UTAJIRI, UONGOZI HAVIJII KWA VIUNGO VYA ALBINO.
Picha ya maktaba.
Toleo letu la jana, tulichapisha habari katika ukurasa wa 11 yenye kichwa cha habari `Viongozi watatokana na Mungu si viungo vya albino.'
Habari hiyo ilikakariwa kutoka kwa Askofu wa Kanisa la Pham Kanda ya Kati, Julius Bundala, alipokuwa akifungua mkutano wa Neno la Mungu uliofanyika katika viwanja vya Kanisa la Pham Bethel, Nzuguni mkoani Dodoma Jumapili iliyopita.
Askofu Bundala alisema viongozi watakaochaguliwa na Watanzania kuongoza nchi kupitia uchaguzi mkuu ujao, ni wale watakaochaguliwa na Mungu mwenyewe na siyo kwa njia za kishirikina za kuwaua watu wenye ulemavu ya ngozi (albino) ili kupata uongozi.
Alisema kamwe Tanzania haitaongozwa na viongozi wanaoamini ushirikina kwa kukata viungo vya albino na kuvipeleka kwa waganga wa kienyeji kwa ajili ya kutoa kafara ili wapate uongozi.
Askofu huyo alisisitiza kuwa viongozi wa taifa hili watapatikana kwa kuchaguliwa na Mungu mwenyewe ili nchi iendelee kuwa na amani, upendo na ushirikiano badala ya kuongozwa na watu hao ambao wamepita kwenye nguvu za giza chini ya masharti ya shetani ambaye siku zote hapendi watu waishi kwa utulivu.
Aidha, aliwataka Watanzania kuwa makini na wanasiasa wanaojishirikisha na imani za kishirikina kwa lengo la kutaka waongoze nchi.
Kauli ya Askofu Bundala inapaswa kuungwa mkono na watu wote wapenda amani na wanaothamini maisha ya kila binadamu.
Mauaji, utekaji na ukataji wa viungo vya albino, limekuwa ni tatizo hapa nchini katika miaka ya karibuni na kuleta sifa mbaya kwa Tanzania inayosifika kuwa ni kisiwa cha amani.
Tatizo hili lilianza kidogo kidogo mwanzoni mwa miaka 2000 lakini kadiri siku zinavyosonga mbele, ndivyo linavyozidi kuongezeka.
Mpaka sasa, takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi 70 wamekwisha kuuawa huku wengine kadhaa wakikatwa viungo vya miili yao na kuachwa walemavu wa kudumu, hali inayowalazimu kubaki tegemezi kwa ndugu zao ama jamii kwa ujumla.
Mauaji na ukataji wa viungo vya albino, huhusishwa na imani za kishirikina.
Yapo madai ama dhana potofu miongoni mwa wachache kwamba viungo vya albino humfanya mtu kuwa tajiri ama kupata nafasi ya uongozi anayoiwania.
Uovu huu unajidhihirisha katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu kote nchini.
Katika kipindi hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu, kumekuwapo na matukio kadha wa kadha ya ama watu wenye ulemavu wa ngozi kuuawa, au kutekwa na kukatwa sehemu za viungo vya miili yao.
Kwa hakika ni jambo la kusikitisha sana kuona kwamba baadhi ya watu wenye nia ya kuwania madaraka mbalimbali ambao sisi tunaamini kwamba wameelimika, kuwa na dhana potofu vichwani mwao kuwa ili kufanikiwa azma hiyo, wanapaswa kudhulumu uhai wa binadamu mwenzao mwenye ulemavu wa ngozi yaani albino.
Kwa mtu msomi, tunatarajia kwamba atakuwa anafahamu kuwa mtu mwenye ulemavu wa ngozi, hana tofauti yoyote na binadamu mwingine isipokuwa kilichomsibu ni tatizo la kibailojia tu.
Kasoro hizo za kibailojia, humfanya binadamu ama awe albino au mweusi kupindukia lakini maumbile mengine yote pamoja na mahitaji mengine yote, hayatofautiani na binadamu mwingine ambaye kwa bahati njema hakukumbwa na kasoro za kibaiolojia.
Sasa inapokuwa hivyo, ni sababu zipi zinazomfanya mtu aache utu wake na kufikiria ama kutenda kosa la kutoa roho ya mwenzake? Je; anasukumwa na uroho wa madaraka ama wa kutaka kupata utajiri wa haraka haraka pasipo kuufanyia kazi?
Watanzania, tunapaswa kufahamu kwamba daima hakuna njia ya mkato katika kufikia mafanikio ya aina yoyote ile iwe ya kupata utajiri ama uongozi bali ni kwa njia halali ya kufanya kazi kwa bidii.
Mafanikio yoyote yale, hupatikana kwa njia ya kazi na kamwe hayaji kwa kumuua binadamu mwenzako ama kwa kutumia viungo vyake.
Tunawasihi wale wenye imani potofu kama hiyo waondokane nayo kwani mbali ya kulitia doa Taifa la Tanzania, lakini pia ni dhambi kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu alimuumba kila mwanadamu aishi hapa duniani kwa siku zake zote alizompangia.
Kwa bahati njema hata watawala wa hapa duniani, nao walitengeneza utaratibu wa kuhakikisha haki ya kila binadamu ya kuishi inalindwa kwa kutumia katiba za nchi zao.
Shime shime ndugu zetu, mauaji ya albino siyo dili bali ni kumkosea Mungu. Na wale wenye dhana hiyo potofu, wanapaswa kubadilika na kuachana nayo. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment