Juma Mtanda, Pascalina Kidyalla, Morogoro.
Mtoto mchanga wa wiki moja na nusu ameokotwa na watembea kwa miguu baada ya kutupwa kichakani na mtu asiyefahamika majira ya saa 1:30 usiku katika eneo la shule ya msingi Mafiga B Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mjini hapa, Mwenyekiti wa mtaa wa CCM Kata ya Mafiga Manispaa ya Morogoro, Hassan Faraji (52) alisema kuwa mtoto mchanga wa wiki moja na nusu ameokotwa baada ya kutupwa kichakani majira ya saa 1:30 usiku.
Tukio hilo lilitokea April 21 mwaka huu katika kichaka kilichopo jirani na kibao cha shule ya msingi Mafiga B kando ya barabara kuu Mzumbe-Mjini baada ya wapitanjia waliotelemka kutoka kwenye daladala kusikia sauti ya mtoto mchanga akilia katika kichaka.
Faraji alisema kuwa wapiti njia hao iliwalazimu kusogea karibu na inapotoka sauti na kuona mtoto mchanga akiwa ameviringishwa khanga mwilini huku pembeni yake kukiwa na mfuko wa rambo uliowekwa nguo mbalimbali za mtoto.
“Kuna wasamaria wema walifika nyumbani kwangu na mtoto mchanga majira ya saa saa 1:45 usiku na walinieleza kuwa mtoto huyo wamemuokota kichakani na mazingira yanaonyesha ametupwa na mtu asiyefahamika.”alisema Faraji.
Aliendelea kueleza Mwenyekiti huyo kuwa baada ya kumpokea mtoto huyo aliongozana na wasamaria wema hao Joseph Chacha na Ramadhan Masabo hadi kituo cha polisi kabla ya kufikishwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro.
“Ni tukio la kinyama na linalopaswa kupigwa vita katika kada mbalimbali ndani ya jamii zetu, kwanini umtupe mtoto ambaye hana hatia?.alihoji.
Aliendelea kuhoji, Hebu fikiria mwanamke aliyemzaa mtoto huyu amebeba mimba miezi tisa alafu leo hii anamtupa mtoto.?”
Mkazi wa kata ya Kichangani Manispaa ya Morogoro, Ayubu Seif alisema amesitishwa na kitendo cha baadhi ya wanawake kutupa ama kutelekeza watoto wachanga mara baada ya kujifungua.
“Serikali inapaswa kutoa adhabu kali kwa wale wanaobainika kutupa ama kutelekeza watoto wachanga mara baada ya kujifungua kwani vitendo hivyo vimekithiri mno na hawana uoga wa unyanyasi na ukatili kwa watoto wasio na hatia.”alisema Seifu.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro Dk. Rita Lyamuya alieleza kuwa April 21 majira ya saa 2:15 usiku walipokea mtoto mchanga wa kiume hospitalini hapo.
Dk Lyamuya alisema kuwa baada ya kumpokea mtoto huyo alianza kupewa huduma za uchunguzu wa afya yake sanjari na kumpa jina la Bahati na kueleza kwa sasa yupo chini ya uangalizi maalumu wa madaktari katika hospitali hiyo.
0 comments:
Post a Comment