Juma Mtanda, Morogoro.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika Manispaa ya Morogoro, umewataka wananchi kuwachagua wagombea watakaosimamishwa na vyama vinavyounda umoja huo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuiondoa madarakani CCM.
Umoja huo umesema chama hicho kinachotawala, kimeshindwa kutatua kero za wananchi na kwamba hakipaswi tena kupewa fursa ya kuondoza serikali.
Wito huo ulitolewa jana na viongozi wa Ukawa walipokuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti katika uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika nchini kote Desemba 14 mwaka huu.
Katika uzinduzi huo uliofanyika katika Kata ya Kiwanja cha Ndege mjini hapa, viongozi hao walidai kuwa badala ya kushughulikia kero za wananchi, viongozi wa CCM, wamejikita katika ufisadi wenye maslahi binafsi na familia zao.
Mwenyekiti wa CUF katika Manispaa ya Morogoro, Abeid Mlapakolo alisema wakati sasa umefika kwa wananchi kuiadhibu CCM kwa kuwakataa wagombea wa chama hicho katika uchaguzi huo utakaotoa mwelekeo ya uchaguzi mkuu wa mwakani.
“CCM ni mafisadi na wafujaji wakubwa wa mali za umma, haishangazi kuona viongozi wa kijiji ama taifa wakishindana katika kutafuna mali za Watanzania huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma muhimu za kijamii,”alisema Mlapakolo.
Mlapakolo alisema kitendo cha Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kuingia katika kashfa ya kuingiziwa mabilioni ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, ni moja ya mifano ya namna viongozi wa CCM wasivyojali maisha ya walalahoi.
Katibu wa Ukawa katika Manispaa ya Morogoro, James Mkude alisema Ukawa imebaini mbinu chafu za CCM ya kutaka kushinda uchaguzi huo kwa kishindo.
Alidai kuwa chama hicho kinachotawala, kimekuwa kikiwaanda wapiga kura nyakati za usiku wa manane, kama mkakati wake wa kupata ushindi mkubwa.
“Tumebaini siri ya CCM ya kutaka kujipatia ushindi wa kishindo Desemba 14 katika uchaguzi huu. Wapanga usiku wa Desemba 13 mwaka huu wapigakura wao watakabidhiwa karatasi tano ambazo tayari watakuwa wamepiga tiki za wagombea wa CCM,”alisema Mkude.
0 comments:
Post a Comment