Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova.
Jeshi la Polisi limemtia mbaroni Harab Mtopu (44), mkazi wa Mbagala, jijini Dar es Salaam aliyekuwa akijifanya katibu wa Rais Ikulu na kuwatapeli watu kadhaa.
Mtuhumiwa huyo alikuwa akijitambulisha kama Prosper Mbena ambaye ni Katibu halali wa Rais.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa jana na amekuwa akifanya utapeli kwa watu mbali mbali.
Alisema polisi ilipata taarifa kutoka kwa raia mmoja ambaye alitapeliwa na mtuhumiwa huyo Sh. 300,000 na iliamua kushirikiana na Ikulu kumnasa mtu huyo.
Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akiingia Ikulu kwa ajili ya kusaidiwa shida zake na kuamua kutumia mwanya huo kuwadanganya watu.
“Kitendo cha kuingia Ikulu na kusaidiwa shida zake amekuwa akijiita yeye ni katibu wa rais Kikwete na huwa anakuja na watu hadi hapo Ikulu na kuwaacha nje ya jengo hilo na kisha kuingia ndani,” alisema Kova
Aliongezea kuwa “Kitendo cha kuingia na kutoka Ikulu kinamuingizia fedha na kuendelea kuwatapeli wananchi huku akitumia cheo cha katibu wa rais,” alisema.
Kamanda Kova alisema mara ya mwisho alimtapeli mwananchi mmoja Sh. 300,000 kwa madai kuwa atamsaidia kwa Rais Kikwete.
Alisema raia huyo aliamua kutoa taarifa kituo cha polisi ambapo jeshi la polisi lilimuwekea mtego wa Sh. 250,000 na kufanikiwa kumkamata.
“Tulimtegeshea 250,000 tukamwambia amuite aje tena kuchukua mzigo wake uliobakia, huu mzigo wa pili ndiyo tuliomkamatisha na hizi fedha zilikuwa za polisi,” alisema Kamanda Kova.
Aidha, Kamanda Kova alisema mtuhumiwa ameshafanya utapeli wa aina hiyo kwenye wizara mbalimbali ikiwamo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Wizara ya Maji.
Alisema ni marufuku kwa watu kutumia ofisi za serikali kufanya utapeli kwani watakaobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Alisema kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakirandaranda kwenye wizara mbalimbali kila siku bila sababu za msingi.
Alisema kwa yoyote ambaye atamuona mtu anazurura kwenye ofisi atoe taarifa kwa jeshi la polisi ili achukuliwe hatua.
Kova alisema jeshi hilo linaweka kikosi maalum katika wizara mbali mbali ili kubaini matapeli na wanaozunguka bila kuwa na kazi maalumu.
Alisema mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu ili kujibu mashtaka yanayomkabili. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment