BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

JK KUSAINI MISWADA INAYOLALAMIKIWA IKIWEMO YA SHERIA YA MAKOSA YA MITANDAO.


 

Rais Jakaya Kikwete akitekeleza moja ya majukumu yake ndani ya ndege hivi karibuni.


Ikulu imesema Rais Jakaya Kikwete atasaini Miswada yote ya Sheria ya Makosa ya Mitandao na ule wa Takwimu ya Mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge katika mkutano wake wa 19, licha ya wadau kumuomba asifanye hivyo. 



Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema anavyojua ni kuwa mchakato wa muswada mpaka unatungwa sheria na Bunge hauna matatizo.

Hivyo, akasema Rais hawezi kuacha kusaini, bali atasaini na kwamba, kama kuna matatizo mengine baada ya hapo, milango ya mazungumzo juu ya marekebisho iko wazi, kwani sheria zote hurekebishwa.

“Nasema Rais atasaini (muswada huo) kwa sababu imepitia taratibu zote. Bunge limefanya kazi yake, limepitisha muswada. Sasa ili muswada ule ukamilike kuwa sheria, mheshimiwa Rais atausaini kusudi uwe sheria,” alisema Rweyemamu.

Alisema atasaini Muswada wa Makosa ya Mitandao kwa kuwa ni sheria nzuri, kwani ina maudhui mazuri.

Aliwataka wadau kuelewa kwamba, sheria hiyo haikutungwa kwa ajili ya kudhibiti uhuru wa habari, vyombo vya habari na waandishi wa habari.

Alisema usalama wa nchi lazima uwepo kwanza kabla ya kutetea na kulinda uhuru wa habari.

“Mimi nilifikiri lazima tuwe salama ndiyo tuzungumze habari,” alisema Rweyemamu.

Aliwaomba wanahabari kama hawataki kuiunga mkono sheria hiyo, ni heri wakanyamaza, kwani siyo lazima kuunga mkono.

“Lakini tunavyoendelea kueleza kama vile sheria mbaya, ni sheria inayotaka kuzuia uhuru wa habari, haiingilii uhuru wa habari, ni sheria ya kulinda jamii,” alisema Rweyemamu.

Aliongeza: “Haiwezekani jamii ikawa exposed, siye tukakaa tumenyamaza kwa kisingizio cha habari, haiwezekani. Ni kwamba, kuna miss used (matumizi mabaya) ya mitandao na nyie mnaijua zaidi kuliko mimi. Na serikali mimi nadhani ukiniuliza kwa maoni yangu tumechelewa.”

Kuhusu sheria ya haki ya kupata na uhuru wa vyombo vya habari, aliwaomba wadau kuunga mkono mchakato, ambao serikali inaendelea nao.

Alisema serikali haina sababu ya kuzuia haki na uhuru huo na kwamba, imeamua kuendelea na mchakato huo kwa kuwa sheria za sasa za habari siyo rafiki sana na kwamba, hata wanahabari wanalijua hilo.

“Na ndiyo maana serikali tangu mwanzo ikasema jamani hebu tutunge sheria inayotoa space zaidi kwa uhuru wa waandishi inayolinda zaidi uhuru wa waandishi wa habari, inayotoa mwanya salama zaidi kusudi waandishi wa habari wafanye kazi zao kwa mazingira mwafaka na bora zaidi,” alisema Rweyemamu.

Alisema mchakato huo haukuanza leo na kusema ndiyo sababu muswada huo ukapelekwa bungeni chini ya hati ya dharura.
Rweyemamu alisema kupeleka muswada chini ya hati ya dharura ni utaratibu unaokubalika kiserikali na bunge na kwamba, sheria hiyo ilianza kujadiliwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Alisema mchakato wa kwanza wa sheria ulianzishwa na serikali na wadau wengine pamoja na washirika wa maendeleo.

Rweyemamu alisema marehemu Jaji Francis Nyalali ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha mchakato huo na kwamba alipofariki, ulichukuliwa na Jaji Joseph Warioba.

Alisema ilishangaza kuona wanahabari wakifunga plasta midomoni, kwani lilikuwa ni swali gumu kujua namna gani wangeweza kueleza malalamiko yao, huku wakiwa wamefanya hivyo.

Rweyemamu alisema hali hiyo ilisababisha muswada huo kukwama na kwamba, hivi karibuni pia waliibuka tena na kuupigia kelele na kusababisha kwa mara nyingine kukwama kujadiliwa na Bunge.

“Mimi ombi langu ni hivi, huu mchakato tuunge mkono kwa sababu mchakato huu utazaa sheria bora zaidi. Tusipouunga mkono huu, tutabaki na sheria zilezile za miaka yote iliyopita. Na ni kama nilivyosema inaweza isiwe sheria rafiki sana kwa shughuli yetu,” alisema Rweyemamu.

Awali, akifafanua sababu za Ikulu kutokutoa taarifa kuhusu safari ya Rais Kikwete nchini Jordan, Jumamosi ya wiki iliyopita, alisema walifanya hivyo kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na nchi hiyo pamoja na nchi nyingine zilizoalikwa katika mkutano wa siku moja kuangalia namna gani dunia wanavyoweza kukabiliana na tatizo la ugaidi katika dunia yao.

Alisema safari ya Rais Kikwete ilikuwa ni kuitikia mwaliko wa Mfalme wa Jordan, Abdullah bin Hussein, kuungana na viongozi wengine wakuu duniani na wakuu wa taasisi na mashirika yanayohusika na usalama, ulinzi na yanayopambana na ugaidi kufanya mkutano huo.

Rweyemamu alisema katika makubaliano hayo, Tanzania, Jordan na nchi nyingine zilizoalikwa walikubaliana mkutano huo ubaki siri wakati unaandaliwa, unafanyika na baada ya kumalizika ili kuwezesha mazingira bora ya mkutano huo. CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: