VURUGU ZA BURUNDI: SERIKALI YA TANZANIA YAPIGA HESABU ZA HATIMA YA RAIA WAKE WALIOPO NCHI YS BURUNDI.
SERIKALI imesema itawaondoa Watanzania walioko Burundi baada ya kupata maombi yao kama wana matatizo kutokana na vurugu ambazo zimekuwa zikiendelea nchini humo kwa wiki kadha sasa.
Machafuko nchini humo yalianza baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwa atawania awamu ya tatu katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi ujao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mindi Kasiga, alisema hadi sasa wizara haijapokea maombi yoyote ya Watanzania wanaoishi Burundi ya kutaka kurejeshwa nchini.
“Unajua huwezi kuwarejesha tu labda wenyewe waone kuna tatizo…hata hayo maandamano yako katika mitaa michache,” alisema Kasiga.
Alisema hata watumishi wa Serikali katika ubalozi wa Tanzania nchini humo wanaendelea na kazi na hakuna malalamiko.
Hadi sasa watu 25 wamethibitishwa kufariki dunia huku zaidi ya wengine 100,000 wakikimbilia mataifa jirani wakihofu kuibuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Hadi kufikia jana wakimbizi walioingia nchini wamefikia 105,294.
Serikali ya Burundi
Pamoja na hali hiyo, Serikali ya Burundi imekana kuendesha vitendo vya kulipiza kisasi dhidi ya wale wanaotuhumiwa kuhusika na jaribio lililoshindwa la mapinduzi lililofanyika wiki iliyopita.
Ofisi ya Rais Pierre Nkurunziza ilisema jana jana kuwa wale waliohusishwa watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa utawala wa sheria.
Wafanyakazi katika hospitali mbalimbali nchini Burundi wamekuwa wakieleza kuwa kumekuwa na mshambulio ya kulipiza kisasi, ambako polisi wamekuwa wakiwajeruhi wanajeshi waliodaiwa kuhusika na jaribio hilo.
Lakini ofisi ya Nkurunziza ilisema serikali haikufanya wala haina nia ya kulipiza kisasi zaidi ya kusikia na kusoma hayo katika vyombo mbalimbali vya habari.
“Watu waliohusika na jaribio la aibu la kutaka kuangusha taasisi halali watakamatwa na kushitakiwa na sheria. Na itakuwa juu ya mahakama kuamua adhabu za kutoa kwa mujibu wa sheria,” iliongeza taarifa hiyo.
Jumatatu, Nkurunziza aliwafukuza kazi mawaziri watatu akiwamo wa ulinzi huku akikana kuwa uamuzi huo unatokana na jaribio la mapinduzi.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amekuwa kiongozi wa hivi karibuni anayetaka uchaguzi nchini Burundi uahirishwe.
Akizungumza baada ya mkutano nchini Angola, Zuma alisema uchaguzi huo haupaswi kufanyika hadi hali ya amani itakaporudi nchini humo.
Wakati hayo yakijiri maandamano yanaendelea Bujumbura kupinga mpango wa Nkurunziza wa kugombea urais kwa muhula wa tatu.
Uchaguzi wa urais umepangwa kufanyika Juni 26 na Nkurunziza amekataa kuuahirisha.
Viongozi kadhaa wa jaribio la mapinduzi wamekamatwa ingawa Jenerali Godefroid Niyombare ambaye alitangaza mapinduzi katika redio Jumatano iliyopita, bado yu mafichoni.
Kwa mujibu wa mashirika ya kimataifa ya wakimbizi, watu 105,000 wameikimbia Burundi kwenda nchi jirani wengi wao Tanzania.
0 comments:
Post a Comment