BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

AKAUNTI FEKI ZA WhatsApp ZAFUNGULIWA KWA FUJO KWA LENGO LA KUWACHAFUA VIONGOZI, MWAPACHU AADHIRIKA.

Zikiwa zimebaki siku 33 kuanzia leo kabla ya kufikiwa kwa siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, hofu imeanza kutanda juu ya kuwapo kwa usambazaji wa taarifa potofu kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp zinazoweza kuwavuruga wananchi ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe unaonyesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa wiki, tayari athari za matumizi mbaya ya mtandao huo kuelekea uchaguzi mkuu zimeshaanza kujitokeza baada ya viongozi wa kisiasa na watu kadhaa maarufu kuanza kuandamwa kupitia akaunti bandia za WhatsApp, baadhi yao wakiwa ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Juma Mwapachu.

Wiki iliyopita, Balozi Mwapachu aliiandikia barua rasmi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kulalamika jina lake kuonekana likiwa na akaunti ya WhatsApp iliyounganishwa katika kundi lililokuwa likijadili mambo mbalimbali yaliyokuwa na dhamira ya kumchafua. 


Wengine walioonekana kuwa na akaunti hizo na kisha kuwa katika kundi la Whatsapp lililokuwa likishiriki mjadala asioujua Mwapachu ni mbunge wa zamani wa Jimbo la Igunga, Rostam Aziz; waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrance Masha; Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda na Mkurugenzi wa Hali Halisi Publishers anayegombea ubunge Jimbo la Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saeed Kubenea.

Kadhalika, wengine wanaodaiwa kukumbwa na kadhia kama hiyo ni makada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) waliokuwa na kundi la 'Whatsapp' liitwalo JPM , ikiwa ni kifupi cha John Pombe Magufuli. Baadhi yao ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angela Kairuki; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba na Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde 'Kibajaji'.

Katika makundi yote hayo ya WhatsApp, wahusika walionekana wakiwa na majina yao halisi na ilidaiwa kuwa kuna mtu alinasa mjadala wao na kupiga picha (screen shot)kabla ya kuvujisha kwa umma, hivyo kuweka wazi kile kinachoitwa kuwa ni majadiliano ya siri ya wahusika yenye nia ya kuhujumu kundi jingine hasimu katika siasa.

Uchunguzi wa Nipashe umedhihirisha kuwa upotofu wa taarifa zinazosambazwa na baadhi ya watu wenye nia ovu kupitia anuani na makundi bandia ya WhatsApp waweza kuwa tishio zaidi kadri siku ya uchaguzi mkuu inavyokaribia.

Hofu hiyo inayothibitishwa na wataalamu kadhaa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) waliozungumza na Nipashe inazidishwa pia na ukweli kuwa ni rahisi sana kuanzisha akaunti bandia za WhatsApp.

Kwa sababu hiyo, vyanzo mbalimbali vimeiambia Nipashe kuwa upo uwezekano mkubwa wa kusambazwa kwa matokeo feki baada ya uchaguzi kufanyika Oktoba 25, na hivyo kuwachanganya baadhi ya watu ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.

Kufuatia uwapo wa hofu ya WhatsApp, Nipashe ilifanya uchunguzi zaidi uliowashirikisha wataalamu kadhaa wa Tehama na kubaini kuwa zipo njia nyingi zinazoweza kutumiwa kuanzisha akaunti za uongo katika mtandao wa WhatsApp na pia makundi ya uongo ya mtandao huo.

AKAUNTI BANDIA WHATSAPP
Katika uchunguzi huo, Nipashe ilibaini kuwa zipo njia tatu rahisi za kuanzisha akaunti bandia ya WhatsApp na ambazo, mamlaka zinazosimamia udhibiti wa mawasiliano kwenye mtandao zinapaswa kutafuta majawabu sahihi ya namna ya kuzuia athari zake.

Mosi, inaelezwa kuwa ni kusajili laini za simu za idadi sawa na majina ya wahusika na kisha kuzianzishia makundi ya mtandao wa WhatsApp (group) pasi na wenyewe (wenye majina) kujijua. Pili ni kwa mtu mmoja kushirikiana na wenzake zaidi ya mmoja kuhakikisha kuwa anahifadhi namba za marafiki anaoshirikiana nao na zilizo na akaunti za WhatsApp kwa majina ya uongo ya watu wanaotaka kuwachafua. 


Njia ya tatu inayohitaji fedha nyingi kidogo, ni kwa mtu mmoja kuwa na simu zaidi ya moja kulingana na idadi ya watu anaotaka kuwachafua na kisha kuendesha mijadala bandia yeye mwenyewe kabla ya kupiga picha na kusambaza kwa umma kuonyesha kuwa majadiliano hayo ni ya watu wale aliodhamiria kuwachafua.

Kadhalika, hatari kubwa kwa taifa ni uwezekano wa kuanzishwa kwa makundi ya WhatsApp yatakayokuwa yakionyesha majadiliano batili, pengine kati ya viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na viongozi wa vyama fulani, kuonyesha jamii kuwa kuna mbinu zinafanywa ili kubadili matokeo ya uchaguzi mkuu.

"Hilo ni jambo la hatari sana. Ni vizuri jamii ikaelezwa kwa kina juu ya udhaifu huu wa WhatsApp ili kila mmoja ajue ukweli na kuacha kuhamaki pindi akikutana na upotoshaji wa aina hiyo, " alisema mtaalamu wa Tehama, Gasper Gaetano, wakati akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki.

"Jamii inapaswa kutambua ukweli huu kuhusu WhatsApp. Kwamba ni mtandao mzuri, lakini ni rahisi kuanzisha akaunti za uongo na hivyo wasichanganywe na baadhi ya taarifa zake. Kadiri tunavyokaribia uchaguzi, ndivyo kila mmoja anavyopaswa kuwa macho zaidi na ujumbe unaosambazwa kwenye WhatsApp ili kuepuka taarifa za uzushi, hasa kuhusiana na matokeo," aliema Gaetano.

USAJILI WA LAINI BANDIA
Kwa mujibu wa wataalamu wa Tehama, njia hii ni mojawapo kubwa kati ya zile zinazotumiwa sana na waovu.


Kisheria, kila laini mpya ya simu humlazimu anayeimiliki kuisajili ndipo iingizwe kwenye mfumo na kuanza kuitumia. Hata hivyo, uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa jambo hili linaonekana kuwa na udhaifu mkubwa. Kinachotokea ni kwamba yeyote huweza kusajili laini mpya kirahisi, tena hata kwa kutumia vitambulisho bandia.

Uchunguzi umebaini kuna upatikanaji holela wa laini za simu na ambazo pia ni rahisi kusajili. Kampuni zinazotoa huduma ya simu na kutakiwa zihakikishe kuwa zinakwepa udanganyifu katika usajili, nazo zinaonekana kushindwa kudhibiti hali hiyo kutokana na ushindani mkali wa kibiashara miongoni mwa wauzaji wa bidhaa zao, hasa mawakala wa mitaani wanaosajili wateja wao bila kuthibitisha kwa kina uhalali wa wahusika na vitambulisho vinavyotumiwa kwa kazi hiyo.

Katika kujiridhisha, mwandishi mmojawapo wa Nipashe alikwenda kwenye duka mojawapo la vifaa vya shule na ofisini (stationery) na kutengeneza kirahisi vitambulisho vinne vyenye majina ya kubuni ya Halima Kondo, Jesca Joel, Abdul Ibrahim na Christopher Mawazo. 


Wote hawa walionyeshwa kuwa ni wafanyakazi wa kampuni ya kubuni tu iitwayo Streika na kila kitambulisho kilikamilishwa kwa gharama ya Sh. 5,000. Mwandishi alitumia picha ndogo za watu tofauti kwa kipimo maarufu cha pasport size, zote akizipata kutoka kwenye mtandao wa intaneti.


Baada ya kupata vitambulisho hivyo ambavyo havikuwa hata na sahihi za wamiliki wala Mkurugenzi wa kampuni yao, mwandishi alitoa nakala za kila kimoja na kwenda kwa vijana wanaouza na kusajili laini za kampuni za simu, ambako huko alifanikisha lengo kirahisi baada ya kulipia Sh. 1,500 kwa kila laini aliyonunua na kuisajili, huku laini isiyosajiliwa ikiuzwa kwa Sh. 1,000.

Masaa mawili baadaye, laini nne alizonunua mwandishi na kusajiliwa kwa vitambulisho bandia tayari zilishakuwa hewani kwa matumizi, bila ya kujali kuwa majina yote yalikuwa ni ya kubuni tu.

Wakala aliyehusika kwa usajili alionekana pia kutojali wingi wa laini zilizokuwa zikisajiliwa na mtu mmoja, akisema kuwa yeye hajawekewa idadi ya juu ya laini kwa kila mtu anayetaka huduma hiyo na hivyo anachojali ni fedha tu.

Alikuwa akitoa huduma kwa yeyote aliyewasilisha vitambulisho vya kazi, au uraia, au vya kupigia kura na hata barua kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa.

"Hapa mwenye nia ovu anaweza kuamua atumie majina ayatakayo. Ni hapo ndipo unapoweza kuona jina la Osama Bin Laden ambaye alishakufa, ya wanasiasa maarufu au mtu yeyote kutegemeana na mahitaji ya mtenda maovu. 


Kinachofuatia huwa ni kuandaa group (kundi) la WhatsApp la wahusika na kazi hii ni rahisi sana, haichukui hata dakika tano," alisema Juma Mzungu, mtaalamu mwingine wa Tehama jijini Dar es Salaam.

"Baada ya hapo, wachafuzi huvaa uhusika wa walengwa ikiwamo kuendesha mijadala waitakayo na kisha kupiga picha mfululizo wa majadiliano hayo bandia kabla ya kujifanya wanaivujisha kwa umma ikiwa kama picha. Jambo hili ni la hatari na hivyo wananchi wanatakiwa kuwa macho, hasa wakati wa uchaguzi ambako wenye nia mbaya wanaweza hata kutumia akaunti bandia za NEC (Tume ya Taiafa ya Uchaguzi) kwa nia ya kuupotosha umma," anaongeza Mzungu.

MAJINA KWENYE SIMU
Inaelezwa kuwa njia nyingine rahisi ya kuanzisha akaunti bandia ya WhatsApp huhusisha watu zaidi ya mmoja, lakini wenye lengo moja tu la kuchafua kundi jingine la watu au kuupotosha umma kwa taarifa zisizokuwa na ukweli.

Hii hufanyika kwa kuruhusu mmoja wa wahusika katika mchezo huu mchafu kubadili majina ya namba za washirika wake kwenye mtandao wa WhatsApp, akihariri majina halisi na kuweka majina bandia ya watu wanaokusudia kuwatumia kwa ajili ya kusambaza ujumbe wa uongo.

Kwa mfano, kama kuna jina la rafikiye wa mtandao wa WhatsApp liitwalo 'X', waovu hulibadili jina na kuweka lile atakalo, kwa mfano kwa kuliita Jaji Lubuva (Mwenyekiti wa NEC). Hilo hufanyika pia kwa majina mengine yanayolengwa katika uchafuzi huo, labda 'Saddam Hussein', 'Carlos The Jacko' au maafisa wa juu wa NEC.

Baada ya hapo, wahusika huanzisha 'group' hilo la kina Lubuva, wakiruhusu mjadala fulani ambao mwishowe wanaamini wakishaupiga picha na kuweka hadharani utawachafua wahusika kwa kiasi kikubwa au kupeleka ujumbe wautakao kwa umma.

Akifafanua zaidi kuhusu njia hiyo, Mtaalamu wa Tehama jijini Dar es Salaam, Allan Mshana, alisema kwa kawaida WhatsApp huwa haionyeshi jina la mtu anayepokea ujumbe bali anayetuma, hivyo majadiliano huonyesha majina ya wahusika bila kumhusisha mpokeaji.

"Njia hii pia ni rahisi sana ijapokuwa huhitaji watu zaidi ya mmoja kuchafua wengine," alisema Mshana.

MTU MMOJA, LAINI ZA SIMU ZAIDI YA MOJA
Uchunguzi wa Nipashe umebaini vilevile kuwa ipo njia ya tatu ambayo hii hailazimishi kuwapo kwa watu wengi licha ya kwamba walengwa wa uchafuzi husika huweza kuwa zaidi ya mmoja.

Mtaalamu wa Tehama aitwaye Estomieh Mollel wa Mikocheni jijini Dar es Salaam aliiambia Nipashe kuwa njia hii ni ya gharama kwani humlazimu anayeifanya kazi hiyo kuwa na simu zaidi ya moja, kulingana na idadi ya watu anaotaka kuwahusisha katika kundi bandia litakaloshiriki majadiliano ya kuwachafua.

Alifafanua kuwa, kama walengwa wako tisa, basi anayefanya kazi ya kuwachafua wahusika huwa na simu tisa zilizounganishiwa huduma ya WhatsApp, lakini zikiwa na laini zenye majina ya walengwa.

Baada ya hapo, mhusika (wa uchafuzi) huanzisha kundi na mwishowe kujianzishia mjadala wenye majina ya watu anaowataka kabla ya kupiga picha na kusambaza kwa umma.

KWA NINI WHATSAPP ?
Mollel anasema mtandao wa WhatsApp ni rahisi kuutumia katika kuchafuana kwa sababu wenyewe usalama wake wa taarifa huwa ni mdogo. Watumiaji hawalazimiki kuwa na nywila (password) kufungua wala kuwa na taarifa binafsi za ziada katika usajili.

Kikubwa kwao ni kuwa na namba za laini za simu zao tu na mengine yote yaliyobaki hufanyika kirahisi zaidi kulinganisha na mitandao mingine ya kijamii kama twitter, instagram na facebook. Bali, inaelezwa zaidi kuwa simu inayotumika kusajili WhatsApp hutambua jina la awali lililotokana na e-mail iliyotumika wakati wa kuisajili, hivyo hata laini nyingine inapowekwa kwenye simu husika bado ujumbe huonekana kuwa unatoka kwa mwenye jina lililotumika awali.

KUBAINI KUNDI ‘FEKI’
Katika uchunguzi wake, Nipashe limebaini kuwa ipo changamoto kwa umma kutambua kuwa majadiliano fulani ni bandia kwani wanaochafua wenzao hujitahidi kadiri wawezavyo kuanzisha makundi wakitumia majina yaleyale ambayo walengwa huyatumia katika WhatsApp zao za kweli.

"Njia mojawapo inayoweza kutambua akaunti bandia ni juu ya maudhui ya kile kinachoandikwa... ni kwa sababu kila mtu ana namna yake ya kuelezea jambo na hilo linaweza kusaidia utambuzi wa kile kinachojadiliwa kuwa ni cha kweli au cha uzushi," anasema Mollel.

ATHARI KWA JAMII
Mzungu ambaye ni mzoefu wa masuala ya Tehama alisema matumizi mabaya ya mtandao wa WhatsApp yanaweza kusababisha athari kubwa katika jamii, Alisema mbali na uwezekano wa kuwachanganya watu wakati wa uchaguzi, baadhi ya athari za kutumiwa kwa akaunti bandia za WhatsApp ni watu kupoteza ajira zao; ndoa kuvunjika na pia amani ya nchi kuwekwa rehani.

Akifafanua kuhusu hilo, Mzungu anasema: "Mtu anaweza kuwachafua wafanyakazi wa kampuni au kitengo fulani kwa kuonyesha kuwa wanaisema vibaya kampuni yao. Hili linaweza kuhatarisha ajira ya wahusika," alisema.

Athari nyingine ni uwezekano wa kuvunjika kwa ndoa pindi mmoja wa wapendanao akatengenezewa 'fitna' na wabaya wake kuonyesha kuwa anawasiliana kimapenzi na mtu mwingine.

TCRA WANENA
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Ally Yahaya Simba, alipoulizwa alisema kuwa kisheria, kuanzisha anauani bandia za WhatsApp na kuchafua watu wengine ni makosa ya jinai na kwamba, hatua ya kwanza ambayo mlalamikaji anapaswa kuichukua ni kwenda kutoa taarifa polisi.

Alisema baada ya hapo, kama polisi ikaona kesi hiyo inahitaji kuishirikisha TCRA, wao wako tayari kutoa ushirikiano wakati wote.

"Polisi wanapotushirikisha maana yake ni kwamba wanataka kupata taarifa za kitaalamu na ambazo sisi tunazo. Ndiyo maana tunasema siyo sahihi kwa mtu yeyote kuja kwetu moja kwa moja ili kulalamika bali anapaswa kufanya hivyo polisi... kama ni adhabu, sisi tunatoa kwa watoa huduma na siyo vinginevyo," alisema Dk. Simba.

Mkurugenzi huyo alitoa rai maalumu kwa viongozi wa kisiasa na watu wengine mashuhuri kuwa waache kulalamika kwenye vyombo vya habari na badala yake, waende polisi ili hatimaye uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe.

"Ili tuchukue hatua ni lazima tupate ruhusa ya polisi. Sheria Mpya ya Makosa ya Mtandao inaelekeza kuwa ni lazima kibali cha kupeleleza jambo kitoke polisi, hatuwezi kukurupuka tu," alisema Dk. Simba.

WITO KWA KAMPUNI ZA SIMU
Katika hatua nyingine, Kaimu Meneja wa Mawasiliano kwa Umma wa TCRA, Semu Mwakifanjala, alisema mamlaka yao inatambua kuwapo kwa kasoro mbalimbali katika usajili wa laini za simu na mara zote wamekuwa wakizihimiza kampuni za simu kufuata miongozo waliyopewa.

“Tunajua kuna watu wanatumia vibaya mitandao hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi. Tunachoshauri kama kuna viashiria vya jinai, Polisi huingilia kati na kama tukitakiwa kutoa ushahidi huwa tunafanya hivyo,” alisema Mwakifanjala.

POLISI WAZUNGUMZA
Akizungumzia vitendo vya kuchafuana kupitia akaunti za bandia kwenye mtandao wa WhatsApp, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu, alisema ni vigumu jeshi la polisi kutoa kauli kwenye suala hilo ikiwa wahusika hawatapeleka malalamiko rasmi kwao.

Alisema nchi inaelekea kwenye uchaguzi na kwamba, kuwapo kwa vitendo vya aina hiyo kunahatarisha amani na utulivu na hivyo, akawataka wale wote watakaokutwa na matatizo hayo kuchukua hatua ya kuripoti polisi na kutoa ushirikiano wa kina ili wahusika wasakwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

"Siwezi kutoa maelezo zaidi kwa sababu hatujapokea malalamiko... labda kwa kuanzia muwaulize hao waliochafuliwa majina yao wametoa taarifa katika kituo gani cha polisi," alisema IGP Mangu.

SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAO
Suala la kuanzishwa kwa akaunti za uongo limezungumziwa katika Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015, ikiwamo katika kifungu cha 15 ambacho kinakataza mtu kujifanya ni mtu mwingine na mhusika akibainika anapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Maeneo mengine yanayogusia suala hili yapo pia katika kifungu cha 16 kinachozungumzia makosa ya kutoa taarifa za uongo na kupotosha umma.

HISTORIA YA WHATSAPP
Kwa mujibu wa tovuti ya Wikipedia, mtandao wa WhatsApp ni maalum kwa ajili ya simu zenye huduma ya intaneti (smartphones) na huruhusu kutuma ujumbe wa maneno, picha za mnato, video na hata ujumbe wa sauti.

Ulianzishwa Marekani mwaka 2009 na wafanyakazi wa zamani wa mtandao wa Yahoo, Brian Acton na Jan Koum.


Kufikia Januari 2015, mtandao wa WhatsApp ulitajwa kuwa maarufu zaidi duniani na hadi kufikia mwanzoni mwa mwezi huu, tayari ulishakuwa na wafuasi hai zaidi ya milioni 900. Facebook waliununua mtandao wa WhatsApp Februari 19 mwaka jana kwa gharama ya takriban dola bilioni 16 (Sh. trilioni 32). CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: