DODOMA TAYARI KUMEKUCHA, MMOJA WA WAGOMBEA URAIS CCM AENGULIWA HATUA YA MAKUNDI YA AWALI.
JINA la Edward Lowassa, mmoja wa wasaka urais kwa udi na uvumba, limeenguliwa katika hatua za awali za kinyang’anyiro hicho. Anaandika Saed Kubenea …(endelea).
Taarifa kutoka kwa watu waliokaribu na mmoja wa viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinasema, jina la mwanasiasa huyo limeondolewa kutokana na shinikizo la baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho.
“Ni kweli jina la Lowassa limeondolewa katika kinyang’anyiro hiki. Baadhi ya wakubwa wamekuja na msimamo na wameapa kutosikia mtu anayeitwa Lowassa likikatiza na kuingia NEC,” ameeleza mtoa taarifa wa gazeti hili.
Vikao vya uteuzi vya CCM – Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CC) na Halamashauri Kuu – tayari vimeanza mjini Dodoma mchana huu. Kikao cha NEC kinatarajiwa kuanza saa mbili usiku.
Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, ikiwa Lowassa ataondolewa katika kainyang’anyiro hicho katika hatua za awali, basi ndoto za mwanasiasa huyo kushika madaraka ya juu katika nchi, zitakuwa zimezimwa.
Lowassa amekuwa akihaha kutaka kuwa Rais wa Jamhuri tangu mwaka 1995, ambako alijitosa kugombea nafasi hiyo.
Hata hivyo, jina lake liliondolewa katika hatua ya awali baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere “kumng’ang’ania” na kushinikiza kuobdolewa kwa jina lake.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Lowassa hakujitosa katika kinyang’anyiro hicho; badala yake alimuunga mkono Kikwete kwa makubaliano ya kufanywa kuwa waziri mkuu na baadaye kuwa rais.
Habari zinasema, kuzimwa kwa ndoto za Lowassa, kunafuatia taarifa kuwa mchakato wa uchujaji majina ya wasaka urais kupitia CCM, kuendeshwa na baadhi ya vigogo kutoka idara ya usalama ambayo imesheheni “wabaya” wake.
Lowassa, mwanasiasa machachari katika siasa za CCM, ni miongoni mwa makada 38 wa chama hicho waliochukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa na chama chao kugombea wa urais wa Jamhuri.
Inaelezwa kuwa vita ya kisiasa anayopigana Lowassa kwa sasa, siyo tena kati yake na chama chake, bali ni kati yake na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).
Mgogoro wa Lowassa na TISS unatokana na ukaribu wa mwanasiasa huyo na aliyewahi kupata kuwa Mkurugenzi mkuu wa idara hiyo, Apson Mwang’onda.
“Lowassa akiteuliwa kugombea nafasi hiyo, atakuwa amewashinda watu wa usalama waliopo sasa; jambo ambalo haliwezi kukubarika,” kimeeleza chanzo kimoja cha taarifa mjini Dodoma.
Anaongeza, “…ikiwa hivyo, maana yake ni kuwa TISS iliyoko kwenye uongozi wa sasa itakuwa imeonyesha udhaifu mkubwa mbele ya Apson anayeratibu mbinu na mikakati ya Lowassa.”
Mkurugenzi wa usalama wa sasa, Othuman Rashid anadaiwa kumuunga mkono Bernard Membe, mmoja wa wasaka urais anayetajwa kuwa chaguo la Kikwete.
Katika hatua nyingine, taarifa zinamnukuu mmoja wa viongozi wa kamati kuu akisema, chombo hicho muhimu katika uteuzi wa wagombea urais, imegawanyika.
“Mgawanyiko unatokana na baadhi ya watu kutaka Lowassa asikatwe, huku wengine wakisema, sharti aondolewe,” anasema mmoja wa watoa taarifa wa gazeti hili.CHANZO http://mwanahalisionline.com
0 comments:
Post a Comment