BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAPAMBE WA WAGOMBEA URAIS VYAMA VYA CCM NA CHADEMA WANONGESHA KAMPENI ZA DK MAGUFULI NA LOWASSA, KAZI KUU NI KUMSAFISHA MGOMBEA WAO TU.


Kutoka kushoto ni mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Edward Lowassa na kulia ni mgombea urais kupitia chama cha Mapinduzi (CCM)Dk.John Magufuli.

Shinyanga, Hai.
Wakati wagombea urais wa vyama vya CCM na Chadema wakijikita kwenye ahadi za mambo watakayofanya iwapo watachaguliwa, wapambe wao wameendelea kufanya kazi ya kujibu kutuma mashambulizi kwenye kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu zinazoendelea kote nchini.

Tofauti na kampeni za mwaka 2010 ambazo wagombea ndiyo waliokuwa mstari wa mbele kulipua mabomu na kukejeli wapinzani wao, mwaka huu Chadema inamtumia zaidi Frederick Sumaye kufanya kazi hiyo, huku CCM ikitumia watu tofauti kutoka kwenye kamati ya kampeni yenye wajumbe 32 pamoja na viongozi wa zamani.

Wagombea hao wawili wamekuwa wakijikita katika kuzungumzia matatizo ya wananchi wa eneo ambalo wanapiga kampeni na kutoa ahadi za kuyamaliza.

CCM imemsimamisha Dk John Magufuli kugombea urais, wakati Chadema imemsimamisha Edward Lowassa ambaye pia anaungwa mkono na NLD, CUF na NCCR Mageuzi ambavyo kwa pamoja vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Sitta amshambulia Lowassa
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga jana, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta alimshukia Lowassa akisema mradi kusambaza maji kutoka Ziwa Victoria ulianza miaka mingi na kusimamiwa na Serikali ya Tanzania na Uholanzi wakati huo Lowassa, ambaye alikuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo wakati wa utekelezaji wake, alikuwa bado mwanafunzi.

Sitta alisema katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu mradi huo ndipo ulianza kusimamiwa na Serikali ya Tanzania chini ya mawaziri mbalimbali.

“Si Lowassa pekee aliyesimamia na kuanzisha mradi huu,” alisema Sitta. “Sasa mbona akisimama jukwaani anajitaja mwenyewe tu, mbona hawataji wenzake. Nawaambieni ndugu zangu viongozi wanaopenda kujikweza kama hawa waogopeni,” alisema Sitta na kushangiliwa.

Dk Magufuli naye alichangia hoja hiyo wakati akijinadi aliposema kuwa mradi huo, ambao umesaidia wakazi wengi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kupata maji, ulianzishwa na kusimamiwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na si Lowassa.

Dk Magufuli, ambaye anajinadi kwa kutumia mafanikio ya ujenzi wa barabara, alisema Lowassa ni mmoja wa mawaziri waliosimamia mradi huo na si yeye aliyeubuni na kuuanzisha kama anavyojinadi katika mikutano yake ya kampeni.

Tangu kuanza kwa kampeni, Lowassa amewaahidi wananchi wa Kigoma, Bariadi na Chato kuwa akiwa, rais atahakikisha wanapata maji kutoka Ziwa Victoria, akieleza kuwa kama aliweza kufanikisha mradi wa maji kutoka ziwa hilo kwenda Shinyanga, hawezi kushindwa katika maeneo hayo.

Lowassa alipokuwa Shinyanga, pia aliwaahidi wananchi wa mkoa huo kuwa akiwa rais watapata maji kutoka ziwa hilo.

Magufuli na barabara
Akijinadi kwenye mkutano huo, Dk Magufuli alisema amejenga barabara nyingi akiwa Waziri wa Ujenzi lakini hawezi kujisifu kuwa yeye ndiye aliyezijenga.

“Siwezi kujisifu kwa kujenga barabara zaidi ya kilomita 17,000 wakati nikiwa waziri wa ujenzi kwa miaka 15 katika Serikali ya Awamu ya Tatu na Nne. Huwezi kuwa na mtoto ukamtuma shambani akachume pamba kisha azilete na kujisifu kuwa zile pamba ni zake,” alisema.

“Eti anasema alileta shule za kata. Hivi alibeba matofali kichwani wakati wa ujenzi wa shule hizi,” alihoji Dk Magufuli akimponda Lowassa ambaye pia, alisimamia ujenzi wa shule za kata wakati akiwa Waziri Mkuu.

Dk Magufuli alisema akiwa rais, atahakikisha kata zote zisizo na maji katika mji wa Shinyanga zinapata maji, huku akisisitiza kuwa maendeleo ni changamoto na kwamba haziwezi kuisha zote.

Waziri huyo wa Ujenzi aliahidi kujenga kilomita 10 za lami katika mji wa Shinyanga mbali na kimomita 32 zilizojengwa mpaka sasa, ujenzi wa soko la kisasa, chuo kikuu cha madini, kufuta ushuru kwa wakulima na kuanzisha viwanda kwa kuhusisha sekta binafsi.

“Shinyanga kuna kero ya kiwanda cha nyama ambacho kinasuasa mpaka kinatia kichefuchefu. Siku nikiapishwa kuwa rais, mwenye kiwanda hiki aidha kifanye kazi au kirejeshwe serikalini,” alisema na kushangiliwa na maelfu ya wananchi.

Alisema ni aibu kwa Watanzania kuwa maskini katika nchi yenye kila aina ya rasilimali.

Sumaye amjibu Magufuli
Wilayani Hai, Sumaye aliendelea na kazi ya kujibu mashambulizi ya CCM na jana alitumia fursa hiyo kumjibu Dk Magufuli aliyesema kuwa utafiti uliofanywa na Twaweza unaoonyesha anaongoza kwa asilimia 65, umempunja ushindi aliostahili.

Sumaye alisema Dk Magufuli hawezi kupata hata asilimia 40 ya kura na ndiyo maana amekuwa akitofautiana na mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Rundugai, Jimbo la Hai, Sumaye alisema Dk Magufuli amekuwa akikisahau hata chama chake na kuwataka wananchi wachague Tanzania ya Magufuli, huku akiomba wananchi wasichome godoro lote lenye kunguni badala yake waue kunguni waliopo kwenye godoro hilo.

“Haiwezekani mkalalia kitanda chenye kunguni si ndiyo,” alihoji Sumaye na kuitikiwa na wananchi “ndiyoooooo”.

“Amesahau hata kusema chagua CCM, anasema chagua Tanzania ya Magufuli,” alisema Sumaye na kuongeza kuwa Tanzania haiwezi kuwa ya Magufuli, bali ni ya Watanzania wote.

Sumaye alisema kuwa hali ya CCM ni mbaya na ndiyo maana wananchi wamechoka na hali zao ni mbaya.

“Wananchi wanataka mabadiliko, hakuna vita itakayotokea kama wanavyohubiri huo ni upuuzi mtupu,” alisema Sumaye.

Sumaye aliwaambia wananchi hao wa Rundugai kuwa nchi nyingi duniani zinapata mabadiliko kwa kubadilisha mfumo uliopo, hivyo wananchi wasiogope kwa kuwa CCM siyo mama yao, bali ni chama cha siasa.

Lowassa na CCM
Wakati Sumaye akisema hayo ,mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa akiomba kura katika mkutano huo alisema kwa mara ya kwanza nchini Tanzania upinzani utachukua nchi.

“Wale wenzangu waliochukia mimi kuondoka CCM, sasa wameanza kukubali uamuzi wangu kwa kuwa CCM imeshindwa kuongoza nchi, haifai tena kuongoza kama Sumaye alivyosema hali ya wananchi ni mbaya sana,” alisema Lowassa huku akishangiliwa.

Lowassa aliendelea kurudia ahadi zake za elimu bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu, pia kuboresha maisha ya Watanzania waondokane na umaskini ambao kila siku amekuwa akisema anauchukia.

Pia, aliwaambia wananchi hao kuwa ataanzisha kituo maalumu cha huduma kwa jamii nchini kote ili kuhakikisha wananchi popote pale wanapokwenda kutafuta huduma wanazipata mahali pamoja kwa haraka zaidi.

“Hiki kituo kitakuwa kikiwasaidia wale wote ambao wamekuwa wakikosa huduma mbalimbali na kuombwa rushwa kupata huduma moja hadi nyingine,” alisema Lowassa.

Ombi maalumu kwa Mbowe
Katika mkutano huo, Lowassa alimsihi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuendelea kuambatana naye kwenye kampeni ili aongeze nguvu kwenye timu yake.

Lowassa alisema Mbowe anaweza kufanya kampeni zake kwenye Jimbo la Hai na kuweka timu ambayo itamsaidia wakati atakapokuwa nje ya jimbo kumpigia kampeni mgombea urais.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbowe aliiponda CCM akisema kwa sasa haijielewi kwa kuwa iko hoi.

Alisema katika uchaguzi huu hawatakubali kuibiwa kura huku akiwaomba askari wakae pembeni ya siasa na kulinda amani ili wanasiasa wacheze ngoma yao wenyewe.

“Askari wetu lindeni amani tuachieni CCM tucheze nao msipendelee upande wowote,” alisema Mbowe.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: