BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CCM KUZINDUA KAMPENI ZA URAIS, UBUNGE NA UDIWANI NCHI MZIMA ZA UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA 25 MWAKA HUU KATIKA VIWANJA VYA JANGWANI DAR ES SALAAM.


Mgombea mteule wa Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, akizungumza na wananchi kwenye viwanja vya Ofisi Ndgo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, Picha ya maktaba.


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kinatarajiwa kuzindua kampeni zake za urais, ubunge na udiwani nchi nzima katika viwanja vya Jangwani leo, katika mkutano utakaorushwa moja kwa moja na televisheni na redio mbalimbali nchi nzima.

Katika uzinduzi huo, CCM pia inatarajiwa kuweka ilani yake ya uchaguzi hadharani, itakayonadiwa na mgombea urais wake, Dk John Magufuli na wagombea wengine wa ubunge na udiwani nchi nzima. 


Moja ya mambo ambayo CCM inatarajiwa kufafanua ni matumaini makubwa ya uwezo wa mgombea wake katika kusimamia utekelezaji wa ilani hiyo, kutokana na historia yake ya utendaji ndani ya Serikali katika nafasi mbalimbali alizokabidhiwa, ikiwemo Waziri wa Ujenzi.

Wageni mbalimbali pia wamealikwa kuhudhuria uzinduzi huo vikiwemo pia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa CCM Mkoa, Juma Simba vile vile wanatarajia wageni kutoka ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam kuhudhuria mkutano huo leo.


“Tumetuma mialiko ya mkutano wa kesho (leo) sio tu kwa wana CCM wenzetu bali pia kwa vyama vingine vya siasa ikiwa ni pamoja na kwa vyama vya ‘Ukawa’,” alisema.

Simba alisema mkutano huo utakuwa mkubwa na wa aina yake ambapo viongozi mbalimbali wa chama wanatarajiwa kushiriki na kwamba mkutano huo ratiba yake itaanza asubuhi saa tatu kwa burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali na wananchi kuendelea kuwasili uwanjani. 


Sifa za Magufuli Mgombea huyo amekuwa akitajwa kuwa na sifa ya mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, ambapo Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alimpachika jina “Tingatinga”.

Rais Kikwete alimpachika Magufuli jina hilo, baada ya kutangazwa kuwashinda makada wengine wawili waliokuwa wakiwania kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Dodoma. 


“Kila mtu anaitwa jembe lakini huyu ni zaidi ya jembe. Ni tingatinga… Magufuli ni bulldozer. Magufuli havumilii ujinga, ni mtu ambaye anataka kuona kazi zake zinafanyika kama alivyoagiza,” alikaririwa akisema.

Kikwete aliendelea kummwagia sifa Dk Magufuli kuhusu utendaji wake akisema kuwa alipokuwa akifuatilia makandarasi kwenye miradi ya ujenzi, alidiriki kuwatimua pale alipobaini walikuwa wakifanya kazi kinyume na makubaliano. 


Baadhi ya watu waliofanya naye kazi wamekaririwa wakisema iwapo atachaguliwa kuwa rais basi wavivu wajitayarishe kukimbia kwani Waziri huyo ni mchapa kazi wa hali ya juu.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mussa Iyombe, aliyefanya kazi na Dk Magufuli kwa zaidi ya miaka 10, alikaririwa akisema kwa kipindi alichofanya kazi na Magufuli ameshuhudia kuwa hataki mchezo katika kazi, hana mzaha na mwenye umakini mkubwa kwa kila anachofanya. Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Segolena Francis alikaririwa akimsifu Magufuli kuwa ni mtu anayejali muda, anayependa kazi yake na asiyetaka mtu legelege.

“Nimejifunza mambo mengi kwake na nina tumaini kuwa kama atakuwa Rais, basi taifa litakuwa limepata mchapakazi. Anafuatilia kila kitu yeye mwenyewe, hana makundi, hana ukabila wala udini,” alikaririwa akisema. 


Katika mkutano huo wa leo , CCM pia inatarajiwa kufafanua mafanikio yake katika miaka 10 iliyopita, ikiwemo kuongeza mapato ya serikali. Taarifa za serikali zinaonesha kuwa mapato ya serikali yameongezeka kutoka Sh bilioni 177.1 mwaka 2005 kwa mwezi, hadi takribani Sh bilioni 850 na kuwezesha bajeti ya serikali kukua kutoka trilioni 4.13 mwaka 2005/2006 hadi trilioni 22.49 mwaka 2015/2016.

Mafanikio hayo ya makusanyo yamewezesha serikali kutekeleza kazi zake na miradi ya maendeleo, huku ikipunguza misaada na mikopo ya washirika wa maendeleo, kutoka asilimia 42 ya Bajeti ya serikali mwaka 2005 hadi asilimia 15 mwaka 2014/2015 na kushusha zaidi hadi asilimia 8 mwaka huu wa fedha wa 2015/2016.


 Barabara Ujenzi wa barabara ni matunda ya ongezeko la mapato ya serikali na udhibiti katika matumizi ya fedha za umma uliofanyika katika uongozi wa Awamu ya Nne.

Taarifa zinaonesha kuwa wakati Tanganyika, sasa Tanzania Bara ikipata Uhuru mwaka 1961, uongozi wa mkoloni uliokaa tangu miaka ya 1884 na 1885 mpaka 1961, uliacha mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilometa 1,360, lakini katika uongozi wa miaka 10 tu ya Serikali ya Awamu ya Nne, mtandao wa barabara za lami uliojengwa na kukamilika una urefu wa kilometa 5,568 katika barabara kuu na kilometa 535, kwa upande wa barabara za mijini.

Ukuaji uchumi Katika ukuaji wa uchumi, CCM inatarajiwa kujivunia miaka kumi ya ukuaji wa uchumi, ambapo Pato la Taifa (NNP) lilikuwa wastani wa takribani asilimia saba na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa 10 ya Afrika na 20 duniani ambayo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa. 


Aidha Pato Ghafi la Taifa (GNP), limetajwa kuongezeka zaidi ya mara tatu kutoka Sh trilioni 14.1 mwaka 2005 hadi kufikia Sh trilioni 79.4 mwaka 2014 na kufanya pato la wastani la Mtanzania kuongezeka kutoka Sh 441,030 mwaka 2005 hadi Sh 1,724,416 mwaka 2014.

Ukuaji kisekta CCM itaendelea kujivunia ukuaji katika sekta ya utalii, ambayo imekua kwa wastani wa asilimia 7.1 na kuchangia asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni. 


Idadi ya watalii katika miaka kumi ya Awamu ya Nne, imeongezeka kutoka watalii 612, 754 mwaka 2005 hadi watalii 1,140,156 mwaka 2014. Idadi ya vitanda katika mahoteli imeongezeka kutoka 15,828 hadi 21,929 na kusababisha mapato kuongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 823.05 mwaka 2005 hadi Dola za Marekani bilioni mbili mwaka 2014.

Viwanda Katika sekta ya viwanda, pia kumekuwa na mafanikio ambapo takwimu zinaonesha kuwa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo vimeongezeka kutoka 11, 544 mwaka 2005 hadi viwanda 51,224 mwaka 2015. 


Kutokana na mafanikio hayo, mchango wa viwanda kwenye mauzo ya bidhaa nje, yanayoimarisha akiba na upatikanaji wa fedha za kigeni, ukiongezeka kutoka asilimia 9.3 mwaka 2005 hadi asilimia 23.3 mwaka 2014.

Nishati Chama hicho pia kinatarajiwa kutumia fursa ya mafanikio katika sekta ya nishati katika kushawishi kupata kura zaidi, ili kipate uhalali wa kuendelea kuongoza katika Awamu ya Tano ya uongozi. 


Katika miaka 10 ya Awamu ya Nne, umeme umesambazwa kwa vijiji 5,336 kati ya vijiji 12,423 nchini, ambapo idadi ya Watanzania wanaopata umeme imeongezeka kutoka asilimia 10 hadi asilimia 40 mwaka 2015.

Mbali na kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia nishati ya umeme mijini na vijijini, pia serikali imesimamia uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara na Songo Songo kwenda Dar es Salaam unaotarajiwa kuwezesha uzalishaji wa megawati 3000 za umeme. 


Elimu Mafanikio mengine yanayotarajiwa kutumiwa na CCM katika kushawishi kupata kura zaidi ni katika elimu.

Bajeti ya elimu katika mwaka huu wa fedha ni kubwa kuliko ya sekta zingine, inayofikia Sh trilioni 3.4 kutoka Sh bilioni 600 iliyokuwepo mwaka 2005. 


Kutokana na hali hiyo, serikali kwa kushirikiana na wananchi ilianza kujenga shule za sekondari za kata, ambapo wananchi walihamasishwa, wakahamasika na wakajenga shule nyingi za sekondari ambapo mwakani itakuwa bure.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: