BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MGOMBEA URAIS WA CCM DKT JOHN MAFUGULI KUSITISHA MFUMO WA KUWAKOPA WAKULIMA, AAHIDI KUTUMIA MFUMO WA PESA KWA PESA.

Mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan akiwa amemkumbatia kichanga alipotembelea wodi ya wazazi katika Zahanati ya Hedaru Jimbo la Same Magharibi , mkoani Kilimanjaro jana wakati akifanya kampeni. Picha na Emmanuel Herman.

Katavi/Same.
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli ameanza rasmi kampeni akiwa Mkoa wa Katavi na kuahidi kuacha kuwakopa wakulima mazao akisema atatumia mtindo wa “pesa kwa pesa”.

Mgombea huyo aliwasili Mpanda saa 4.10 asubuhi na kuanza safari ya kuelekea Mishomo ambako aliahidi kuboresha huduma za barabara, umeme, maji, elimu na kukomesha kitendo cha Serikali kuwakopa wakulima mazao yao.

“Suala la Serikali kuwakopa wananchi mazao yao katika Serikali ya awamu ya tano nitalikomesha, itakuwa pesa kwa pesa. Nafahamu mnalima sana tumbaku, hivyo nitahakikisha mazao yenu mnapopeleka sokoni kama ni tumbaku lazima upate fedha zako,” alisema.

Alisema akipatiwa ridhaa ya kuwa rais, atajenga barabara za Mpanda hadi mpakani mwa Uvinza, Mpanda hadi Tabora na Mpanda-Kanoge-Ukala kwa kiwango cha lami.

“Tukitengeneza barabara, vijana na kina mama watapata ajira, wawekezaji wataanzisha viwanda ama vya karanga au tumbaku,” alisema.

Baraza la mawaziri
Alisema akichaguliwa ataunda baraza la mawaziri la kuwahudumia wanyonge atakalosimamia kikamilifu.

Akihutubia mamia ya wakazi wa Mpanda katika Viwanja vya Azimio, Dk Magufuli alisema: “Nitakuwa rais mkali kweli kwa baraza langu. Nataka baraza nitakalolichagua liwe kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hasa wanyonge. 


Nataka Tanzania yenye neema, Tanzania yenye maendeleo, nataka Tanzania itakayotoa ajira kwa Watanzania wote. Mimi siyo mkali sana lakini nikichaguliwa nitakuwa mkali sana kwa mawaziri ili niwafukuze harakaharaka,” alisema na kushangiliwa.

Akiwa katika Kijiji cha Majalila aliposimama kwa muda, alisema Serikali imeshafanya usanifu na upembuzi yakinifu wa Barabara ya Mpanda-Uvinza yenye urefu wa kilomita 194 lakini itaanza na kilomita 30 na kumalizia zilizobaki.

Alisema anataka Waziri wa Ujenzi atakayemteua afanye kazi kuliko yeye.

Katika Kijiji cha Vikonge, mgombea huyo alisema Serikali yake itaendeleza ujenzi wa zahanati na hospitali kila kijiji, kata, wilaya na mkoa.

Aliwatoa hofu wakazi wa eneo hilo wenye asili ya Burundi waliopatiwa uraia akisema wataendelea kuishi kwa amani na hakuna atakayewasumbua.

Akimtambulisha, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema chama hicho hakikufanya makosa kumteua Dk Magufuli ambaye alimwita ni “jembe”, tingatinga, “mwanamume wa shoka”.

Samia na wagonjwa
Wakati Magufuli akiwa Katavi, mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan jana alizindua kampeni mkoani Kilimanjaro akiwaahidi wananchi kuwa Serikali ijayo chini ya chama hicho tawala, itatoa Sh50 milioni kila wilaya kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.

Aliwataka wananchi kutowapigia kura wagombea wagonjwa kutoka vyama vya upinzani.

“CCM ina wagombea wazuri ambao siyo wagonjwa,” alisema.CHANZO:MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: