MAAJABU YA DUNIA JUU YA MTI WA MBUYU.
Mbuyu ni mti wa kipekee ambao kutokana na ukubwa wake usiolinganishwa na mti mwingine wowote ule duniani, umekuwa pia sehemu ya vivutio adimu vya utalii nchini.
Nchini Tanzania miti hii ya mibuyu inapatikana maeneo mengi, hasa mikoa ya kati, mikoa ya pwani ya Bahari ya Hindi pamoja na mwambao wote wa Ziwa Nyasa.
Kwa mfano, katika maeneo mengi ya mwambao wa Ziwa Nyasa, hasa katika kijiji cha Mkili, miti hii ya mibuyu inapatikana kwa wingi, lakini wakazi wake wengi wa eneo hilo hawana ufahamu kama miti hiyo inaweza kuwaongezea kipato kutokana na utalii.
Aidha, miti hiyo pia inapatikana kwa wingi katika Mkoa wa Mbeya, hasa kwenye bonde la mto Songwe wilayani Chunya, pamoja na barabara kuu ya Mbeya-Dar es Salaam, hasa katika maeneo ya mikoa ya Iringa na Morogoro.
Wataalamu wa sayansi ya mimea wanasema mti huo wa mbuyu una sifa na faida kemkem zinazoufanya mmea huo kuwa wa kipekee duniani.
Kwa mujibu wa wataalam hao, mbali na mmea huo kuweza kuvutia utalii, kila eneo la mti huo lina manufaa yake kwa binadamu na kiuchumi. Kwa mfano, matunda ya mti wa mbuyu, ambayo yanatoa ubuyu, hutumika kutengenezea kinywaji baridi cha juisi. Watoto na watu wazima hupendelea pia kula matunda ya mibuyu ambayo yanaelezwa kuwa na virutubishi vingi kwa afya ya binadamu.
Mtaalamu wa Ekolojia kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Mkoa wa Iringa, Godwel Olemeng’ataki, ameeleza kuwa kasha la matunda ya mbuyu, linaweza kutumika kwa mambo mbalimbali, ikiwemo kuhifadhia vitu vidogovidogo ndani ya nyumba, au huweza kutumika kama mapambo pia.
Olemeng’ataki anasema: “Kasha la matunda ya mbuyu, linaweza kutumika kama chombo cha kiasili kwa ajili ya kuwekea majivu ya sigara. Kasha linaweza kutengenezwa katika urembo mbalimbali na kuuzwa kwa watalii baada ya kuwa katika mtindo wa urembo wa kiasili,”
“Katika baadhi ya maeneo kama vile umaasaini, jamii ya kabila hilo hutumia makasha ya matunda ya mbuyu kama chombo cha kupakulia na kulia chakula na kunywea maji, huku kina mama wakitumia makasha hayo kuwanyweshea watoto maziwa na vitu nvingine.”
Kuna baadhi ya jamii hapa nchini zinazoamini kwamba unga unaotokana na matunda ya mbuyu, ni dawa yenye uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali, ikiwemo kuongeza kinga ya Ukimwi.
Mkazi mmoja wa Songea, mkoani Ruvuma, Abdallah Rashid, ameiambia FikraPevu kwamba yeye ni mmoja kati ya watu wanaoamini kuwa unga wa ubuyu ni dawa tosha ya kuongeza kinga ya mwili kwa mtu mwenye virusi vya Ukimwi.
Kwa mujibu wa Rashid, yeye mwenywe aligundulika kuwa na vurusi vya ugonjwa huo zaidi ya miaka 20 iliyopita, lakini ameendelea kuishi akiwa na afya hadi sasa kutokana na kupendelea kutumia majani ya mti kama sehemu ya mlo wake wa kila siku pamoja na kunywa uji unatokana na unga wa ubuyu.
“Wenzangu karibu wote ambao tuligundulika kuwa na virusi vya Ukimwi miaka zaidi ya 20 iliyopita, wameshafariki dunia kwa Ukimwi, lakini mimi bado ninaishi kwa sababu ya kupendelea kuchemsha majani ya mti wa mbuyu na kunywa kama chai pamoja na uji unaotokana na unga wa ubuyu,” anasema Rashid.
Anaongeza: “Watu wengi nimewaelimisha faida ya majani ya mbuyu. Mimi mwenyewe nilifumbuliwa macho na Padre mmoja mzungu ambaye alinifundisha kutumia majani ya mbuyu hata kabla ya dawa hizi za kurefusha maisha hazijagunduliwa. Majani haya ya mbuyu yanatibu pia ugonjwa sugu wa malaria pamoja na magonjwa mengine yanayoshindikana kutibika hospitalini.”
Utafiti mbalimbali uliofanywa kuhusu magome ya mti huo wa mbuyu, umebaini pia kwamba magome hayo yakitumika kitaalamu, yanaweza kuwa nyenzo muhimu katika sekta ya ujenzi, kwa magome hayo kusagwa na kuchanganywa na saruji kidogo tu kwa ajili ya kupigia ripu kuta za nyumba na pia kutengeneza sakafu, mazulia pamoja na karatasi ngumu zinazoweza kutumika kama vifungashio vya bidhaa mbalimbali kama vile maboksi.
Aidha, tafiti hizo zimebainisha kwamba asali ya nyuki inayozalishwa kutoka kwenye maeneo ya wazi ya mti wa mbuyu, ina ubora wa kipekee ikilinganishwa na asali nyingine yoyote ya nyuki inayozalishwa kutoka maeneo mengine.
Katika baadhi ya makabila ya jamii za Kitanzania, hutumia mti wa mbuyu kufanya matambiko yao mbalimbali, kama vile ya kuomba mvua inyeshe, kuomba mabalaa yanayoikumba jamii husika yaondoke na kadhalika kutokana jamii hizo kuamini kuwa mti huo wa mbuyu una miungu wenye uwezo wa kusiliza na kutatua shida zao mbalimbali.
Baadhi ya jamii za mataifa ya Afrika Magharibi, zina imani kubwa na mti huo wa mbuyu, zikiuheshimu mti huo kama mzazi na mlezi. Kwa hiyo, mti wa mbuyu unapokauka, ukaanguka na kufa, jamii hizo huomboleza na kufanya taratibu zote za mazishi kwa ajili ya mti huo kama ilivyo kwa binadamu.
Wataalamu Ekolojia wanasema imani hizo za jamii ya mataifa ya Afrika Magharibi, hasa wananchi wa nchi za Ghana na Burkinafaso, zamani zilikuwepo hata hapa Tanzania.
Kutokana na maajabu yote hayo ya mti wa mbuyu ndiyo yanayowafanya watalii kutoka ndani na nje ya nchi watamani kuutafuta mti huo popote ulipo ili kufanya utalii na kujifunza mengi ambayo yanahusiana na mti huo wa kipekee duniani, ikiwemo matumizi yake, maumbile yake na imani mbalimbali kuhusu mmea huo.
0 comments:
Post a Comment