BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KINGUNGE NGOMBALE-MWIRU ALIA KUKATWA KWA EDWARD LOWASSA KUWA MGOMBEA WA URAIS CCM, JE DK JOHN POMBE MAGUFULI HATOSHI URAIS ?.



Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru amesema CCM inamuhitaji Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu na kukitaka chama hicho kujadili jambo hilo ili kuondoa tofauti zilizojitokeza kabla ya kupiga kura za kumchagua Rais na wabunge.


Katibu huyo wa zamani wa halmashauri Kuu ya CCM amesema Kamati ya Maadili na Usalama iliteka majukumu ya Kamati Kuu baada ya kuamua kuchuja majina ya makada waliojitokeza kuwania urais kwa tiketi ya chama hadi kufikia watano, akisema jitihada hizo zilizofanywa kuvunja kanuni zililenga kumuengua Lowassa kuwania kuingia Ikulu.


Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, Kingunge, ambaye alijitokeza waziwazi kumpigia debe Lowassa, alisema kitendo cha kumuengua Lowassa kwa kuvunja kanuni kimeacha kasoro kubwa ndani ya chama hicho tawala kwa sababu taratibu zilikiukwa ili kupata viongozi.


Alisema kosa hilo si la Dk John Magufuli aliyepitishwa kuwa mgombea urais wa CCM, na wala si la Lowassa, bali ni la waliopendekeza majina ya walioingia tano bora.


Jina la Lowassa, ambaye alijidhihirisha kukubalika ndani na nje ya CCM kutokana na harakati zake za kusaka wadhamini kujaa watu, halikupelekwa kwenye Kamati Kuu, kwa mujibu wa Kingunge na hivyo kutojadiliwa na chombo hicho ambacho kilimpitisha Dk Magufuli, Dk Asha Rose Migiro, January Makamba, Bernard Membe na Balozi Amina Salum Ali.
Kingunge Ngombale Mwiru akizungumza na waandishi wa habari Nyumbani kwake Victoria, Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame
“Jitihada zote ambazo zimefanywa za kuvunja taratibu zilikuwa zinaelekezwa kwenye kumzuia Lowassa asipate haki. Badala ya yote nani kashinda? Kashinda Lowassa kwa sababu imeonekana wazi kuwa yeye ndio kipenzi cha Watanzania na hakuna kitu kikubwa kama kupendwa na watu,” alisema.


“Kuanzia sasa wana-CCM tutafute namna ya kushikamana vizuri, tuimarishe umoja wetu maana ndio nguvu yetu na katika hili ndugu Lowassa ana nafasi muhimu na ya kimkakati ana mamilioni ya Watanzania wana imani naye. 


“Mpaka sasa tunaulizwa maswali kutoka pande zote za nchi, hatuna majibu. Tukitaka kufanikiwa kama chama tuunde mazingira yatakayotuwezesha kutumia nguvu tulizonazo twende katika uchaguzi na tushinde kwa kishindo. Lakini lazima yaliyotokea yazungumzwe ndani ya chama maana tunahitaji ushirikiano wa Lowassa.”


Akielezea utaratibu wa uteuzi wa wagombea, Kingunge alisema Halmashauri Kuu ya CCM ndiyo inachagua Kamati Kuu ya chama inayoitwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa na ndiyo ambayo inaunda chombo cha Halamshauri Kuu ya Taifa kinachoitwa Kamati Kuu.


Alisema pia Halmashauri Kuu inaunda Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, kwamba ndani ya CCM vipo vitengo ambavyo vinahudumia vikao, kikiwamo cha Kamati ya Maadili.


Alisema kwa utaratibu wa kikatiba, kazi ya sekretarieti ni kuhudumia Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, katika kupitisha wagombea urais, Sekretarieti hukusanya majina ya walioomba kugombea na kuwasilisha taarifa yake kwenye Kamati Kuu.


“Sekretarieti si kikao cha maamuzi, wala si kikao rasmi cha mapendekezo. Mchakato hasa unatakiwa uanzie kwenye Kamati Kuu na ndiyo utaratibu uliotumika mwaka 1995. Wagombea wote wanatakiwa kupita Kamati Kuu na kila mmoja kujieleza sababu za kutaka kugombea urais,” alisema.


Katika kuteua mgombea urais wa CCM, vikao vya Kamati ya Maadili na Usalama, Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu vilipishana kwa muda mfupi kutoka kikao kimoja hadi kingine na kufanya suala hilo liamuliwe katika muda wa siku mbili.


Awali ratiba ilionyesha kuwa Kamati ya Maadili ingekutana Julai 8 na kufuatiwa na Kamati Kuu (Julai 9), na baadaye Halmashauri Kuu (Julai 10) kabla ya Mkutano Mkuu kumalizia mchakato Julai 11 na 12.


Saa chache baada ya Kamati Kuu kuwapitisha makada watano, wajumbe watatu wa Kamati Kuu, wakiongozwa na mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi waliongea na waandishi wa habari kueleza kuwa wanajitenga na uamuzi huo kwa kuwa ulifanywa kinyume na kanuni baada ya majina machache kuwasilishwa mbele yake.


Kingunge jana alipongeza uamuzi wa wajumbe hao watatu, akifafanua kuwa kilichotokea katika uteuzi huo ni batili na ni jambo jipya kwa sababu kazi ya kupata watu watano wa kupelekwa NEC ilifanywa na Kamati ya Maadili ambayo nayo alisema imevunja maadili kwa kufanya kazi ambayo si yake.


“Wagombea wote 38 waliojitokeza hawakupita Kamati Kuu kuulizwa maswali. Hata katika Kamati ya Maadili hawakuhojiwa. Kuna mahali watu fulani wachache wamekaa na kutengeneza orodha yao na kutaka kamati kuu imeze,” alisema.


“Nchi hii ni yetu wote na tunaowapa madaraka wasifike mahali wakafikiria nchi hii ni yao. Madaraka ni dhamana tu, wenyewe ni wananchi na hata CCM ni mali ya wanachama ni chetu wote.”


Alisema vikao na madaraka yake yakipuuzwa na kuletwa mtindo mwingine, ni dharau kwa wanachama wote, waliomba ridhaa ya chama hicho kupitishwa kugombea urais na kusisitiza kuwa kitendo hicho hakikubaliki.


“Bahati mbaya katika nchi yetu wananchi ni wavumilivu mno. Tunawapa madaraka wakubwa zetu na wanaamini wanaweza kufanya lolote kwa sababu hakuwezi kuwa na chochote. Lakini katika kusema tutasema tu,” alisema Kingunge.


Alisema NEC nayo ilitakiwa kujadili majina matano yaliyopendekezwa na Kamati Kuu, kwamba kutokana na safari hii majina hayo kutolewa na ‘kitengo cha maadili’, NEC iliyapokea bila kuhoji lolote na kusisitiza kuwa viongozi wastaafu wa chama hicho nao walipewa taarifa zisizo sahihi na kujikuta wakiunga mkono dhuruma badala ya kutetea haki.


Akizungumzia tuhuma za ufisadi dhidi ya Lowassa na kuhusishwa kwake na kashfa ya Richmond iliyosababisha ajiuzulu, alisema alifanya hivyo kuwajibika kisiasa, hata yeye (Kingunge) alimshauri afanye hivyo na kwamba suala hilo lilimpa ushindi.


“Hata Rais (Ali Hassan) Mwinyi alijiuzulu kwa makosa ya wengine. Serikali iliitumia Takukuru kutafuta ukweli uliotokea katika Wizara ya Nishati na Madini na taarifa zilizotolewa zilionyesha hakuna fedha zilizopotea ila bado Lowassa anaitwa fisadi,” alisema na kufafanua kuwa hata sakata la vua gamba iliyomlenga Lowassa kwa sasa imebaki hadithi tu.


Alisema Lowassa ana historia nzuri ndani ya CCM na angekuwa mwenyekiti mzuri wa chama hicho kwa maelezo kuwa anakijua vizuri, kwamba wengine ili wawe wenyeviti bora watalazimika kujifunza mambo ya chama hicho.


Alisema licha ya mbunge huyo wa Monduli kutopitishwa kugombea urais, yeye ndiye mshindi katika saka hilo kwa maelezo kuwa ukweli umedhihirika kuwa anapendwa na Watanzania na CCM imewapuuza wananchi waliokuwa wakimtaka.


“Mkitaka nchi ijiongoze lazima chama kijiongoze kwa kufuata misingi ya kidemokrasia. Watu wamehukumiwa katika vikao bila kusikilizwa. 


Kama makao makuu ya CCM yamepuuza haki ya wagombea, vipi kama hilo likitokea katika katika chaguzi za chama za mkoa, wilaya, kata na tawi,” alisema huku akisisitiza kuwa hawezi kuhama CCM ingawa chama hicho si mama yake mzazi.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: