VYAMA VYA SIASA ZANZIBAR VYAGOMA KUSAINI WALAKA WA MAADILI CHINI YA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI ZANZIBAR.
Zanzibar. Viongozi wa vyama vya siasa visiwani hapa wamekataa kusaini waraka wa maadili ya uchaguzi ya vyama vya siasa uliowasilishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), vikitaka vyombo vya usalama vijumuishwe.
Makubaliano ya maadili hayo ya uchaguzi yalitakiwa yasainiwe kwenye kikao hicho baina ya ZEC, iliyoongozwa na mwenyekiti wake, Jecha Salum Jecha na viongozi wa vyama vya siasa kwenye Hoteli ya Grand Palace.
Maadili hayo yanatakiwa kuwa mwongozo kwa vyama vya siasa wakati wote wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25 kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi kufanyika kwa uhuru na haki.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa alisema hawatasaini waraka wa maadili hayo hadi kitakapoingizwa kipengele kitakachoeleza wazi majukumu ya polisi na vikosi vya SMZ alivyodai vimeonyesha ishara mbaya katika siku za hivi karibuni.
Jussa alisema licha ya kuwa vikosi vya SMZ havitakiwi kisheria kusimamia uchaguzi, vimekuwa vikiingilia uandikishaji wa wapigakura na kukiuka haki za binadamu, sheria, kanuni na taratibu za uandikishaji, jambo ambalo limesababisha malalamiko makubwa kwa wananchi na wadau hao.
Alisema bila ya kuwekewa kipengele mahususi kwa polisi na vikosi vya SMZ, maadili hayo yatakuwa hayana maana yoyote kwa kuwa hivi karibuni Wazanzibari wameshuhudia baadhi ya askari wakiwa wamefunika nyuso zao.
Alidai kuwa askari hao wamekuwa wakibeba silaha za moto na za kienyeji kama mapanga, nondo na misumeno ya kukatia miti na kuwatisha wananchi na waandishi wa habari.
“Mwenyekiti mimi na chama changu hatukubali kusaini maadili haya na ninawashawishi wenzangu wakatae hadi hapo kitakapoingizwa kipengele ambacho kitaeleza bayana majukumu ya polisi, majukumu ya vikosi vya SMZ,” alisema.
“Hivi juzi tu vimeonyesha mfano mbaya kwa askari kuvaa masoksi usoni kuwavamia na kuwapiga watu, kuvamia vituo vya redio na kufanya uhuni mkubwa. Kwa hivyo kama hawajaingizwa hawa kwenye mwongozo huu wa maadili hatuwezi kutia saini. Kikao kivunjwe, mkaingize na kisha tuitane tena kuja kusaini,” alisema.
Kauli ya Jussa iliungwa mkono na wadau wengine waliopiga makofi kukubaliana naye.
Wajumbe hao walisema ni kweli kuna kila sababu ya polisi na vikosi vya SMZ kuwekewa utaratibu wa maadili kwa kuwa wao ndio waharibifu wa uchaguzi hivyo si vyema maadili yakawaacha nyuma.
Suleiman Mohammed Abdallah kutoka chama cha NRA alisema anashangazwa kuona Serikali ikikaa kimya licha ya kelele zote zilizopigwa dhidi ya ukiukwaji wa sheria na haki wa kuingilia uandikishaji huku Jeshi la Polisi likiwakana watu wao na kusema hawawajui wenye kuendesha vitendo hivyo.
“Nashangaa, Serikali inaona vitendo vilivyokuwa vikifanyika. Njiani vya watu wanabeba silaha za moto, mapanga, misumeno ya kukatia miti wanatumia magari ya polisi na wengine wamevaa sare. Sasa hawa kama hawajawekewa utaratibu maalumu au hawajaingizwa kwenye haya maadili watakuja kutuletea maafa baadaye,” alisema Mohammed.
Akitaja kipengele cha kuongeza katika maadili hayo, Jussa alisema kifungu cha 15 kwenye wajibu wa Serikali na ZEC kuongezwe wajibu wa Jeshi la Polisi na vikosi vya SMZ.
Alisema wajibu wa Jeshi la Polisi uwe ni kuhakikisha wanalinda usalama wa raia na mali zao, wanalinda wapigakura, maofisa wa ZEC, lakini pia kuhakikisha wanalinda amani na usalama na hawaingiliwi na taasisi nyingine ya ulinzi kwa kuwa wao ndio wenye mamlaka ya ulinzi.
Pia alipendekeza kuwa katika kipengele hicho Jeshi la Polisi lihakikishe linafuata sheria na katiba na kwamba kwenye idara maalumu za SMZ kuna sheria iliyozianzishwa na majukumu na hivyo zikubali kuwa hazitaingilia kwa hali yoyote katika uchaguzi.
Juma Said Sanani kutoka ACT-Wazalendo alisema kuwekwa maadili ya uchaguzi ni muhimu kwa kuwa yatakuwa ni mwongozo wa kuipelekea nchi kwenye amani na kufanyika uchaguzi huru na wa haki. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment