BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAAJABU YA HIFADHI YA NGORONGORO, UKOO WA MOLLEL KATIKA JAMII YA WAMASAI ETI WANA UNDUGU NA WANYAMA.


Arusha. Licha ya umaarufu wake, Hifadhi ya Taifa Ngorongoro iliyopo mkoani Arusha ina mambo mengi ya kuvutia yanayoifanya muda wote kuwa ya kipekee duniani.

Upekee huo unatokana na mfumo wa maisha ya binadamu yanavyohusiana moja kwa moja na maisha ya wanyama.


Siyo jambo geni kusikia kuwa binadamu hasa wa jamii ya Kimasai wanaoishi kwenye eneo la hifadhi hiyo wanaishi na mifugo yao katika maeneo yaliyo na wanyamapori bila kudhuriana.


Hata hivyo, jambo linaloweza kuwa geni na la ajabu ni baadhi ya koo za Kimasai ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kuelezwa kwamba ‘zina udugu’ na baadhi ya wanyama.


Licha ya maelfu ya watalii kutembelea hifadhi hiyo ili kufaidi na kuona wanyama waliosheheni Ngorongoro, kasi ya wageni hao pia ni kubwa kutembelea jamii ya Wamasai inayoishi eneo hilo ili kujua mila na tamaduni zao na namna wanavyoweza kuishi na wanyama.


Hakika hakuna ubishi kwamba Wamasai wa Ngorongoro na wanyama katika Hifadhi ya Ngorongoro ni marafiki.


Ukweli huo unakwenda mbali zaidi na kubainisha kuwa hata baadhi ya koo za Kimasai, ‘zina udugu’ na wanyama kwa kadri ya majina yao.


Inaelezwa kuwa kuna ukoo wenye ‘udugu’ na nyoka, mwingine simba hata wanyama wengine.


Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Vincent Mbilika anaeleza kuwa zipo koo ambazo majina yao yana uhusiano na wanyama hata wadudu.


Mfano; ukoo wa Mollel unatajwa kuhusiana na faru, Laitayok unahusiana na tembo na mbogo, nyani na tumbili wanahusianishwa na ukoo wa Ilukumai, ambao fisi na nyoka wanaelezwa kuwa na uhusiano na ukoo wa Illtarru-sero.


Mbilika anaeleza kuwa katika koo iliyo ndugu na nyoka, jamii hiyo ikikuta nyoka ndani ya nyumba yao haipambani naye tofauti na ilivyo kwa jamii nyingine, zinachofanya ni humwekea maziwa kwa kumwagia, naye huyanywa.


“Baada ya kupewa maziwa, hutoa ndimi zake na kulamba maziwa kisha hutoka ndani ya nyumba bila kudhuru mtu, tena anatokea mlangoni. Hivyo, koo yenye udugu na nyoka hata kama ni mkubwa kiasi gani, ikiwa ameingia ndani ya nyumba, hata kufikia hatua ya kulala kitandani na mtoto mdogo, hauawi,” anasema Mbilika.


Anasisitiza kuwa koo iliyo na udugu na nyoka ni marufuku kuua nyoka.


“Huu ni utalii wa aina moja ambao unaweza kuwapo sehemu nyingi nchini na hili ni kwa wanyama wote. Ndiyo sababu Wamasai hawali wanyamapori,” anasema.


Katika juhudi zake kuhakikisha wananchi wanashiriki masuala ya utalii hasa wa mila na utamaduni, mwaka 1988 NCAA ilianzisha mradi unaohusisha utalii huo pamoja na kuanzisha maboma ya Kimasai yanayotumika kwa utalii.


Kuanzishwa kwa maboma hayo imekuwa ni faraja kwa wenyeji wa Ngorongoro, kwani sasa yanawapatia fedha kutoka kwa watalii ambao hutembelea kujifunza mila mbalimbali na kuchezewa ngoma.


Maboma saba
Seneto ni moja ya maboma saba yaliyo katika eneo la NCAA, yote yakiwa ya kitamaduni.


Katika maboma hayo, kuna nyumba ndogo zisizopungua 24 ambazo mtalii huweza kuingia na kujifunza mambo mbalimbali ya asili ya Kimasai.


Kiongozi wa Boma la Seneto, Kimati Sabore anasema kupitia maboma hayo, wameweza kuingiza fedha nyingi.


Anasema kuwa kwa sasa katika boma hilo ambapo watakaa kwa miaka miwili, kuna watu 124 wanaotoka Kata ya Ngorongoro.


Sabore anasema katika vijiji vitatu vya kata hiyo, wamechukuliwa kina mama wanane kutoka kila kitongoji na morani 18, huku wengine wakialikwa kupeleka huduma mbalimbali kwenye boma na kusaidia kuimba.


Anasema kuwa wanapata fedha kwa watalii, wanaoingia katika boma hilo kutazama utamaduni na kwa kila gari linaloingia, hulipa Sh20,000.


“Wakija huku ndani, wanaona tamaduni zetu, watachezewa ngoma na kununua vitu mbalimbali vya kitamaduni kama shanga na mapambo ya asili,” anasema.


Anasema baada ya kukaa katika boma hilo, kwa miaka miwili, hugawana fedha na kununuliana mifugo na kupisha kundi jingine. “Kwa utaratibu huu, ambao unalenga kaya maskini, walau kila familia hupata nafasi ya kuishi katika boma hili na baada ya miaka miwili hupata fedha za kujikimu” anasema Sabore.


Hata hivyo, anasema kuwa kuna changamoto zinazowakabili katika miaka ya karibuni, ambazo ni pamoja na kusambaa kwa biashara ya vitu vya asili ya Kimasai, hivyo kupata watalii wachache wanaowatembelea.


Kiongozi wa kina mama katika boma hilo, Zeena Namayai anaeleza kuwa kila siku asubuhi baada ya kuamka huandaa vyakula vya kitamaduni na kujipanga ili kuwaimbia watalii.


Anasema pia hujiandaa kutoa maelezo kwa watalii juu ya tamaduni zao, pia kuuza vitu mbalimbali ambavyo huwa tayari vimewekwa ndani ya uwanja wa boma la asili.


“Kwa jumla, maboma haya yanatusaidia kuendesha maisha yetu, kusomesha watoto na tunaipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kubuni mradi huu,” anasema na kuongeza: “Hapa tunaishi kama ndugu, ndiyo sababu kuna shule ya muda hapa. Kwa miaka miwili watoto wadogo huweza kusoma chekechea na baadaye tukirudi nyumbani, wanaendelea na masomo shule ya msingi.”


Wavuna mabilioni
Kaimu Meneja wa Utalii wa NCAA, Asantaeli Merita anasema kuwa utalii wa utamaduni umesaidia kuboresha maisha ya wenyeji wa Ngorongoro.


Anasema kuna utalii wa aina mbalimbali ambao unahusisha moja kwa moja wenyeji wa Ngorongoro kupitia NCAA.


“Tumeanzisha utalii wa kutumia punda kwa watalii wanaotembelea baadhi ya maeneo kuelekea Kreta ya Embakai,” anasema


Anasema wenyeji wanatumia punda mmoja, kubeba mizigo na kusindikiza watalii na kwa wastani kwa kila safari moja hujipatia kiasi cha Sh35,000.


Anasema kupitia maboma ya kitalii Ngorongoro sasa kuna maboma 7saba ambayo yanafanyakazi na mwaka uliopita kiasi cha Sh77 milioni kilitolewa kwa maboma hayo.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: