BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAGOMBEA WAEPUKE KAMPENI ZA UHASAMA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 25 TANZANIA.

Vyama vya siasa vilivyokamilisha vigezo vilivyowe kwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuingia katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini kote Oktoba 25, mwaka huu, vimepata kibali rasmi cha kuanza kampeni za kunadi sera za vyama vyao ili kuwashawishi wapiga kura kuchagua viongozi na vyama wavipendavyo.

Mara ya mwisho Uchaguzi Mkuu ulifanyika nchini Oktoba 2010, na kwa kiwango kikubwa wagombea waliweza kujinadi kwa sera za vyama vyao bila kuwepo na matusi, kashfa, kejeli na ghasia nyingine ambazo zingesababisha kuwepo na uvunjifu wa amani nchini.

Ni dhahiri kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kumejitokeza mwamko mkubwa wa kisiasa kwa wananchi kwa kufuatilia kwa ukaribu sera pamoja na mawazo, mitazamo pamoja na mapendekezo ya wagombea na vyama vyao, na kutathmini kama wanayoyaahidi kwao yanaweza kutekelezwa kwa faida ya maendeleo yao na taifa.

Katika kipindi hiki, wagombea wa nafasi tatu za urais, ubunge pamoja na udiwani watakuwa na fursa ya kuuza sera, miongozo pamoja na dira za vyama vyao kwa wapiga kura, ni wakati muhimu sana kwa mustakabali wa taifa hili kutokana na ukweli kuwa viongozi bora watakaochaguliwa kidemokrasia, watakuwa dira ya kusogeza mbele maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wake.

Tunaamini kuwa kipindi hiki cha kampeni, kitakuwa na msisimko wa pekee kwa wengi kutokana na mwamko wa kisiasa ulivyo miongoni mwa wananchi wengi, hata hivyo tunachotarajia ni kampeni ambazo zitahusu masuala ya kijamii zaidi, hatutarajii kusikia wagombea wakishambuliana na kuchafuana wao kwa wao kwa masuala binafsi.

Tunaamini kuwa kwa binadamu kutofautiana kimawazo ni jambo la kawaida, na pia kuwa na itikadi tofauti au kuwa na mawazo na fikra zinazotofautiana katika masuala ya siasa isije ikasababisha uvunjifu wa amani na kuharibu umoja na mshikamano wa kitaifa uliopo.

Ni dhahiri kuwa wale waliopewa dhamana ya kusimamia sheria na ulinzi wakati wa kipindi hiki cha kampeni hadi uchaguzi, watafanya hivyo kwa ukamilifu na nidhamu kubwa ili kuhakikisha amani inadumu, hakuna haja ya kufanya ubabe kwani mwisho wa yote, amani na ustawi wetu ndiyo rasilimali kubwa kupita vyote.

Mara nyingi amani hutoweka pale ambapo wagombea hufanya hila za kupata ushindi kwa njia na gharama zozote, ni wakati huo ambapo wagombea husahau wajibu wao wa msingi wa kuwatumikia wananchi na badala yake huangalia maslahi yao binafsi, wananchi wanatarajia viongozi wawasaidie kuondokana na umaskini, wapate elimu bora, huduma za afya, masoko ya mazao yao na huduma nyinginezo muhimu.

Tunaamini katika amani, mshikamano na umoja kama nguzo na tunu adimu ya taifa letu, tunaamini kuwa nguvu ya kutufikisha mwisho wa mchakato huu kwa utulivu itapata msukumo pia kutoka kwa viongozi wa dini, serikali na wa kijamii watakapokuwa wakikemea hotuba zote za uchochezi na maneno mengine ya kuchafuana na kushambuliana.

Tungependa kuwashauri wapiga kura kuwa wawe makini kwa kuwasikiliza wagombea wa ngazi zote, kuwachambua, na hatimaye wafikie maamuzi sahihi ya kumchagua kiongozi atakayewaletea maendeleo, waepuke kushabikia kwa jaziba vyama au mgombea na waonyeshe ukomavu wa kisiasa kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani. CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: