WASEMAVYO WALIOTINGA 5 BORA YA URAIS CCM, BERNARD MEMBE.
Dar es Salaam. Kwa mtazamo wa wengi, ilionekana dhahiri kwamba Berbard Membe alikuwa miongoni mwa wanaCCM wenye nguvu kubwa walioomba kuteuliwa na chama hicho kuwania urais.
Kutokana na ukweli huo, haikushangaza pale Kamati Kuu (CC) ya CCM ilipomuweka katika kundi la makada wake watano kwa ajili ya kupigiwa kura na kuingia katika mchujo wa mwisho wa Mkutano Mkuu.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, tangu awali alionekana kujiamini katika mkakati wake huo huku akizindua kampeni yake Juni 8 huko Lindi kwa kishindo.
Siku hiyo alisema katika utawala wake, ataboresha elimu, ataweka msisitizo katika utawala bora, maendeleo ya jamii, uchumi na masuala mbalimbali ya kisiasa na kidiplomasia.
“Nimetafakari sana, nimeona ninatosha kwa nafasi hii nyeti… nafasi adhimu na si ya mzaha japo naona wapo wanaofanya mzaha. Nimeangalia nikaona hakuna mwingine wa kufanana na mimi. Sikukurupuka, zipo nafasi za kukurupuka na wapo wanaokurupuka, lakini si vyema kukurupuka kwa nafasi ya urais,” alisema.
Mbunge huyo wa Mtama ambaye ameshatangaza kutogombea tena kiti hicho, amepita katika vikwazo mbalimbali kwenye mchakato wa chama hicho, mpaka kufikia hatua hiyo.
Alikuwa miongoni mwa makada sita waliofungiwa mwaka mmoja na CCM kwa kuanza kampeni za kiti hicho mapema.
Machi mwaka huu, alikwenda Butiama na kuzuru kaburi la Mwalimu Nyerere na kupiga goti na kumweleza nia yake ya kuutaka urais.
“Nilipiga goti nikamwambia Mwalimu, navitaka viatu vyako, alivivaa Mzee Mwinyi (Ali Hassan), Mzee Mkapa (Benjamin) na Kikwete (Jakaya), sasa nataka kuvaa mimi na nina hakika vinanitosha. Ninaamini vitanitosha. Nikamwambia chondechonde, kama havitanitosha, niambie… timu yangu ya mikoani ikawahi kuniambia unatosha,” alisema Membe.
Safari ya kusaka wadhamini
Baadaya ya kuzindua kampeni, Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alianza safari ya kusaka wadhamini ambako huko alikuwa akitoa kauli mbalimbali zilizoibua mijadala katika vijiwe vya siasa.
Mathalan, Juni 10 akiwa mkoani Mbeya alieleza kuwa, atamuunga mkono Profesa Mark Mwandosya ikitokea jina lake likakatwa na mgombea mwenzake huyo likarudi.
“Natamka hili kwa moyo wangu wa dhati, jina langu lisiporudi ndani ya chama, nitampigia kampeni Profesa Mwandosya. Sina tatizo lolote hata wakisema mimi nimuachie Mwandosya nipo tayari, kwani ndiyo wanaotakiwa kwa sasa kuongoza nchi yetu,” alisema.
Akiwa Shinyanga Juni 19, aliwataka Watanzania kuwa makini katika kuchagua viongozi, badala ya kukurupuka, kwa kuwa baadhi ya waliochukua fomu za kugombea urais wanataka kujaribu tu.
“Lazima uwe na hekima na busara unapotaka kugombea nafasi ya ngazi ya juu ikiwamo urais, huwezi kwenda kuchukua fomu wakati hata hujawahi kushika wadhifa wowote ndani ya chama. Unataka kwenda kujifunza ukiwa madarakani? Watu kama hao kuweni nao makini,” alisema Membe.
Alisema mtu anayetaka kugombea urais, anapaswa kuzingatia vigezo 13 vilivyowekwa na chama, lakini wapo ambao wameshindwa kujipima kabla ya kuchukua fomu.
Juni 28, akiwa Mjini Sumbawanga, alikiri kwamba katika kinyang’anyiro cha urais ndani CCM, mtu anayemnyima usingizi ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
“Wengine wote hawanitishi nitawagonga lakini nikifika kwa Pinda itabidi nipumue kwanza... kwa hiyo mimi na Pinda ni pacha nikishindwa mimi nitamuunga mkono, lakini akishindwa naamini ataniunga mkono, ndiyo maana hata wakati nakuja huku nimewasiliana naye akanieleza nenda na amenisaidia nimepata wadhamini wa kutosha,” alisema.
Tuhuma za ufisadi
Akiwa Dar es Salaam Juni 30, Membe alilazimika kutoa ufafanuzi wa sakata la mabilioni kutoka Libya ambayo amekuwa akihusishwa nayo.
Alisema Serikali za Libya na Tanzania zilitiliana saini mkataba wa nyongeza ambao ulizungumzia, pamoja na mambo mengine, matumizi ya fedha hizo.
“Ni mkopo uliotolewa kwa Kampuni ya Meis kwa mujibu wa Mkataba wa Makubaliano ya Uwekezaji (Investment Agreement) wenye masharti ya kibenki. Masharti hayo ya kibenki yanamtaka mwekezaji kuweka dhamana, kulipia riba, kuwekewa muda wa kurudisha mkopo na anawekewa hatua za kuchukuliwa endapo atashindwa kulipa mkopo,” alisema.
Kutoka ubunge hadi uwaziri
Safari ya Membe kisiasa ilianza mwaka 2000 kwenye Uchaguzi Mkuu alipoomba ridhaa ya ubunge wa Mtama, Lindi na akaibuka na ushindi ikiviacha vyama vingine kwa mbali wakati huo akiwa na umri miaka 47.
Aligombea tena na kushinda kwa asilimia 79 mwaka 2005, kwani Isack Wolfgans Ndaka wa TLP na Said Hamis Mtepa wa CUF hawakumpa upinzani mkubwa.
Baada ya uchaguzi huo, Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia Januari 2006 hadi Oktoba 2006 alipomhamishia Wizara ya Nishati na Madini ambako alishikilia wadhifa kama huo hadi Novemba 2007 alipopanda ngazi na kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akichukua nafasi ya Dk Asha-Rose Migiro. Aliomba tena ridhaa mwaka 2010 na kushinda kwa asilimia 81.76.
Anavyotazamwa kwao
“Kasi ya maendeleo ni ya kawaida na kuna mafanikio machache yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Membe lakini nahisi ni kutokana na ukubwa wa jimbo,” anasema Hassan Said, mkazi wa Kijiji cha Majengo.
Mkazi wa Kijiji cha Mtauni Ditrick Makota, anasema licha ya changamoto zilizopo amefanya mamb yanayoonekana. Amepeleka kituo cha mafuta, kituo cha afya na ujenzi wa Mahakama.
“Nitafurahi akipata urais, nahisi maendeleo yatazidi katika jimbo letu kwa sababu tulikuwa tunabeba wagonjwa kwa machela hadi Hospitali ya Nyangao. Ana tabia ya ushirikiano na kukubali kubadilishana mawazo,” anasema Makota ambaye anaishi kijiji kilicho karibu na alipozaliwa Membe.
Mkazi wa Chiponda aliyekuwa darasa la pili wakati Membe anamaliza darasa la saba, Seif Chilepela anamtaja kama kioo cha uongozi tangu walipokuwa shule.
“Tulikuwa tunacheza pamoja na alishaonekana kuwa kiongozi ila kutoka kwake nje ya nchi mara kwa mara nahisi kumemwongezea chachu ya maendeleo,” anasema.
Asilimia kubwa ya wakazi wa alikozaliwa mbunge huyo, wanasema ushindi wake katika kiti cha urais ni chachu ya kuwafanya waishi kama ‘Ulaya’, huku wale wa maeneo ya Nyangao na vijiji vya jirani wanaona ni bora asijaribu kwani hatashinda.
Katibu Mwenezi wa CCM, Kata ya Mtama, Omar Omar anasema Membe amefanya mengi lakini changamoto za majisafi na salama na ukubwa wa jimbo bado zimesalia.
“Maji siyo tatizo lakini si salama, tuna visima na mito lakini asilimia 80 ya miundombinu yetu ni ya miaka 15 iliyopita,” anasema Omar.
Mkazi wa Nyangao John Cassian, anasema hajatekeleza ahadi zake nyingi ikiwamo ya kukuza utalii ambao ungetoa ajira kwa vijana. Anasema Membe ni kiongozi mwenye nia ya maendeleo lakini uwaziri ulimfanya awasahau wananchi wake na kuishia kuahidi visivyotekelezeka.Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chiponda, Wenje Msafiri anasema maendeleo yanaonekana kwa macho licha ya kusalia changamoto za umeme, maji na ujenzi wa shule.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment