RAIS AWAACHISHA KAZI, WAKUU JESHNI
Mkuu wa jeshi wa Nigeria, Jenerali Kenneth Minima.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, amewafuta kazi wakuu wa jeshi la angani,wanamaji na nchi kavu.
Inaaminika kuwa rais huyo mpya wa Nigeria amewatimua maafisa hao wakuu jeshini kwa 'kushindwa' kukabiliana na kundi la wapiganaji wa Boko Haram.
Hatua hii haikuwashangaza wachanganuzi wa maswala ya kiusalama nchini humo kwani rais Buhari ambaye mwenyewe ni jenerali mstaafu alikuwa ameahidi wapiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita kuwa ataitokomeza kabisa kundi hilo la Boko Haram.
Habari hii ya kutimuliwa wakuu imetangazwa siku chache tu baada ya mkuu wa jeshi Jenerali Kenneth Minima kusema kuwa
''ongezeko la mashambulizi yanayoshuhudiwa nchini yanalenga kuwatisha wanajeshi ambao yamkini wamewabana Boko Haram''
Jenerali huyo alisema kuwa kundi hilo limeanza kushambulia watu walioko sokoni na katika majumba ya ibada kwani wameshindwa kupambana na wanajeshi.
Zaidi ya watu 220 wameuawa katika kipindi cha siku 10 tu zilizopita kufuatia mashambulizi ya mabomu na ya kujitolea mhanga.
Shambulizi la hivi punde zaidi lilitokea katika mji wa Fotokol ulioko karibu na Cameroon ambapo takriban watu 13 walipoteza maisha yao jumapili.
Viongozi wakuu wapya wa jeshi wanatarajiwa kutangazwa muda mchache ujao.
0 comments:
Post a Comment