BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WASEMAVYO WALIOTINGA 5 BORA YA URAIS CCM, JANUARY MAKAMBA

 

January Makamba 


Alijiandaa na haikushangaza kusikia akiwa miongoni mwa wagombea watano waliovuka katika mchujo wa Kamati Kuu (CC) na kuingia katika hatua ya kupigiwa kura na Halmashauri Kuu (NEC).


Tangu alipotangaza nia, January Makamba (41), amekuwa katika hekaheka za kujitangaza na kujinadi siyo kwa wanaCCM pekee, bali hata wananchi kupitia machapisho mbalimbali.


Hata hivyo, hadi mwaka 2012, Naibu Waziri huyo wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, hakuwa na mipango ya kugombea urais. Aliwahi kuhojiwa katika kipindi cha mikasi cha Televisheni ya EATV na kusema hana mpango huo kabisa.


Pengine Mbunge huyo wa Bumbuli alikuwa na lake moyoni kwani Julai 2, mwaka jana aliweka bayana nia yake wakati alipohojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC na kusema atagombea urais kwa sababu Tanzania inamhitaji mtu mwenye sifa kama zake, wa kizazi cha sasa.


Tangu wakati huo, January amefanya mambo mengi ya kujizatiti kwenye nia yake hiyo ikiwamo kutoa kitabu maalumu cha maswali 40, kilichoandikwa na mwandishi Privatus Karugendo kikionyesha kikijibu maswali mbalimbali kuhusu namna mwanasiasa huyo kijana atakavyoweza kupambana na changamoto za urais iwapo chama chake kitampa ridhaa na Watanzania wakamchagua.


Wakati akiendelea na harakati zake Februari, 2014 yaliibuka mambo yasiyotarajiwa baada ya vikao vya CCM kutoa “onyo” dhidi yake na wanachama wengine watano kuwataka wasiendelee na “mchezo mchafu” wa kampeni za urais kabla chama hicho hakijaanzisha mchakato huo rasmi, hapo ndipo wengi wakang’amua kwamba January anausaka urais wala hatanii.


Mtoto huyo wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Mzee Yusuph Makamba, aliingia rasmi kwenye siasa mwaka 2010 alipoomba ridhaa ya CCM kuwa Mbunge wa Bumbuli, wilayani Lushoto na katika kura za maoni za chama hicho, alimshinda mbunge mzoefu, William Shelukindo kwa kupata kura 14,612 dhidi ya 1,700. Baada ya kushinda ndani ya chama chake, January hakukutana na mpinzani yeyote kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na hivyo akaingia kwenye rekodi ya wabunge waliopita bila kupingwa.


Katika Bunge la 10, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na mwaka 2011, CCM ilimteua kuwa Katibu wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa akichukua nafasi ya Benard Membe. Alitumikia wadhifa huo ndani ya chama chake hadi mwaka 2012 alipomuachia Dk Asha-Rose Migiro.


Katika Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM, January alichaguliwa kuwa kati ya wajumbe 10 wa Kamati Kuu ya chama kutoka upande wa Tanzania Bara akipata kura 2,093.


Atangaza nia mara ya pili
Juni 7, akiwa Dar es Salaam, January alitangaza nia kwa mara nyingine ya kuwania urais akiahidi kwamba Serikali yake itaunda baraza la mawaziri wasiozidi 18 wasiotiliwa shaka na wananchi juu ya uwezo na uadilifu wao.


Alisema ametafakari kwa kina kuhusu changamoto zinazoikabili nchi na aina mpya ya uongozi inayohitajika na kuamua kuomba ridhaa ya urais ili azitatue.


“Sijagombea kugombana na watu, nimegombea kupambana na changamoto za watu. Naiomba nafasi huku nikiifahamu kiu ya Watanzania kupata aina mpya ya uongozi wa zama za sasa utakaotoa matumaini mapya yatakayozaa Tanzania mpya. Naelewa misingi iliyojenga nchi yetu ya haki, umoja, amani, upendo na mshikamano… inayotakiwa kulindwa kwa gharama zote.”


Alisema kiongozi atakayechaguliwa Oktoba anapaswa awe na majawabu mapya ya changamoto za Watanzania yatakayomtofautisha na wengine.


“Sitaunda Serikali ya waporaji na wabinafsi. Nitaunda Serikali yenye utu, inayowasikiliza watu, itakayotimiza wajibu wake bila chembe ya uonevu wala ulegevu… nitaunda Serikali ya mawaziri 18 ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa shaka uadilifu wake au uwezo wake,” alisema Makamba huku akishangiliwa.


Alisema Serikali yake itakuja na vipaumbele vitano vya kukuza vipato vya watu kwa shughuli zote, huduma bora na za uhakika za kijamii; utawala bora, utawala wa sheria, usimamizi wa uchumi na kulinda amani, umoja na usalama wa nchi.


Alichukua fomu Juni 10 na kusisitiza kuwa hakuingia katika kinyang’anyiro cha urais kujaribu na wala hajajipanga kwa ajili ya miaka ijayo, bali kushinda sasa na atafanya jitihada zote ndani ya kanuni kuwashawishi wana-CCM wamchague.


Alisema anataka kuleta mabadiliko nchini na atainadi ilani kuhakikisha analeta nguvu mpya na chachu ili CCM iendelee kuaminiwa na kuwa tumaini la kweli kwa Watanzania.


“Maarifa ninayo, upevu ninao, ukomavu ninao, dira ninayo na nitahakikisha kwamba ndani ya kanuni za chama ninafanikiwa ili nipate fursa na heshima ya kukiongoza.” Alisema ana imani na viongozi wakuu wa CCM katika kuongoza mchakato wa kupata mgombea mmoja, katika hekima, busara na upevu wao.


Alisema uzee wala ujana siyo sifa, bali uzalendo, uadilifu, maarifa, ukomavu, utulivu, hekima na uwezo wa kuongoza nchi.


Alisema akiwa Rais, atafanyia kazi taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na watumishi ambao taasisi zao zitabainika kuwa na matumizi mabaya ya fedha watasimamishwa kazi na hatua za kisheria zitafuata.


Alirejesha fomu Julai 2 na kusema kuwa ana imani vikao vya kuwachuja wagombea wa urais vitafanya uamuzi kwa kujiamini na siyo kwa hofu.


“Tumepata nafasi ya kupitia michakato mingi migumu kuliko hata huu, tumefanya uamuzi katika mambo mengi na makubwa na bado tumeendelea kubaki kuwa wamoja. Nina imani hata katika hili pia tutavuka salama,” alisema.


Alisema wananchi wengi hasa vijana wanaangalia CCM itamteua mgombea wa aina gani na wanataka aina mpya ya uongozi ambao unaangalia mbele na unaoakisi matarajio yao.


Makamba alisema wana-CCM, kama walivyo wananchi wote, wanachukizwa na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na wanachukizwa na chama chao kuhusishwa na masuala hayo.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: