi husika kutoka IPTL,” imeeleza ripoti hiyo ya CAG ukurasa wa 35.

Kodi hiyo ya VAT inayodaiwa IPTL kwa mujibu wa CAG, ni Sh bilioni 26.9, kama ilivyoainishwa katika barua ya aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya kupitia barua yake yenye kumbukumbu Na. 100-221-969/214 ya Oktoba 29, 2013, kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile.

Ushauri wa wanasheria
Katika mgogoro wa ukokotoaji wa tozo ya uwekezaji, Juni 30, 2004 Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco ilialika kampuni ya Mkono and Co Advocates kuwasilisha taarifa ya uchunguzi kuhusu gharama za uwekezaji zinazotozwa na IPTL.

“Tanesco ilishauriwa kutokubaliana na ankara za malipo ya gharama za uwekezaji zitakazowasilishwa na IPTL, baada ya kubaini kuwa kiwango cha tozo hizo, hukokotolewa kwa kuzingatia mtaji wa wanahisa, ambao ni dola za Marekani milioni 38.16, badala ya Sh 50,000,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa CAG, baada ya ushauri kutoka kampuni ya Mkono, Bodi ya Tanesco iliunda Kamati Ndogo ya Bodi iliyoundwa na Arnold Kilewo, B. Mrindoko na Dk Enos Bukuku, ambayo iliandaa taarifa na kuiwasilisha katika kikao cha Bodi.

“Kamati ilibainisha kuwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 38.16, kilikuwa mkopo wa wanahisa kwa kampuni na kilikuwa kinarejeshwa kama mkopo na si kama gawio. Hivyo kamati ilishauri Wizara ya Nishati na Madini kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kuitisha mazungumzo baina ya pande mbili (Tanesco na IPTL), ili kutatua mgogoro huo,” ilieleza taarifa hiyo ya CAG na hiyo ilikuwa Agosti 2004.

Pamoja na ushauri huo wa Kampuni ya Mkono na Kamati ndogo ya Bodi ya Tanesco, Bodi ya Tanesco katika kikao chake hicho cha kupokea ushauri wa Kamati ndogo cha Agosti 13, 2004, iliazimia kupata maoni mengine ya kisheria kutoka kwa Kampuni ya Hunton and Williams LLP, ambao ni mawakili wa Tanesco katika kesi iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).

Kampuni ya Hunton and Williams katika ushauri wake ilieleza, “Kwa kutolipa gharama za uwekezaji, Tanesco hawakuwa na nafasi ya kushinda katika shauri (kesi iliyopo ICSID) na hivyo kushauriwa kukaa pamoja na IPTL, kujadili kukubaliana juu ya mtaji halisi uliowekwa na wanahisa.”

Ushauri huo ulitokana na hoja ya Kampuni ya Hunton and Williams kwamba ujenzi wa mitambo ya IPTL kwa kutumia mtaji wa Sh 50,000, haileti mantiki katika uhalisia wake kinyume na ilivyoainishwa na kampuni ya Mkono, kwamba mtaji wa wanahisa ni Sh 50,000 na hivyo tozo ya uwekezaji ukokotolewe kwa kutumia mtaji huo.

Katika taarifa ya Serikali iliyosomwa Bungeni na Profesa Sospeter Muhongo, alibainisha kuwa Oktoba 9, 2013, Tanesco na IPTL walikutana na kufanya majadiliano yaliyowezesha kukubaliana malipo stahiki kwa IPTL.

Katika kikao hicho, IPTL madai yao yalikuwa Sh bilioni 370 lakini baada ya majadiliano na Tanesco, walikubaliana madai halisi ya IPTL ni Sh bilioni 274.56.

Profesa Muhongo alisema baada ya makubaliano hayo, Tanesco ilipaswa kulipa fedha hizo, lakini walipokwenda katika akaunti hiyo ya Escrow ambapo Tanesco ilikuwa ikilipa fedha za matumizi ya umeme wa IPTL na tozo ya uwekezaji, walikuta Sh bilioni 182.77 tu, ambazo zililipwa IPTL.

Kutokana na hali hiyo, mpaka sasa IPTL inaidai Tanesco Sh bilioni 123, ambazo ni nyingi kuliko kodi ambayo TRA inaidai IPTL, ya Sh bilioni 26.9.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: