MGOMBEA URAIS KUPITIA UKAWA AKUMBWA NA VIZINGITI VYA KAMPENI KILA KONA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU OKTOBA MWAKA HUU.
SIKU moja baada ya mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kuzuiwa na polisi kutembelea wananchi mitaani, Manispaa ya Ilala imeuzuia umoja huo kutumia viwanja vya Jangwani kufungua kampeni zao keshokutwa kwa maelezo kuwa vimewahiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ukawa inayoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD iliomba kufanya mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu katika viwanja hivyo Agosti 29.
Awali Ukawa waliomba Uwanja wa Taifa, lakini walikataliwa kwa maelezo kuwa uwanja huo ni wa Serikali na hauruhusiwi kutumika kwa shughuli za kisiasa.
KAULI YA MANISPAA YA ILALA
Jana Manisipaa ya Ilala ililieleza MTANZANIA kwamba CCM, tayari waliomba kutumia viwanja vya Jangwani Agosti 23 kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni zao na siku tatu zaidi kuanzia Agosti 28 hadi 30 kwa matumizi mengine ya kisiasa.
Ofisa Utamaduni wa Manispaa ya Ilala, Claud Mpelembwa alisema kuwa Ukawa walichelewa kuomba viwanja hivyo, kwani CCM licha ya kuvitumia Agosti 23, wameviomba tena Agosti 28, 29 na 30 kwa ajili ya shughuli zao za kisiasa.
“Hatujawanyima uwanja, hata barua tuliyowaandikia wanayo inajieleza. Unajua Jangwani ni mojawapo ya maeneo ya wazi, mtu yeyote anaweza kuomba. Ukawa wao waliomba Uwanja wa Taifa na baada ya kukataliwa hawakuleta maombi kwetu.
“CCM waliomba kutumia Agosti 21, 22 na 23 na kisha wakaomba tena kutumia Agosti 28, 29 na 30. Chadema wamekuja kuomba Agosti 24. Walipokuja tukasema basi tukae tuongee, tunaweza kuwapatia Septemba 3,” alisema Mpelembwa.
Alisema kwa kuwa ndiyo kwanza kampeni zimeanza, bado wanaweza kuzungumza ili wapewe tarehe nyingine.
Hata alipoulizwa kuhusu ratiba ya kampeni inayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inayoviongoza vyama vya siasa kufanya kampeni mkoa kwa mkoa, Mpelembwa alisema ratiba hizo huwa hazipelekwi kwenye manispaa.
“Hizo ratiba huwa NEC hawatuletei, bali ni vyama ndivyo vinakuja na maombi ya viwanja… kwa kuwa huu ni mwezi Agosti, kampeni bado zinendelea hadi Septemba na Oktoba, waje tu kuomba. Siyo dhamira yetu kuwanyima uwanja,” alisema Mpelembwa.
MKURUGENZI NEC
Alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani, Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhan Kombwey, alisema bado hawajapata taarifa kutoka Chadema kuhusu kunyimwa kufanya uzinduzi wa mkutano wa kampeni kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.
“Bado sijapata taarifa yoyote kutoka Chadema kama kuna tatizo kama hilo, ngoja niwasaliane kwanza na Chadema pamoja na Manispaa ya Ilala halafu nitakupatia jibu sahihi,” alisema.
UWANJA WA TAIFA
Hivi karibuni Serikali ilikataa ombi la Chadema la kutumia Uwanja wa Taifa kuzindulia kampeni zake.
Akitoa majibu ya Serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Assa Mwambene, alisema kwa mazingira ya sasa hayaruhusu kutumika kwa uwanja huo kwa ajili ya mihadhara ya vyama vya siasa.
“Kwa kipindi hiki haturuhusu Uwanja wa Taifa kutumika kwa mihadhara ya kampeni za vyama vya siasa. Uamuzi huu unalenga kuweka uwanja katika mazingira rafiki ya michezo na kuepuka athari zozote zinazoweza kujitokeza kutokana na mihemuko ya kisiasa.
“Ni kweli kwamba tulipata barua ya Chadema kuomba Uwanja wa Taifa kutumika kwa ajili ya mhadhara wa kisiasa wa Chadema, hasa kuzindua kampeni zao kwenye uwanja, tayari tumeshawaandikia kuwaarifu kuwa uwanja ule hauwezi kutumika kwa ajili ya shughuli zozote za kisiasa,” alisema Mwambene.
JAMES MBATIA
Awali kabla ya kutolewa kwa kauli ya Manispaa ya Ilala, Mwenyekiti mwenza wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema mkutano huo uko palepale hata kama wamezuiwa.
Mbatia pia alilalamikia kitendo cha vyombo vya usalama na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuingilia harakati zao za siasa huku vikiipendelea CCM.
“Sasa tunasema tutazindua kampeni zetu Jangwani kama tulivyopanga. Tumefuata taratibu zote, tumeandika barua, lakini tulipotaka kulipia, tukaambiwa kuna watu wameshaomba lakini hawataki kumsema,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Tulifuata taratibu zote baada ya kunyimwa Uwanja wa Taifa ambao uko kwa ajili ya shughuli mbalimbali, na ni kwa ajili ya Watanzania wote…Ukisema uchaguzi ulio huru na wa haki siyo siku ya kupiga kura tu bali hata mambo kama haya.”
MIZENGWE KILA KONA
Mbali na kuzuiwa kutumia viwanja vya Jangwani kuzindulia kampeni zao, Mbatia alilalamikia upendeleo unaofanywa na viongozi wa Serikali na vyombo vya dola kwa CCM huku vikikandamiza vyama vya upinzani.
“Kwa sheria ya sasa, chama tawala (CCM) kinashiriki uchaguzi kama chama dola. Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alikataza mikutano na mikusanyiko ya vyama vya siasa kwa kuwa vyama vyote vimetia saini maadili. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam naye alisema anatii agizo la mkuu wake wa kazi,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Jumapili Mkuu wa Mkoa Sadiki alikuwa Jangwani kwenye mkutano wa CCM uliofanyika hadi saa moja kasoro wakati ulitakiwa uishe saa 12 kamili jioni. Kamanda Kova naye alikuwepo na alipigia saluti uvunjwaji wa sheria na taratibu. Nilimpigia IGP Ernest Mangu simu kumweleza.”
Alisema katika mkutano huo, Rais Jakaya Kikwete alisimamia uvunjwaji wa sheria na taratibu huku kukiwa na lugha chafu zilizotolewa na viongozi wa CCM, akiwamo Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyesema “watu wanaotaka kuleta ukombozi wa kisiasa ni wapumbavu na malofa”.
Huku akitaja matukio mbalimbali, Mbatia alisema hujuma zilianza muda mrefu ambapo Agosti 12, mgombea urais wa Ukawa, Lowassa, akiwa na msafara wake walizuiwa kwenda kumzika kada wa zamani wa CCM, Peter Kisumo wilayani Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.
“Kampeni zimeanza, mgombea wetu anakwenda kuangalia hali za wananchi na masoko mitaani. Leo alitakiwa aende hospitalini, wamemzuia. Mbona mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu jana alikwenda kutembelea hospitali? Hivi mimi nikitaka kwenda sokoni lazima niombe kibali? Mbona Mkurugenzi wa NEC hamzungumzii Samia? Mbona hazungumzii CCM kupitisha muda wa mkutano?
“Hivi karibuni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alitoa kauli za kuudhi kwa Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo, naye alimsamehe. Lakini polisi walimkamata na kumfungulia kesi. Mbona viongozi wa kitaifa wametukana matusi na hawakamatwi?” alihoji Mbatia.
MATUMIZI YA HELIKOPTA
Juzi, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeonya kuhusu matumizi ya helikopta maeneo ya hatari na mikusanyiko ya watu katika kipindi cha uchaguzi.
Chadema imekuwa ikitumia helikopta katika harakati zake za siasa tangu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kwenye chaguzi ndogo na operesheni zake mbalimbali za kisiasa.
Mwaka 2010, CCM nayo ilifuata nyayo za Chadema na kutumia helikopta kwenye uchaguzi mkuu na ikatumia tena katika mchakato wa kupata mgombea wake wa urais mwaka huu.
Hata hivyo, mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema hatatumia helikopta katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu.
Katika taarifa yake, Kaimu Mkurugenzi wa TCCA, Charles Chacha, ameonya matumizi ya helikopta katika kampeni za uchaguzi kwa maelezo kuwa kuna uwezekano wa kuleta athari za kiusalama.
“Mamlaka inatambua kwamba matumizi ya helkopta wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 yanatarajiwa kuongezeka na kuna uwezekano wa kuleta athari za kiusalama kwa maisha ya watu na mali pamoja na watumiaji wa vyombo hivi.
“Pia vitendo vya kuning’niza vitu kama mabango ya matangazo mbalimbali kwa kutumia ndege (helkopta ikiwamo) yanaweza kuleta hatari endapo sheria na taratibu zinazohusiana na matumizi hayo hazitazingatiwa,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imezungumzia mahitaji ya jumla ya kiuendeshaji, usalama wa eneo la kutua na kuruka, usimamizi wa chombo kikiwa angani na usalama kwa umma, kuchukua na kuangusha vitu ardhini na kupeperusha mabango angani na kutoa taarifa za matukio.
DONDOO MUHIMU
Agosti 23: Mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM ulipitisha muda hadi saa 12: 40 wakati muda sahihi ni saa 12:00. Katika mkutano huo, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alitoa kauli za kuudhi akisema ukombozi wa nchi umeshapatikana kupitia kwa vyama vya TANU na ASP, hivyo wanaotafuta ukombozi sasa ni wapumbavu na malofa.
Si NEC, Jeshi la Polisi wala Msajili wa Vyama vya Siasa aliyekemea au kutoa adhabu kwa vitendo hivyo vya CCM
Agosti 24: Mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa, alipanda daladala kutoka Gongo la Mboto na kwenda Mbagala jijini Dar es Salaam kujua hali za wananchi mitaani na Agosti 25 akatembelea masoko ya Tandale, Tandika na Kariakoo, na siku hiyohiyo polisi wakapiga marufuku ziara zake hizo.
Agosti 25: Lowassa alipanga kutembelea baadhi ya hospitali za umma Agosti 26, lakini siku moja kabla -Agosti 25, Wizara ya Afya ikatoa tamko la kukataza wagombea kwenda hospitali.
Wakati ikitoa tamko hilo, Agosti 25 hiyohiyo, mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu, aliwatembelea wagonjwa katika Hospitali ya Huruma, Rombo mkoani Kilimanjaro.
0 comments:
Post a Comment