MABASI YA ABIRIA YAPANGA KUFANYA MGOMA TENA KWA NCHI MZIMA.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra)
Siku 17 baada ya madereva wa mabasi mchini kugoma na kutikisa nchi, Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani (Taboa) kimetangaza mgomo mwingine nchi nzima.
Mgomo wa Aprili 9, mwaka huu uliodumu kuanzia alfajiri hadi saa 7:00 mchana ulitikisa nchi na kuwaathiri abiria wengi waliokuwa wanasafiri kwenda maeneo mbalimbali ya nchi.
Jana Taboa walitangaza kusitisha utoaji huduma kuanzia kesho ikiwa ni hatua ya kupinga nauli mpya za mabasi zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Kufuatia hali hiyo, Taboa kimewataka mawakala kutokatisha tiketi kuanzia leo kwa abiria hadi hapo Sumatra itakapotoa taarifa za kuruhusu nauli ya zamani ziendelee kutumika.
Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, alitoa taarifa hiyo jana wakati akitoa majumuisho ya mkutano mkuu wa dharura uliojumuisha wadau wa usafirishaji.
Mkutano huo ulikuwa na ajenda kuu tatu ambazo ni ajali za barabarani, nauli mpya zilizotangazwa na Sumatra, madaraja ya mabasi, mgomo wa madereva na vituo vya kubadilishia madereva wanaokwenda umbali mrefu.
Mrutu akisoma maazimio hayo baada ya kumalizika kwa majadiliano hayo, alisema sababu iliyotolewa na Sumatra kushusha nauli kutokana na bei ya mafuta kushuka siyo kigezo muhimu bali ni shinikizo kutoka kwa wanasiasa.
“Kesho kutwa (kesho) hakuna gari ambalo litatoka kituo cha mabasi Ubungo kwenda mkoani na kama tutapigwa mabomu tupigwe, ila msimamo wetu uko pale pale wa kutotoa magari hadi Sumatra watakapotoa tamko la kutaka nauli za awali ziendelee kutumika,” alisema.
Kuhusu ajali, alisema kutokana na kukithiri kwa ajali za mabasi, wanakubaliana na utaratibu uliowekwa na serikali wa madereva kubadilishana wanaokwenda masafa marefu katika vituo ambavyo vitatengwa ili kupunguza ajali hizo.
KILOMITA 80 KWA SAA
Mrutu aliagiza madereva wote watumie mwendo wa kilomita 80 kwa saa na wazingatie sheria za usalama barabarani na watakaokiuka sheria hizo wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema kuanzia Mei mosi, mwaka huu wataanza kutumia vituo maalum vya kubadilishia madereva kwenye mabasi ya masafa marefu kwa muda wa miezi mitatu kwa majaribio.
Vituo hivyo ni Singida mjini, kwa mabasi ya Dar es Salaam kwenda Mwanza, Bukoba, Kahama; na kituo cha Morogoro kwa mabasi yanayokwenda mikoa ya nyanda za juu kusini.
Uamuzi huo umechukuliwa kutokana na mapendekezo ya Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani, kubainisha kuwa chanzo cha ajali kwa mabasi yaendeyo masafa marefu ni uchovu wa madereva.
Mrutu aliwataka wamiliki wa mabasi kuhakikisha madereva wao wanazingatia taratibu na sheria zilizowekwa na Jeshi la Polisi pamoja na Sumatra ili utoaji wa huduma uweze kwenda vizuri.
Alisema madereva ambao wameanza tabia ya kuwachafua wamiliki wa mabasi kwamba wamekuwa wakielekezwa kwenda mwendo wa kasi ili kuwahi abiria watawachukulia hatua kwasababu suala hilo siyo la kweli.
“Mimi ninunue gari la mamilioni halafu nimlazimishe dereva aende mwendo kasi ni kitu ambacho hakiniingii akilini inamaana sina uchungu na gari yangu,” alisema Mrutu
Alisema mwendokasi wa kilomita 80 kwa saa, uwepo wa vituo vya kubadilisha madereva wa mwendo mrefu na kukoma kwa urasimu miongoni mwa askari polisi kuwa suluhisho la ajali za barabarani nchini.
Mrutu alisema katika utafiti wao wamebaini kuwa chanzo kimojawapo kinachosababisha kutokea kwa ajali nchini ni ubovu wa miundombinu ya barabara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji wa maadili iliyopewa jukumu la kuchunguza tatizo la ajali nchini, Abdulrazack Kimaro, alisema ajali za barabarani zinasababishwa na mwendokasi.
Alisema katika uchunguzi wao wamebaini hakuna hata dereva mmoja anayezingatia sheria za usalama za barabrani ingawa Sumatra na askari wa kikosi cha usalama barabarani wanakuwapo bali kinachofanyika ni kumalizana kwa kupeana ‘kitu kidogo’.
Abdulrazack alisema wao kama wamiliki wa mabasi hawako tayari kuendekeza madereva wanaokwenda kinyume cha sheria, hivyo kila mmiliki kwa muda wake atoe somo kwa dereva wake juu ya makubaliano hayo ili kudhibiti ajali.
Alisema madereva wanatakiwa kusimamiwa kikamilifu kwenye utendaji wao na kwamba kila mmiliki anapaswa kuwasilisha majina ya dereva wake na vyeti, leseni kwa Taboa ili kuthibitisha ufanisi wake kwa kazi anayoifanya.
Naye Katibu wa Wamiliki wa Mabasi Mkoani Kigoma (Kiboa), Hussein Kalyango, alisema serikali inatakiwa kuyafanyia marekebisho baadhi ya mambo yakiwamo kanuni za usafirishaji zinazomkandamiza mmiliki zaidi huku zikimwacha dereva nje ya lawama mfano chanzo cha ajali.
Kalyango alisema utaratibu wa sheria za Sumatra zinamlenga mmiliki wa basi kwa utovu wowote wa basi ambao anaufanya dereva.
“Tunaiomba Sumatra ibadilishe sheria makosa anayofanya dereva adhibitiwe dereva na hata kuchukuliwa sheria za zaidi na tunatakiwa kushirikiana Sumatra, polisi na sisi kumaliza ajali hizi za barabarani,” alisema.
SOURCE: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment