BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MGOMBEA URAIS UKAWA AGEUKWA NA SWAHIBA WAKE WA KARIBU KATIKA MKUTANO WA KAMPENI WA DK MAGUFULI CHATO, AITWA DHAIFU NA ASIYEFAA KUPEWA MADARAKA KAMA YA URAIS.

 
Mgombea urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Dk. John Magufuli, amepata mapokezi makubwa ambayo yanaweza kufananishwa na gharika kutokana na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika jimbo lake la Chato.

Dk. Magufuli alipokelewa na umati wa wananchi ambao wengine walianza kumsindikiza kwenda uwanja wa mpira wa Chato wakati anatoka nyumbani kwake katika kijiji cha Mlimani maeneo ya Chato mjini mkoani Geita alipokuwa kwa mapumziko ya siku moja.

 
Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli.

Jimbo la Chato liko mkoani Geita na mgombea huyo wa urais wa CCM amekuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 20 na kwa miaka kumi mfululizo alipita bila kupingwa.

Wananchi wenye bendera za CCM na mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kumuunga mkono mgombea huyo wa CCM walisimama barabarani huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Baadhi ya mabango yalisema: ‘Dk. Magufuli umethubutu umeweza, tunakuamini, tunakupenda, tumekukubali, ukitaka mabadiliko chagua tinga tinga, tuna imani na Magufuli kero yetu maji’.

Mabango mengine yalisema walimu CWT (Chama cha Walimu Tanzania) tutakupa kura Magufuli, Magufuli wewe ni jembe, mafisadi sasa mwisho, pembejeo za kilimo haraka, mafisadi wanakuogopa.

Mkutano wa Chato ndiyo umevunja rekodi ya kuchukua muda mrefu kuliko mikutano mingine kwani ulianza saa saba na nusu na kumalizika saa 12 jioni.

MKE WAKE
Mke wa mgombea huyo wa CCM alikuwa kivutio kwenye mkutano huo aliposimama kwa mara ya kwanza kumnadi mumewe tangu kuanza kwa kampeni hizo Agosti 25, mwaka huu.

Janeth aliwashukuru wana-Chato kwa kujitokeza kwa wingi kumuunga mkono mgombea huyo wa CCM ambaye alikuwa Mbunge wao kwa kipindi cha miaka 20 mfululizo.

“Nawashukuru sana wana-Chato mahudhurio haya makubwa ni heshima kubwa kwa Mbunge wenu kwa muda wote huo aliowatumikia na sasa CCM wamemuona anafaa wamemteua kugombea urais hivyo msifanye makosa Oktoba 25 ni Dk. John Magufuli maana anatosha,” alisema.

Hotuba ya Janeth Magufuli ilikatishwa kwa dakika kadhaa kwa kelele za wananchi hao waliomtaka asimwite Dk. Magufuli Mbunge na badala yake amtambulishe kama Rais.

Wananchi hao walisikika wakishangilia kwa nguvu Dk. Magufuli: Rais, Rais, Rais. 


Aliyekuwa kambi ya Lowassa awa kivutio.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ ambaye alikuwa swahiba mkubwa wa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chadema, Edward Lowassa, alikuwa kivutio kwenye mkutano huo kutokana na kumgeuka na kuanza kumrushia makombora.

Msukuma ambaye wakati Lowassa anatangaza kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais mkoani Arusha alishuka kwa helikopta kabla ya kuhamia Chadema, kwenye mkutano huo alisema Lowassa ni dhaifu na mwenye tamaa ya madaraka ambaye hafai kupewa madaraka makubwa kama ya urais.

Alisema yeye ni mtu ambaye anaweza kumwelezea kwa ufasaha Lowassa kwasababu alikuwa rafiki yake mkubwa na wametembea naye sehemu mbalimbali nchini.

“Mimi nimemtembeza Lowassa kwenye helikopta yangu nchi nzima namfahamu vizuri kuliko mtu yeyote, inawezekana watu wanamshabikia bila kumjua sasa nawaambia wana-Chato kwamba tuchague Rais msafi ambaye hana kashfa na huyu si mwingine ni Dk. Magufuli msifanye majaribio,” alisema.

Dk. Magufuli ashangazwa mapokezi
Dk. Magufuli aliwashukuru wananchi wa Chato kwa mapokezi makubwa na kusema hayajawahi kutokea kwenye mikutano yake mingi aliyoifanya tangu kuanza kwa kampeni hizo Agosti 25, mwaka huu. 


Alisema yeye ni mtetezi wa wanyonge na hasa Watanzania maskini, hivyo serikali yake itajitahidi kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi na kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana ili wajikwamue kiuchumi.

BULEMBO AMJIBU MBOWE
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa, Abdallah Bulembo, alisema chama chake hakitabadilisha kauli mbiu ya Magufuli for Change ( M4C) ambayo imelalamikiwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kwamba chama hicho kimeiba kutoka kwao.

Alisema anashangaa Mbowe kulalamika kwamba CCM imeiba nembo yao, huku akisahau kwamba hata mavazi yanayovaliwa na chama chake hivi sasa yaliwahi kuvaliwa na akina waasisi wa CCM kama Mzee Mfaume Rashid Kawawa. CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: