Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungi.
Wadau
wa mawasiliano mkoani hapa, wameiomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA), kudhibiti matumizi mabaya ya simu za mkononi na mitandao
hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
nchini Oktoba 25, mwaka huu.
Wadau hao walitoa rai hiyo juzi mjini hapa, kwenye warsha
iliyotolewa na TCRA kwa lengo la kuwakumbusha wananchi manufaa ya
mawasiliano.
Wadau hao walisema kadri siku za uchaguzi zinavyokaribia, ndivyo
ujumbe wa kupigana vijembe kwa lengo la kuchafuana kisiasa zinazidi
kukithiri na kuendelea kuwachanganya wananchi.
Akizungumza kwenye warsha hiyo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Wilaya ya Njombe, Edward Mgaya, aliwataka wananchi wasitumie simu
zao vibaya kwa kuchafuana au kufanya malumbano kwenye mitandao ya
kijamii hasa wakati huu wa uchaguzi.
“Ndugu zangu wananchi wa Njombe ninawaombeni kipindi hiki cha
uchaguzi tumieni simu zenu vizuri msichafuane ili muweze kufanya
uchaguzi kwa amani na mpate kiongozi atakayewatatulia changamoto zenu,
”alisema.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliohuduria warsha hiyo, walitoa
tahadhari ya matumizi ya simu kifamilia kwa kutopokea picha zinazoweza
kuhatarisha au kuvunja ndoa zao.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto, Pindi Chana, aliwataka wakazi wa Njombe kutumia mawasiliano ya
simu kutafuta masoko ya mazao yao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, aliitaka Mamlaka hiyo kupunguza gharama za simu.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungi (pichani),
amewaondoa hofu wananchi wanaoishi karibu na minara ya mawasiliano
kuwa haina madhara kwao.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment