BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KOCHA MKUU WA KLABU YA SIMBA SC AIGA MFUMO WA UFUNDISHAJI WA KLABU YA AZAM FC.

Kocha wa timu ya Simba ,Dylan Kerr .


Dar es Salaam.
Mafanikio ambayo klabu ya Azam imeyapata kwenye mashindano ya Kombe la Kagame mwezi uliopita kwa kucheza mechi sita bila kuruhusu bao, yameishawishi Simba kuiga mfumo huo.

Timu hiyo ambayo sasa hivi inahangaika kupata kikosi bora cha kwanza kitakachoiwezesha kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu msimu huu, imeamua kujaribu mfumo wa 3-5-2, unaotumiwa na Azam inayosifika kwa kuwa na ukuta wa chuma.

Simba ambayo tangu kuwasili kwa kocha Dylan Kerr imekuwa ikitumia mfumo wa 4-4-2 na kuwachezesha, ilianza kujaribu mfumo huo wa 3-5-2 kwenye mechi dhidi ya Mwadui, Jumatatu ambayo ilimalizika kwa sare ya 0-0.

Hata hivyo, mfumo huo unaohitaji mabeki wawili wa pembeni wenye uwezo mkubwa wa kushambulia na kurudi nyuma kuzuia kwa haraka kama ilivyo kwa Shomari Kapombe, Erasto Nyoni ulionekana kuipa shida timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi iliyowakosa nyota wake kadhaa waliomo Taifa Stars.

Kocha anapotumia mfumo wa 3-4-3 hupendelea kuwatumia Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto na Ibrahim Ajibu kwa pamoja kutokana na uwezo wao wa kumiliki mpira na kupandisha mashambulizi kwa haraka.

Hata hivyo kocha anapotumia mfumo wa 4-4-2 hupendelea kuwachezesha Majabvi, Awadhi Juma na Kazimoto katikati huku akimtumia Peter Mwalyanzi kama kiungo wa pembeni lakini anayekuja katikati pia ili kuwapa uhuru mabeki wake wa pembeni, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Hassan Kessy kusaidia mashambulizi kupitia pembeni.

Wakati mwingine kocha anapotumia kikosi cha pili huwatumia Awadhi Juma, Abdi Banda pekee katikati huku katika winga akiwachezesha Issa Ngoah na Simon Sserunkuma ambao pia huingia katikati. Hii ni katika mfumo wa 4-4-2.

Beki mpya wa Simba, Emery Nibomana aliliambia gazeti hili kuwa mfumo 3-5-2 ni miongoni mwa ile ambayo klabu yao itaitumia kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

“ Huu ni mfumo mpya ambao kocha wetu atautumia pia kwenye ligi. Unapoingia kwenye ligi huwezi kutegemea mfumo mmoja na ndiyo maana kama unavyoona leo tumecheza huu wa mabeki watatu ambao naamini tutauzoea haraka,” alisema Nibomana, raia wa Burundi.

Naye kiungo mzoefu, Mwinyi Kazimoto alisema kuwa japo timu hiyo haikuumudu vyema mfumo huo wa 3-5-2, anaamini kuwa ni mzuri na utaweza kuisaidia timu hiyo kwa kiasi kikubwa siku za usoni.

“Mnapocheza viungo watano katikati mnakuwa na nafasi kubwa ya kutawala mpira na kuwanyima wapinzani nafasi ya kucheza . Ni kweli siku ya kwanza umeonekana kutupa shida, lakini ndiyo maana ya kucheza mechi za kirafiki,” alisema Kazimoto.

Iwapo Kerr ataamua kuendelea na mfumo huo, atakuwa amefuata nyayo za Mwingereza mwenzake wa Azam, Stewart Hall ambaye tangu aliporudi kuinoa klabu hiyo amekuwa akiutumia mfumo huo ambao umeifanya timu hiyo kuwa ngumu kufungika.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: