CELINA KOMBANI KUAGWA UKUMBI WA KARIMJEE KABLA YA MWILI WAKE KUSAFIRISHWA MOROGORO KWA MAZISHI KESHO.
Marehemu Celina Kombani enzi za uhai wake.
MWILI wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani, utaagwa leo katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kwenda nyumbani kwake mkoani Morogoro kwa ajili ya maziko yatakayofanyika kesho shambani kwake.
Akitoa taratibu za mazishi kwa waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu Mikocheni, Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama alisema serikali pamoja na familia ya marehemu wamekubaliana kuwa mwili huo uzikwe nyumbani kwa marehemu mkoani Morogoro.
Mhagama alisema mwili wa marehemu utaagwa leo katika Viwanja vya Karimjee kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nane mchana kisha kusafirishwa kwenda mkoani Morogoro. Mwili huo utasafirishwa kwa njia ya barabara hadi mkoani Morogoro na utafikishwa moja kwa moja nyumbani kwake katika eneo la Forest Hill ukisindikizwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na Bunge.
Baada ya kuwasili mkoani hapo, ratiba mbalimbali zitafuata ikiwemo ibada ya kumwombea marehemu kwa mujibu wa dhehebu lake na kisha kuzikwa kesho shambani kwake Lukobe, nje kidogo ya mkoa wa Morogoro.
Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, Peter Munuo, Kombani aliyefariki dunia Alhamisi Septemba 24, mwaka huu katika Hospitali ya Apollo nchini India alikokuwa akitibiwa, ameacha watoto watano; wa kike wanne na mvulana mmoja pamoja na wajukuu wanne.
Mwili wake uliwasili nchini juzi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa serikali, ndugu, jamaa na marafiki na kisha kupelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo.
Katika hatua nyingine, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma imetoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na Serikali kwa ujumla kutokana na kifo cha Kombani. Kombani aliyezaliwa mwaka 1959, kabla ya wadhifa wake wa sasa, aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) kati ya mwaka 2008 hadi 2010.
Nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri wa Tamisemi, Ofisa Mtawala Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Kilimo, Meneja wa Kiwanda cha Ngozi Morogoro pamoja na Ofisa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment