KIVUMBI CHA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA TANZANIA CHAWAKA MOTO 2014.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro (SAPC), Leonard Paulo (wa pili kushoto)akiongoza askari kufanya mazoezi kuwaweka tayari kulinda usalama katika uchaguzi unaofanyika leo. Picha na Juma Mtanda.
Dar es Salaam. Watanzania leo wanaingia kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofunikwa na malalamiko kadhaa ya ukiukwaji wa kanuni, huku chama tawala CCM na wapinzani wakitambiana kushinda.
Tangu ulipotangazwa rasmi Septemba mwaka huu hadi jana, Jumamosi ambayo ilikuwa siku ya kufunga kampeni, mchakato wa uchaguzi huo umegubikwa na mapingamizi na dosari lukuki, mambo ambayo vyama vya siasa vya upinzani vinadai yataufanya usiwe huru na haki.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ukiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vinatuhumu kuwepo kwa faulo na uvunjaji mkubwa wa kununi uliofanywa na Serikali ili kukipa ushindi wa bure chama tawala, CCM.
Wagombea waenguliwa
Uchaguzi huo unafanyika leo, huku kukiwa tayari na wagombea 228 wa Chadema ambao wameenguliwa katika nafasi mbalimbali walizokuwa wakigombea kutokana na sababu tafauti.
Hadi kufikia Ijumaa iliyopita, kulikuwa na mapingamizi 257, ambayo hayajatolewa uamuzi jambo ambalo limewaacha baadhi ya wagombea katika giza nene la kutokujua hatma yao.
Tatizo la wingi wa mapingamizi na dosari nyingine ziliilazimu Chadema kumwandikia barua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa nyakati tofauti ili aweze kuchukua hatua zaidi.
Desemba Mosi mwaka huu, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe aliainisha kasoro kadhaa za uchaguzi huo ikiwamo sehemu A ya maelezo ya mgombea katika kipengele cha jinsi baadhi ya wagombea walioondolewa kutokana na kuandika kwa maneno, badala ya kukata maneno yaliyopo kwenye mabano ya me/ke.
Barua nyingine ya chama hicho kwa Pinda, iliandikwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa Novemba 14 mwaka huu. Katika barua hiyo Slaa alielezea baadhi ya dosari zilizopo katika Mwongozo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuzifanyia kazi.
Majibu ya Serikali
Mratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutoka Tamisemi, Denis Bandisa alisema kuwa wana taarifa ya mapingamizi mbalimbali katika mchakato wa uchaguzi huo, lakini mengi yameshughulikiwa na Kamati za Rufaa za Wilaya.
Bandisa aliwataka baadhi ya wagombea ambao hawakuridhika na uamuzi wa kamati hizo kwenda mahakamani kwa hatua zaidi, hasa baada ya Serikali kuwa tayari imetoa mwongozo wa taratibu wa rufaa.
“Kwa kifupi tumebaini pingamizi nyingine hazikuwa na ushahidi wowote wa kuthibitisha uhalali wake ni mambo yanayosababishwa na siasa. Sisi tunaendelea na utaratibu tuliouweka na uchaguzi utafanyika kwa tarehe ile ile iliyopangwa,” alisema Bandisa.
Mwamko ukoje?
Mwamko wa kujiandikisha kupiga kura mwaka huu ni hafifu. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tamisemi, Khalist Luanda alisema ni asilimia 62 pekee ya watu ndiyo waliojitokeza kujiandikisha kupigakura.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa watu 11,491,661 wamejiandikisha kupiga kura leo, tofauti na idadi ya watu 18,587,742 waliotarajiwa na Tamisemi kwamba wangejiandikisha.
Luanda alisema maandalizi yote kwa ajili ya uchaguzi wa leo yapo tayari na kwamba watu milioni 18.6 waliokuwa wakitarajiwa ni asilimia 42 ya Watanzania wote kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya mwaka 2012.
Wanasiasa watambiana ushindi
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Nape Nnauye alisema kuwa wamejipanga vizuri kwa uchaguzi huo na kwa hakika watashinda kwa kishindo.
“Tumejipanga vizuri kwa sababu tunakwenda kwenye uchaguzi tukiwa na mtaji wa kutosha. Mtaji wetu wa kwanza ni asilimia 96 ya kura za wananchi tuliyoipata mwaka 2009, ambapo wapinzani walibaki na asilimia zilizobaki,” alisema Nnauye.
Aliendelea kueleza kuwa, mtaji wa pili ni utekelezaji wa mambo waliyoahidi kwa wananchi mwaka 2009.
“Huduma za barabara, maji, elimu, afya. Vijiji vingi hivi sasa vimeungwanishwa na umeme, visima vimechimbwa, zahanati zimejengwa, madaktari wamepelekwa, walimu wameongezwa na maabara zimejengwa,” alieleza Nnauye.
Aliutaja mtaji wao wa tatu kuwa wagombea wake kupita bila kupinga katika mitaa zaidi ya 600 na wakipita zaidi ya vijiji 2,800 vitongoji zaidi ya 26,000.
“Katika mazingira hayo maana yake ni moja tu, kwamba ushindi wetu uko wazi…hatuna shaka kwa sababu tuna asilimia kubwa zaidi ya wapinzani.
“Tumeweza kupita bila kupingwa kwa sababu wapinzani hawakuwa na mgombea katika maeneo hayo au mahali pengine inawezekana walikuwa na mgombea ambaye hakuwa na sifa hivyo akaondolewa,”alifafanua Nnauye.
Alisema kwa picha hiyo ni dhahiri kuwa hata malalamiko yanayotolewa na baadhi ya watu kwamba kuna upendeleo kwa CCM, hayana hoja ya msingi.
Baadhi ya vyama havikupeleka wagombea kwenye uchaguzi huo katika baadhi ya maeneo na Nnauye akisema kwa hali hiyo ni lazima mgombea wa CCM ashinde.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Shaweji Mketo alisema chama hicho kimejipanga vizuri kwa ushindi wa kishindo, lakini kinasikitika kwamba CCM na Serikali yake imejipanga kuwahujumu.
“Sisi tumejipanga kwa ushindi wa kishindo, lakini niseme tu kwamba CCM na Serikali yake imejipanga kutuhujumu. Imejipanga kutumia wanajeshi na Jeshi la Polisi kuuhujumu upinzani na tayari nimemwandikia barua Waziri Mkuu (Pinda) ili afanyie kazi suala hilo,” alisema Mketo.
Kwa mujibu wa Mketo, usiku wa kuamkia jana, wanajeshi waliwakamata viongozi wanne wa chama hicho huko Tandahimba mkoani Mtwara, kuwapiga na kuendeleza vitisho kwamba watawashughulikia wafuasi wa chama hicho cha upinzani katika uchaguzi huo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika amejigamba kuwa chama hicho kikubwa cha upinzani kitajizolea viti vingi vya nafasi ya uenyekiti na wajumbe nchi nzima.
“Hatuna mchezo sisi, tumejipanga kushinda maeneo mengi sana na leo (jana) tunamalizia moto wetu majukwaani,” alisema Mnyika muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kwenda kwenye kampeni.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment