Wakati Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara inatarajia kuendelea tena leo katika viwanja saba nchini, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm, amesema kikosi chake kitashuka kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kuikabili Mtibwa Sugar kikiwa na jukumu moja la kusaka pointi tatu muhimu.
Pluijm alisema kuwa licha ya kuwakosa nyota wake wawili wa kikosi
cha kwanza ambao ni Haruna Niyonzima, ambaye amefiwa na dada yake na
kulazimika kurejea Rwanda na Mbuyu Twite anayetumikia adhabu ya kadi
nyekundu, hana wasiwasi na mchezo wa leo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Pluijm, alisema kuwa haumizi
kichwa kuwakosa wachezaji hao kwa sababu ana wigo mpana wa kuchagua
nyota wengine wa kuziba nafasi hizo.
“Wachezaji waliopo watafanya kazi ile ile, najua mchezo utakuwa
mgumu kwa sababu Mtibwa Sugar ni timu nzuri na imepata matokeo mazuri
katika michezo yote, lakini nitatumia mfumo ambao utanipatia matokeo
mazuri,” alisema Pluijm.Aliongeza kuwa kikosi chake hakitakuwa na
mabadiliko makubwa kiuchezaji ukilinganisha na kile kilichocheza dhidi
ya Simba na hiyo inatokana na kasi na ‘njaa’ ya kuhakikisha ushindi
unapatikana kwenye mechi zote.
“Uchezaji wetu katika mechi ya kesho (leo) utategemea na kasi ya
wapinzani wetu pamoja na mfumo wao kama ilivyokuwa kwa Simba, tutakuwa
tunabadilika kwa kuangalia mazingira ya mchezo unavyokwenda, ” Pluijm
alisema.
Kukosekana kwa Niyonzima na Twite huenda Mholanzi huyo akawaanzisha
viungo Salum Telela na Juma Abdul katika mechi hiyo ambayo Mecky,
Mexime, Kocha wa Mtibwa Sugar, ametamba kwamba anaijua ‘dawa’ ya Yanga.
Mexime alisema kuwa timu yake haina wasiwasi yoyote katika mchezo
huo na kusema kwamba wamejipanga kuisimamisha Yanga na hatimaye kushika
usukani wa ligi.
“Naijua Yanga ni timu kubwa lakini naamini timu yangu ni nzuri na
wasitarajie mteremko kwenye mchezo wa kesho (leo),”alisema beki huyo wa
zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars.
Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, alisema jana kuwa wachezaji wake
wanapaswa kusahau matokeo ya mchezo uliopita na kuelekeza akili zao
kwenye mchezo wa leo na kusahau kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa
mahasimu wao Yanga.
“Ligi bado mbichi huwezi kujua kitakachotokea mbele, tumepoteza
mchezo dhidi ya Yanga na hilo limepita, nataka tuingie uwanjani kesho
(leo) huku tukielekeza akili zetu kwenye mchezo huo, ushindi
utaturudisha kwenye mstari,” alisema Kerr.
Mechi nyingine za ligi hiyo zinazotarajiwa kufanyika leo ni kati ya
Azam FC watakaoikaribisha Coastal Union kutoka Tanga huku Majimaji
wakiwa wenyeji wa Ndanda FC mjini Songea na Kagera Sugar inayotumia
Uwanja wa Ali Hasan Mwinyi mkoani Tabora watacheza na JKT Ruvu ya
Pwani.
African Sport wataivaa Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini
Tanga, wakati Tanzania Prisons watacheza na Mwadui huku kesho Alhamisi
Toto Africana wakiikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa CCM Kirumba
Mwanza.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment